AV

Kunde: Ladha ya Afrika yasambaa Marekani

Get monthly
e-newsletter

Kunde: Ladha ya Afrika yasambaa Marekani

Akara na é: Tamaduni za mapishi zinazounganisha bara Afrika na Waafrika walio Ughaibuni
Franck Kuwonu
24 December 2019
Black eye peas

Ni mlo maarufu katika sehemu za kusini mwa Marekani, chakula chenye harufu ya kuvutia na chenye jina la kupendeza. Hoppin’ John— kilichoandaliwa kwa kunde na wali, vitunguu vilivyokatwakatwa, nyama ya nguruwe ilivyokatwakatwa na chumvi— mlo usio na kifani.

Hoppin’ John, jambalaya, na feijoada ni baadhi ya vyakula vinavyotokana na mlo wa Afrika Magharibi. Vyakula hivyo vina mseto wa maharagwe, nyama na mboga zinazochanganywa na wali na hivyo ni mlo maaarufu kwa watu wenye asili ya Kiafrika wanaoishi Marekani na kote ulimwenguni.

Kutoka mwambao wa Afrika Magharibi hadi Marekani Kusini na Karibia—kunde imekuwa nembo thabiti ya uhusiano wa kitamaduni ambao bado unaunganisha Afrika na ughaibuni. Keki zilizoandaliwa kwa kunde zilizopondwa na kukaangwa ndani ya mafuta ya nazi huuzwa barabarani kwa majina mengi yanayofanana kwenye mabara tofauti tofauti.

Huku kunde zikiwa sehemu ya liche ya watu wanaoishi India na Myanmar, huwa zinaliwa kwa wingi katika mataifa ya Afrika Magharibi hasa, Benini, Gine, Nijeria and Senegali, pamoja na Karibia, Brazil na Marekani Kusini, ambayo kwa muda mrefu imekuwa na idadi kubwa ya Wamarekani Weusi. Kunde zinasemekana kufikishwa Karibia na Marekani kwa meli za watumwa.

Kangni Alem, mwanariwaya na mwanatamthilia kutoka Togo aliiambia AfrikaUpya kwamba hakuamini alipokutana na wanawake kule Brazil wakiuza é barabarani. Alikuwa amezuru Salvador, mji mkuu wa Bahia, unaojulikana kwa wengi kama “Mji mkuu wa Afrika Magharibi huko Marekani Kuisini,” alipokuwa katika ziara ya kitamaduni.

“Kwa mara ya kwanza nilidhani niko Lomé,” Bw. Alem alisema, sio kwa sababu ya uraia wa watu, lakini kwa sababu “walikuwa wakikaanga keki ya maharagwe hapo nje,” alistaajabu. Alipendezwa sana hivi kwamba baadaye aliandika kuhusu tajriba hiyo katika riwaya yake Les enfants du Brésil (Watoto kutoka Brazil).

Nyama ya masikini

Kunde ni sehemu ya lishe la kila siku la mamilioni ya watu barani Afrika. Huwa zinachemshwa na kuliwa kwa wali au zikakaangwa kwa nyanya na vitunguu na kuliwa kwa mseto wa wali na ndizi za kukaangwa. Pia zinaweza kusagwa na kuwa unga wa uji.

Huku zikijulikana kama Ծéé katika sehemu fulani za Sahel, kunde zimepatiwa jina la majazi la “maharagwe ya muujiza,” au “nyama ya masikini” katika sehemu nyingi Kusini mwa Sahara kwa sababu ya thamani yazo ya lishe na uwezo wa kukua katika hali mbaya ya hewa.

Kulingana na Taasisi ya Kimataifa ya Kilimo cha Kitropiki (IITA), kunde “zina 25% ya protini na pia zina vitamini na madini kadhaa. Hazizuiwi kukua na ukame, hukua vizuri katika aina kadhaa za udongo, na kwa pia hurutubisha udongo ulio na rotuba hafifu mizizi yake ikiachwa ioze.”

Ingawa habari kuhusu matumizi yake duniani na kuhusu mapato yake ya biashara ni chache, Nijeria ndio mzalishaji mkubwa, mwagizaji na mtumizi mkubwa wa kunde ulimwenguni. Utafiti wa mnamo 2016 wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa ulikadiria kuwa matumizi ya kunde ni takribani kilo 18 kwa kila mtu nchini Nijeria, kilo 9 kwa kila mtu nchini Ghana na kilo 1.8 kwa kila mtu nchini Cote d'Ivoire.

Mataifa ya Afrika yalizalisha zaidi ya 96% ya makadirio ya mazao ya tani milioni 5.4 ya kunde mwaka huo, Nijeria pekee ilizalisha 61% ya mgao wa bara na 58% ya mavuno ya dunia kulingana na IITA.

Aina kadhaa za kunde zimezalishwa na IITA kama sehemu ya shughuli za utafiti wa taasisi hii. Baadhi ya aina zina mbegu kubwa na zina uzalishaji wa juu na zinakomaa haraka; nyingine zimeundwa kuwa sugu kwa wadudu. Katika hifadhijini la Taasisi hii kuna mkusanyiko mkubwa wa kunde, ikijumuisha sampuli za kipekee 15,122 kutoka mataifa 88.

Huko Marekani, katika Mkahawa wa Sweet Home Café kwenye Makavazi ya Historia na Mila za Wamarekani weusi jijini Washington, D.C., bango lililoko ukutani linamnukuu Mwanaharaki wa Kilimo na Vyakula vya Marekani Natasha Bowens akisema: “Pamoja na mataifa mengi barani Afrika na athari tata za historia kutoka kusini, tamaduni za chakula za Wamerekani weusi na hadithi zilizomo ni pevu na za kina mno.”

Kitabu cha Bowens kilichochapishwa mnamo 2015, The Color of Food: Stories of Race, Resilience, and Farming kinaangazia umuhimu wa ardhi na tamaduni za chakula katika historia ya utambulisho wa Wamerakani weusi na kuonyesha jinsi baadhi ya vyakula vinavyoliwa leo vina misingi katika asili yao ya Kiafrika.

Ndani ya Makavazi yake na katika mkahawa ulio katika jiji kuu la Marekani na kwenye mwambao wa Brazil, ushawishi sugu wa athari ya Afrika kwenye vyakula vinavyochukuliwa kuwa vya kawaida hauwezi kupingika.