¹ú²úAV

Jumuiya za Kikanda za Afrika zitafaidi wote

Get monthly
e-newsletter

Jumuiya za Kikanda za Afrika zitafaidi wote

— Ibrahim Mayaki ni Afisa Mkuu Mtendaji wa Ushirikiano Mpya wa Maendeleo ya Afrika (NEPAD), ambao kwa sasa unageuka kuwa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Afrika (AUDA)—chombo cha utekelezaji wa Umoja wa Afrika.
Kingsley Ighobor
24 December 2019
Ibrahim Mayaki
Ibrahim Mayaki
Ibrahim Mayaki ni Afisa Mkuu Mtendaji wa Ushirikiano Mpya wa Maendeleo ya Afrika (NEPAD), ambao kwa sasa unageuka kuwa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Afrika (AUDA)—chombo cha utekelezaji wa Umoja wa Afrika.

Ibrahim Mayaki ni Afisa Mkuu Mtendaji wa Ushirikiano Mpya wa Maendeleo ya Afrika (NEPAD), ambao kwa sasa unageuka kuwa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Afrika (AUDA)—chombo cha utekelezaji wa Umoja wa Afrika.

Shirika la AUDA-NEPAD lilibuniwa Niamey, Nijeri, mnamo Julai 2019, wakati wa Baraza la Umoja wa Afrika. Uundaji wake ulikuwa ni matokeo ya mageuzi katika Umoja wa Afrika ulioongozwa na Rais wa Rwanda, Paul Kagame, Mwenyeketi wa zamani wa Umoja wa Afrika.

Katika mahojiano na Kingsley Ighobor wa AfrikaUpya jijini New York Dkt. Mayaki alitoa maelezo zaidi kuhusuÌýÌý wajibu wa AUDA katika ajenda ya maendeleo ya Afrika na kujadili muungano wa kikanda na mpango wa shirika lake la kuunda mamilioni ya ajira. Hapa chini tunatoa muhtasari wa mahojiano hayo:

AfricaUpya: Je, tofauti kubwa kati ya AUDA na NEPAD ni zipi?

Dr. Mayaki: AUDA lina wajibu pana. Linatarajiwa kushughulikia changamoto za utekelezaji kuhusu maamuzi yaliyofanywa na Umoja wa Afrika.

Kwa mfano, sisi sasa ndilo kundi la kiufundi la Umoja wa Afrika na washirika wa maendeleo kama vile Uchina, India, Marekani, G20, Mkutano wa Kimataifa wa Tokyo juu ya Maendeleo ya Afrika (TICAD). Hii ni muhimu sana ili kufuatilia utekelezaji wa makubaliano yaliyoafikiwa na washirika hawa.

AUDA pia litalenga utafutaji wa rasilimali na uunganisho kati ya sekta kadhaa ili kuepuka njia iliyo na wakala wengi, ambayo kama unavyojua ni sehemu muhimu ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs). Kwa mfano, tunapofanya kazi katika kilimo, tunazingatia pia maji, nishati, ardhi, nk.

Sasa kuna mgawanyiko wa kazi kati ya Kamisheni ya UA, Jumuiya za Chumi za Kanda na AUDA katika kutekeleza mfumo mkakati wa UA katika ngazi za kitaifa na kikanda.

Umesisitiza kwamba Jumuiya ya kikanda ina jukumu kubwa katika maendeleo ya Afrika. Je, mara nyingi huwa kuna mvutano kati ya taasisi za kikanda na serikali za kitaifa?

Swali lako ni muhimu kwa sababu jumuiya za kikanda zitapiga hatua tu ikiwa serikali za kitaifa— ambazo zinasimamia taasisi za kikanda — zitatumia maamuzi ya kikanda.

Tunaona serikali za kitaifa zikishinikiza mikakati ya maendeleo ya kikanda. Katika Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kwa mfano, mawaziri wa kilimo hukutana mara kwa mara kujadili mabadiliko ya kilimo katika kanda yao. Jumuiya ya Chumi za Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS) hukutana mara kwa mara kuhusu mkakati wa kawaida wa nishati.

Tatizo linahusu jinsi maamuzi ya kimsingi ya kikanda yanayotokana na mfumo wa bara hutekelezwa na nchi. Hapo wajibu wetu unakuwa muhimu. Tunahitaji kuhakikisha kuwa kuna ushirikiano kati ya mikakati ya kikanda na mipango ya kitaifa.

Eneo huru la biashara Afrika, kwa mfano, ni mpango wa bara. Hadi kufikia Juni mwaka huu, Nijeria na Benin walikuwa hawajaridhia. Je, unahakikishaje serikali za kitaifa zinatekeleza miradi ya UA?

Moja kati ya visababishi muhimu vya mafanikio katika jumuiya ya kikanda ni kumshirikisha kila mmoja. Kama kuna makubaliano—na hilo huchukua muda kujenga —tunaweza kuwa na mikataba madhubuti na hivyo kuanza kufikiria juu ya mpango wa utekelezaji. Kadri unavyopata uungwaji mkono zaidi katika kubuni mradi, ndivyo upinzani unavyokuwa mdogo wakati wa utekelezaji.

Pia, bajeti yetu hupitishwa na nchi wanachama wa UA. Programu hizi zinaonyesha vipaumbele vya nchi wanachama kwa sababu ni pesa zao, kwa hivyo, kwa mfano, ikiwa tuna mpango katika nishati mbadala katika Afrika Mashariki, lazima ipate kipaumbele katika kanda hiyo.

Kwa kuzingatia mwelekeo mpya wa maendeleo wa AUDA-NEPAD, una matumaini gani ya ukuzaji wa kikanda kwenye bara?

AU imepiga hatua kubwa sana, haswa katika eneo huru la biashara. Ilichukua muda kuliunda na kushirikisha kila mtu. Tunajua ustadi wa kiufundi tunaohitaji, na kuna uamuzi wa kisiasa wa kutekeleza makubaliano.

Katika kukosa uhakika duniani kwa sasa, tunahitaji kuimarisha biashara ndani ya masoko yetu ya kikanda; vinginevyo hatutashughulikia changamoto zetu za maendeleo. Utekelezaji hautakuwa rahisi kwa sababu ya viwango vya juu vya ufadhili vinavyohitajika na pia mahitaji ya kuoanisha sera kati ya mataifa, lakini tuko kwenye njia sahihi.

Umetetea pia mbinu ya maendeleo ya kutoka chini kwenda juu. Je, hiyo haipingani na malengo ya mfumo wa kikanda ambao ni wa juu kwenda chini?

La, haiwezi kuwa juu kuenda chini, kwa sababu hakuna mfumo wowote utakaofanya kazi ikiwa hautawezesha jamii za wenyeji.

Kwa mfano, unajua kuwa upatikanaji wa umeme barani Afrika uko chini sana - zaidi ya 60% ya watu wetu wa vijijini hawana umeme. Lakini mazao ya kilimo hayataongezeka ikiwa suala la nishati halijashughulikiwa. Njia bora ya kutatua tatizo la nishati ni kugatua huduma za nishati katika kiwango cha jamii, nishati isimamiwe na jamii za mashinani. Hii ndio ninayoita chini kwenda juu. Unaweza kuwa na mkakati mkubwa, lakini utekelezaji na uvumbuzi, lazima utoke chini.

Ìý"Ukoloni ulikuwa mfumo wa usafirishaji haramu wa fedha," ulisema hivi karibuni kwenye hafla katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa. Je, unamaanisha nini?

Tazama miundombinu yetu ya Afrika ya kabla ya uhuru, na hata mbele ya hapo. Ilikuwa barabara, ilikuwa inaunganisha eneo la migodi na bandari. Kwa hivyo, miradi yote ya miundombinu, isipokuwa katika nchi na mahali ambapo wakoloni walikuwa wakitaka kuishi kwa hakika, miradi mingine yote ya miundombinu ilielekezwa kuelekea usafirishaji, usafirishaji, usafirishaji! Usafirishaji wa madini, usafirishaji wa mazao ya kilimo, na kadhalika.

Miundombinu ya kipindi cha ukoloni bado imesimama barani Afrika, licha ya kuwa imesasishwa. Ni nini kinafaa kufanywa kuihusu?

Hiyo ndio sababu tuliunda Programu ya Maendeleo ya Miundombinu barani Afrika (PIDA). Inabadilisha mitindo hiyo ya miundombinu ya usafirishaji kwa kulenga miradi ya kikanda na barabara za usafirishaji ambazo hurahisisha uchukuzi na maendeleo. Kwa njia hiyo tunaongeza biashara ya ndani ya Afrika.

Ulitangaza mpango wa kuunda ajira milioni 1. Je, utafikiaje hayo?

Mataifa wanachama wa Umoja wa Afrika yalitaka kuwa thabiti sana kuhusu ajenda ya kuunda ajira. Walisema tunapaswa kuwa na lengo linaloweza kupimika ili tuwajibike. Tulisema, "Sawa, wacha tuweke lengo la ajira milioni 1 katika miaka mitatu ijayo." Lakini kama unavyojua serikali haziundi ajira; sekta binafsi huunda ajira, na sekta binafsi barani Afrika inaongozwa na biashara ndogo na za kati (SMEs). Benki ya Maendeleo ya Afrika inatuambia kuwa 60% ya SME zetu zina wafanyikazi wasiopungua 20 na 40% iliyobaki zina wafanyakazi wasiozidi 10. Kwa hivyo, ikiwa tutasaidia SMEs 100,000, tunaweza kufikia ajenda hiyo ya ajira milioni 1.

Je, Afrika inahitaji ajira mpya milioni 1?

Ndio. Kila mwaka tunahitaji kuunda ajira milioni 20. Kwa miaka mitatu ijayo, Afrika inahitaji kuunda ajira milioni 60, lakini tunaweza kulenga ajira milioni 1 kwa sasa. Hata hivyo, tunataka kutumia njia bora kuhusu uundaji wa SME, vituo vya uzalishaji, ulinzi wa mali za kitaalamu, ufadhili wa SME na benki za maendeleo za kitaifa, mazingira mazuri, motisha, na nyingine. Tunataka mazoea haya bora yaweze kurudiwa tena katika nchi zote.

Kwa kuzingatia ukosefu wa ulinganifu wa chumi za Afrika—zilizo na SME zilizojikita katika nchi zilizoendelea zaidi kiuchumi — inaonekana nchi masikini zitafaidika kidogo kutoka kwa mpango huu.

Tunalenga nchi zisizoendelea sana. Pesa tunazopata kutoka Umoja wa Afrika hazijatumika kwa miradi ya Misri, Afrika Kusini au Nijeria. Lengo la Jumuiya ya kikanda ni kuinua nchi zisizoendelea sana, na huu ndio ubora wa Umoja wa Afrika. Jumuiya ya kikanda ina msingi wake kwenye mshikamano, na tunajua kuwa mshikamano sio tu wa maadili. Unao mwelekeo wa kiuchumi unaofaidi kila mtu.