Mnamo 2013, wawakilishi wa mataifa wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) walijumuika katika makao yake makuu huko Addi Ababa, Uhabeshi, ambako Shirika la Umoja wa Afrika (OAU) lilianzishwa mwaka wa 1963, ili kuadhimisha miaka 50 tangu uasisi huo.
Katika sherehe hiyo ya kufana, viongozi waliketi kutafakari na kuyakabili maswali magumu; Tumepiga hatua zipi katika kutimiza malengo yaliyowekwa na AU na tunaposonga mbele, ni ipi ruwaza ya Afrika tunayopendekeza kwa miaka 50 ijayo? Aidha, ni changamoto gani kuu katika kutimiza matamanio ya watu wetu?
Nkosazana Dlamini-Zuma, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, alikuwa ameyazuru mataifa mbalimbali akikusanya maoni kutoka kwa serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali na Waafrika walio nje ya Afrika, kuhusu wanalohisi kuwa suala kuu linalokumba Afrika na ambalo AU inastahili kulikabili.
Wengi walikiri kuwa mizozo imesalia kuwa changamoto kuu inayokabili Afrika. AU pia inaiona mizozo kama moja kati ya vikwazo vikuu katika utekelezwaji wa Ajenda 2063. Ni kweli, kulikuwa na changamoto nyinginezo zinazokabili bara hili, ikiwa ni pamoja na umaskini, ukosefu wa usawa, ukosefu wa nafasi za ajira, mabadiliko ya tabianchi, pesa haramu, ufisadi, na kadhalika, lakini tatizo la mizozo ndilo linaloongoza.
“Kabla ya kuondoka Addis Ababa, viongozi hao wa AU walikubaliana kutorithisha vizazi vijavyo mzigo wa mizozo na kwa sababu hiyo walibuni mradi wa ‘Kuzima Bunduki Barani Afrika kufikia 2020’ kama moja kati ya miradi muhimu ya mipango kabambe ya kimaendeleo ya Ajenda 2063.” Bi. Aïssatou Hayatou, meneja wa mipango wa “Kuzima Bunduki” aliambia AfrikaUpya.
Aliongeza kuwa: “Lengo lilikuwa kupata amani ili kuwezesha maendeleo kote Afrika.”
Mpango huu ulikusudia kuwepo kwa Afrika isiyo na mizozo, kuzuia mauaji ya kimbari, kuleta amani halisi kwa wote na kumaliza vita, mizozo ya vurugu, ukiukaji wa haki za kibanadamu, na majanga ya kibinadamu barani Afrika. Viongozi hao walitumai kuwa bunduki zote zitakuwa zimezimwa kufikia 2020.
Tangu 2014, Afrika imepiga hatua katika kusaka amani na usalama, hasa kwa kuimarisha mifumo na asasi za kushughulikia dharura barani, pamoja na kushirikiana na Umoja wa Mataifa na mashirika mengine nyanjani. Mipango hii imefaulu.
Katika miongo miwili iliyopita, bunduki zimezimwa katika maeneo yaliyokuwa hatari awali kama vile Angola, Côte d’Ivoire, Liberia na Sierra Leone. Hatua kubwa zimepigwa katika mataifa yenye hali ngumu kama Somalia na Sudan. Haya ni kwa mujibu wa Institute for Security Studies (ISS), taasisi yenye makao yake makuu jijini Addis Ababa. Mipango ya kukuza amani barani pia imechangia kuzuia kuchipuka ghafla kwa mizozo.
Hata hivyo, mapigano bado yanashuhudiwa nchini Libya, Sudan Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), na katika Bonde la Ziwa Chad, ambalo linajumuisha Chad na maeneo fulani ya Nijeria, Nijer na Kameroon. Siasa kali za vurugu katika Sahel na katika Upembe na Mashariki ya Afrika ni changamoto kubwa pia.
Kuna tishio kutoka kwa ugaidi na uhalifu unaovuka mipaka ya kitaifa barani pia. Mizozo ya kijamii kati ya wachungaji na wakulima kwa sababu ya maji na nyasi; uhalifu na vurugu mijini na tamaduni za vurugu kama wizi wa mifugo, ni tishio pia kwa kuwa bunduki ndizo hutumiwa zaidi ikilinganishwa na silaha za kitamaduni zisizo hatari.
Uchunguzi wa 2017 wa Oxfam, The Human Cost of Uncontrolled Arms in Africa unakadiria kwamba watu wapatao 500,000 hufa kila mwaka na mamilioni hulazimika kuhama kwao au kudhulumiwa kwa sababu ya vurugu kwa silaha za kivita na mizozo.
Nani wenye bunduki barani Afrika?
Kwa mujibu wa utafiti wa Small Arms Survey (SAS), 80% ya silaha ndogondogo barani Afrika zimo mikononi mwa raia. SAS ni kituo kinachojitegemea cha utafiti kilichoko Geneva na ambacho huzalisha maarifa ya ushahidi, horomo na yenye umuhimu kwa sera na uchanganuzi kuhusu bunduki ndogondogo pamoja na masuala ya vurugu kwa silaha. Utafiti huu huwa na manufaa kwa serikali, watunga sera, watafiti na mashirika yasiyo ya kiserikali.
Kulingana na utafiti wa SAS na Umoja wa Afrika wa 2019 uitwao Weapons Compass: Mapping Illicit Small Arms Flows in Africa, raia na vikundi vya waasi na wanamgambo, wanamiliki zaidi ya bunduki na silaha ndogondogo milioni 40, ilhali vikundi vya kiserikali vinamiliki chini ya milioni 11.
Bunduki hizi zinatoka wapi?
Nyingi ya silaha zilizomo Afrika zinaagizwa kutoka nje. Matumizi rasmi ya kijeshi barani Afrika yalikuwa takriban dola bilioni 40.2 mwaka wa 2018, huku Afrika Kaskazini ikitumia dola bilioni 22.2 nayo mataifa chini ya Jangwa la Sahara yakitumia dola bilioni 18.8, kulingana na ISS.
Kati ya 2014 na 2018 mataifa yaliyouzia Afrika bunduki nyingi zaidi yalikuwa Urusi, Uchina, Ukraine, Ujerumani na Ufaransa. Kwa mujibu wa Stockholm International AV Research Institute (SIPRI), taasisi ya kimataifa huru inayochunguza mizozo, vifaa vya kijeshi, udhibiti wa silaha na kutoa silaha mikononi mwa raia, mataifa yaliyopokea silaha kwa wingi yalikuwa Misri, Algeria na Morocco. Hifadhidata ya Uhamishaji wa silaha ya SIPRI hutoa habari kuhusu uhamishaji wa kimataifa wa silaha kuu (pamajo na uuzaji, zawadi na utengenezwaji kisheria) kwa mataifa, mashirika ya kimataifa na vikundi visivyo vya serikali.
Mataifa ishirini na mawili ya Afrika pia huunda bunduki ndogondogo na silaha nyepesi za aina mbalimbali. Uundaji wa silaha wa haramu nyumbani pia umeenea barani. Silaha hizo husemwa kuendeleza uhalifu katika mataifa kadhaa.
Japo mataifa ya Afrika yanaweza kudhibiti ununuzi wa bunduki halali, ni vigumu kufuatilia ulanguzi wa silaha haramu na maenezi yake barani. Mipaka inayovuja na fuo ndefu aidha huwasaidia walanguzi kupitisha bunduki ndogondogo katika mataifa. Kuna wasiwasi pia kuhusu namna hazina ya bunduki za kitaifa zinavyosimamiwa kuhakikisha kwamba silaha hizo haziishii katika mikono haramu.
Bunduki zipi?
“Bunduki ndizo silaha maarufu barani Afrika. Zinasababisha vifo vingi zaidi kuliko mabomu, gruneti na mabomu ya kutega. Bunduki aina ya AK-47 imesalia kuwa silaha hatari mno ya maangamizi barani Afrika kwa sasa,” anasema Bi. Hayatou, huku akiongeza kwamba sehemu kubwa ya siaha ziagizwazo kihalali Afrika huelekezwa kwingine kiharamu kutokana na ufisadi. Aghalabu hazina za serikali huvamiwa au vikosi vya kijeshi au maafisa wa polisi huuliwa kwa manufaa ya silaha zao. Silaha nyingi kutoka Libya, ambazo zilimilikiwa na Muammar Gaddafi na ambazo sasa zimeishia Sahel zinatia wasiwasi sana. Nyingi kati ya silaha hizi sasa zimo mikononi mwa waasi waliojitenga kaskazini mwa Mali.