AV

Mwezi wa Msamaha wa Afrika: Mwito wa kuzisalimisha bunduki haramu Septemba hii

Get monthly
e-newsletter

Mwezi wa Msamaha wa Afrika: Mwito wa kuzisalimisha bunduki haramu Septemba hii

— Mr. Ivor Richard Fung, Deputy Chief of theConventional Arms Branch, UN Office for Disarmament Affairs(UNODA)
Zipporah Musau
Afrika Upya: 
29 August 2020
Armed Turkana herdsmen guard their livestock at a watering hole at Oropoyi in Kenya
AFP via Getty Images/Tony Karumba
Wachungaji wa Kitrukana wachunga mifugo wao karibu na kisima cha maji katika eneo la Oropoyi, wilaya ya kaskazini magharibi ya Turkana, nchini Kenya. Uvamizi kwa silaha na wizi wa ng’ombe kwa sababu ya maji na maeneo ya malisho ni maarufu mno miongoni mwa jamii katika maeneo fulani ya Uganda, Kenya, Sudan na Uhabeshi.

Septemba ndio mwezi uliotengwa na Umoja wa Afrika ambapo raia walio na silaha haramu wanahimizwa kuzisalimisha kwa serikali bila kutiwa mbaroni wala kushtakiwa. Bwana Ivor Richard Fung, Naibu Mkuuwa Tawi la Mkataba kuhusu Bunduki la Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Masuala ya Usalimishwaji wa Silaha (UNODA), aliongea naZipporah Musauwa AfrikaUpya kuhusu umuhimu wawa Mwezi wa Msamaha na shughuli zilizopangwa. Kuna madondoo hapa:

Ivor FUNG
Tunataka kuwasilisha ujumbe kwamba hatukulaumi wala kukukashifu wewe kwa kuwa na silaha kinyume cha sheria. Hii ndiyo sababu unaitwa mpango wa msamaha: hakuna lawama, hakuna mashtaka, hakuna adhabu. Ni fursa ya kuwa na usalama mkuu tu. Mpango huu wa msamaha ni fursa kwa watu kujitokeza, kuongeza idadi ya silaha zilizosajiliwa. Kwa hivyo, kama huwezi kuisajili, isalimishe tu – huu ndio ujumbe
Bwana. Ivor Richard Fung
Naibu Mkuu wa Tawi la Mkataba kuhusu Bunduki, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Masuala ya Usalimishwaji wa Silaha (UNODA)

Mwezi wa Msamaha wa Afrika unahusu nini, utatekelezwa lini na utahusisha kina nani?

Mwezi wa Msamaha wa Afrika ni mpango wa kukamilishana wa ruwaza muhimu ya ‘Kuzinyamazisha Bunduki’ ya Umoja wa Afrika inayokusudia kuimaliza mizozo kufikia 2020 na unalenga kuwahusisha raia katika kuzisaidia serikali kupunguza usambazaji haramu wa silaha katika bara hii.

Mwaka wa 2017, kupitia kwa Uamuzi 645 (XX1X), Baraza Kuu la Umoja wa Afrika liliutangaza mwezi wa Septemba wa kila mwaka kufikia 2020 kama “Mwezi wa Msamaha wa Afrika” kwa usalimishaji na ukusanywaji wa bunduki ndogondogo haramu na silaha nyepesinyepesi kulingana na miongozo bora ya Kiafrika na kimataifa, kwa njia yenye mshikamano na endelevu.

Shughuli nyingi kuhusu udhibiti wa silaha ndogondogo hivi sasa zinalenga silaha zinazomilikiwa na wanajeshi na polisi. Hata hivyo, kimataifa asilimia 85 ya bunduki ndogondogo na silaha nyepesinyepesi (SALW) ziko mikononi mwa raia. Katika bara Afrika, raia wanamiliki zaidi ya milioni 40 ya silaha ndogondogo, na raia wachache sana wanaomiliki wana liseni.

Inakadiriwa kwamba takriban bunduki ndogondogo na silaha nyepesinyepesi milioni 40 zinasambazwa kiharamu barani Afrika, na takriban 85 yazo hazijasajiliwa. Yaani hakuna anayejua ni nani aliye na silaha hizi, hakuna aliye na liseni.

Mwezi wa Msamaha unakusudia kuwashirikisha raia katika kuzisaidia serikali kupunguza ueneaji haramu wa silaha katika bara hili.

“Mwezi wa Msamaha” unachukuliwa kama mchango kwa Mkakati Mkuu wa Hatua Halisi za Kuzinyamazisha Bunduki kufikia 2020 wa Umoja wa Afrika, unaojulikana pia kama “Mkakati wa Lusaka”, ambao ni mpango muhimu wa Muungano wa Umoja wa Afrika ‘kuongeza kasi” ya kutimiza ahadi ya AU.

Ni kwa nini unasherehekewa mwezi wa Septemba?

Septemba ni mwezi wa kitaashira kwa kuwa kila mwaka Siku ya Kimataifa ya Amani inasherehekewa duniani kote tarehe 21 Septemba. Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitangaza siku hii kama siku iliyotengwa kuimarisha kanuni za amani, kwa kuzingatia saa 24 bila vurugu pamoja na kusitisha vita.

Mnalenga kupata silaha za aina gani?

Tunalenga kukusanya bunduki ndogondogo na silaha nyepesinyepesi; haswa kundi la bunduki ndondogo. Kundi hili linajumuisha bunduki za mkononi (bastola, bombomu na mzinga), bunduki mrao, bunduki za masafa mafupi, bunduki kubwa (bunduki za kivita, bunduki za mdungizi, bunduki za mitutu mifupi, na kadhalika) pamoja na risasi zao. Ni vyema kutambua kwamba baaadhi ya bunduki hizi zimeigwa katika mataifa mengi ya Afrika ambako ufundi wa kuziunda umeimarika sana kiteknolojia.

Wajibu wa Umoja wa Mataifa ni upi katika mpango huu?

Wajibu ambao Umoja wa Mataifa unatekeleza kuhusu Mwezi wa Msamaha wa Septemba, haswa kwa toleo la 2020, ni kuzindua mradi katika mataifa saba ya Afrika – Burkina Faso, Cameroon, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Cote d'Ivoire, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Uhabeshi na Kenya.

Ni vigezo vipi vilivyotumiwa kuyachagua mataifa saba?

Kwanza, Muungano wa Umoja wa Afrika umefadhili shughuli za Mwezi wa Msamaaha wa Septemba katika miaka iliyotangulia na umenadumisha mawasiliano na mataifa yanayotaka kuushiriki mpango huu.

Kigezo kingine kilikuwa kushiriki kwa mataifa haya katika Mpango wa Hatua dhidi ya Bunduki Ndogondogo na Silaha Nyepesinyepesi wa Umoja wa Mataifa, pamoja na utekelezwaji wa vyombo vya kikanda vinavyohusiana na udhibiti usambazaji haramu wa silaha; udhibiti wa bunduki ndogondogo na silaha nyepesinyepesi.

Bila shaka, tungependa kuwa na mataifa mengi zaidi yanayoshiriki, ila ufadhili tulio nao uliweza kufadhili idadi tuliyo nayo tu kwa sasa.

Ni shughuli zipi mlizoratibu Mwezi wa Msamaha wa Septemba katika hayo mataifa saba?

Tutatekeleza shughuli nne, kulingana na sheria na maelekezo ya kitaifa na ahadi za mataifa hayo kuzingatia mikataba ya kimataifa, kikanda na kieneo kuhusu bunduki ndogondogo.

Ivor Fung, Deputy Chief of UNODA’s Conventional Arms Branch
Bwana. Ivor Richard Fung.
Picha: Martin Desbiolles

Kwa ushirikiano, UNODA pamoja na AU, washirika watekelezaji wakiwemo Kituo cha Kikanda kuhusu Bunduki Ndogondogo (RECSA), na wawakilishi wa tume za kitaifa na vitovu muhimu vya kitaifa kuhusu Udhibiti wa Bunduki Ndogondogo (kama vituo vilivyotengwa kitaifa kwa mradi huu) walianzisha hatua za kitaifa katika kiwango cha nchi na mipango ya mawasiliano kwa manufa ya mradi huu.

Ya kwanza ni kampeni kuu ya kuhamasisha na kuwazindua raia wa Afrika kuhusu hatari za ulanguzi haramu wa silaha ndogondogo, na pia kuwashirikisha, haswa watu walio na silaha kinyume cha sheria, kujitokeza na kuzisalimisha.

Serikali za mataifa haya yanayoshiriki, kama serikali za mataifa mengine yanayounga mkono uamuzi wa AU, zimeahidi kutomshtaki yeyote aliye na silaha kwa kinyume cha sheria mradi ajitokeze na kuzisalimisha mwezi huu wa Septemba. Hii ndiyo sababu unaitwa ‘Mwezi wa Msamaha’.

Shughuli ya pili ni kuzikusanya silaha haramu, ilhali ya tatu ni kuziharibu silaha ambazo zitakuwa zimekusanywa.

Shughuli ya nne ni kuandaa warsha za kutoa mafunzo kuhusu ushirikiano wa polisi na raia katika kuhakikisha usalama. Hii ni kwa sababu ya uelewa kwamba mtu anapoamua kubeba silaha huwa ni kwa haja ya kujihakikishia usalama. Maadamu mpango huu hauna malipo ya kifedha kwa watakaozisalimisha silaha hizo, wafadhili wa mradi – Muungano wa Umoja wa Afrika na wafadhili - waliamua kuwa na namna fulani ya kuipongeza jamii husika. Hili lina maana kwamba ushirikiano kati ya polisi na raia utaimarishwa, na jamii zitakuwa na wajibu wa kutekeleza.

Je, kuna shughuli zinazowalenga vijana na watahusishwa vipi?

Ndio, katika muktadha wa shughuli ya kwanza, ambayo ni ya uhamasishaji katika kiwango kipana, uzinduzi, na shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na maonyesho ya muziki katika vyombo vya habari. Kutakuweko pia na shindano la vijana kutunga kaulimbiu za kitaifa za mpango huo, na pia wanahimizwa kuandika taarifa kuhusu shughuli hizi.

Vijana ndio wengi katika jumla ya idadi ya watu katika bara Afrika, na wana wajibu mkuu katika kuutekeleza mpango huu. Watahusika katika shughuli zote ikiwa ni pamoja na masuala yanayohusiana na, kwa mfano, kuziharibu silaha hizo.

Vijana wanastahili pia kuhusika katika kusaka suluhisho. Tunataka haswa kuwahusisha, hususan katika mkabala wa kudhibiti silaha na kuzitoa mikononi mwa raia na kusaidia kuanzisha hali ya kuwajibika katika kudhibiti bunduki na amani.

Wafadhili wa Mwezi wa Msamaha waa Afrika
  • Serikali ya Ujerumani
  • Serikali ya Japan

Kutafuta msaada wao katika shughuli za kuziharibu silaha kutachangia katika mchakato wa kuondoa mtazamo hasi kuhusu umuhimu wa bunduki katika jamii ya Afrika inayoibuka. Huu ni ujumbe mzito wa kitamaduni.

Je, watu wanaotaka kushiriki wanaweza kuhusika vipi?

Ni rahisi mno. Kupitia kwa uhamasishaji katika vyombo vya habari, na kaulimbiu ambazo tutakuwa tukizipeperusha, watu watajua ni shughuli zipi zitakuwa katika jamii zao. Hata pale ambapo hakutakuwa na shughuli zionekanazo za mradi huu, redio, runinga, magazeti na matangazo katika mitandao ya kijamii yatamwezesha kila mmoja kusikia na kuchukua hatua dhidi umiliki haramu wa bunduki katika mazingira au jamii zao.

Shughuli zaweza kuwa vipindi vya redio, mijadala katika vikundi katika mezaduara, mashindano ya muziki na kadhalika kwa nia ya kuwapa watu motisha, haswa mashirika ya kiraia, jamii za mashinani, vikundi vya kidini, makanisa, viongozi wa kitamaduni. Tunawazia pia kushirikiana na machifu wa kitamaduni ili kuona jinsi wanavyoweza kuwahamasisha watu kwa lugha asilia. Kila mtu ashiriki katika mpango huu.

Tunazialika jamii hizi zote kuzimiliki shughuli hizi kulingana na uhalisia wao wa kijamii/kitaifa.

Wanawake wanaweza kutekeleza wajibu gani katika shughuli hii?

Wanawake wana wajibu mkubwa wa kutekeleza. Tunatarajia vikundi vya wanawake katika mataifa yanayoshiriki kuhusika katika shughuli za utunzi wa sheria ambao kila taifa linastahili kufanya.

Ushiriki wa pili wa wanawake utakuwa katika shughuli za kiasasii na kiutekelezwaji kuhusu bunduki ndogondogo na silaha nyepesinyepesi kama ukusanyaji wa silaha hizo. Wanawake wanaweza kuhusishwa kupitia kwa uanachama katika asasi ya kiushirikishi ya kitaifa, kama kitovu kikuu cha kitaifa au tume ya kitaifa, kutegemea taifa. Wanawake wanastahili kuyatekeleza majukumu rasmi katika asasi hizi.

Aidha, kuna majukumu mengine yasiyo rasmi ambayo wanawake wanaweza kutekeleza. Wanaweza kuhamasisha katika maeneo yao ya mashambani, katika miji, majadiliano katika mezaduara, hata katika lugha zao asilia ili kuwasilisha ujumbe, na pia namna wanavyoliona suala hili kama wanawake, kutokana na tajriba zao za kibinafsi.

Wanaume ndio hujeruhiwa pakubwa risasi inapolipuliwa. Lakini wanawake, haswa katika jamii yetu ya Afrika, wanaathiriwa zaidi na kwa muda mrefu. Itakuwa vizuri wajitokeze na kusimulia visa vyao. Hii pia itakuwa fursa yao kuonyesha mambo wayafanyayo katika jamii zao.

Mwezi wa Msamaha wa Afrika umekuwa ukisherehekewa tangu 2017. Je, kuna ufanisi wowote kufikia sasa?

Ndio, kumekuwa na ufanisi. Kwa mfano, mwaka wa 2017 mpango huu ulisherehekewa katika mataifa ya Burkina Faso, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Madagaska, Sudan na Zambia. Ujumbe umeenezwa kwingi mno katika mataifa haya ili kuwahamasisha watu kuhusu suala la bunduki ndogondogo.

Pili, silaha zimekusanywa katika mataifa haya. Watu walijitokeza na kuzisalimisha silaha zao, na silaha hizo ziliharibiwa.

Serikali pia zimepiga hatua mbele na kuboresha sheria. Hata hivyo, haitoshi kuwa na sheria nzuri tu, unastahili kuitekeleza. Kwa hivyo, ni awamu ya utekelezwaji, haswa wajibu wa wale maafisa wanaotekeleza sheria, ambayo ni muhimu zaidi na ndiyo tunayotilia mkazo.

ni mradi muhimu zaidi wa Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika.



Lengo:Kuvimaliza vita, mizozo ya wenyewe kwa wenyewe, dhuluma za kijinsia, mizozo ya vurugu na kuzuia mauaji ya kimbari barani Afrika kufikia 2020.

Asili: Muungano wa Umoja wa Afrika

Mambo zaidi mazuri yamekuwa yakifanyika katika bara hili.

Kwa mfano, kuanzia Disemba 2019 taifa la Afrika Kusini limezindua msamaha kwa walio na bunduki ndogondogo na silaha nyepesinyepesi kwa miezi sita na kukusanya zaidi ya silaha 46,000. Hili bila shaka limepata msukumo kutoka kwa mwezi wa msamaha.

Haya ndiyo mambo chanya ambayo tunastahili kuyaonyesha na kuyawekea msukumo. Yanaweza kuigwa na mataifa mengine mengi, ikiwa ni pamoja na yale yanayoibuka kutoka kwa mizozo, yale yanayoshuhudia mizozo, na hata yale yanayoishi katika amani ya kiasi fulani. Hii ni kwa sababu hata kama kuna mahali palipo na amani ya kiasi fulani, bado kuna uhalifu, kuna vitendo vya uhalifu vilivyopangwa vinavyovuka mipaka ya mataifa.

Ni changamoto zipi zinazojitokeza katika kuzikusanya hizi silaha haramu?

Changamoto ya kwanza ni kwamba kila mara kuna ile hali ya wale wanaozimiliki silaha hizi kutotaka kujitokeza. Na hii ndiyo sababu tunatilia mkazo uzito wa jumbe zinazostahili kuwasilishwa kwa raia katika Mwezi huu wa Msamaha.

Tunataka kuwasilisha ujumbe kwamba hatukulaumu wala kukukashifu wewe kwa kuwa na silaha kinyume cha sheria. Hii ndiyo sababu unaitwa mpango wa msamaha: hakuna kulaumu, hakuna kukushtaki, hakuna mashtaka, hakuna adhabu. Ni fursa ya kuwa na usalama mkuu tu.

Mpango huu wa msamaha ni fursa haswa kwa watu kujitokeza, kuongeza idadi ya silaha zilizosajiliwa. Kwa hivyo, kama huwezi kuisajili silaha yako, isalimishe tu – huu ndio ujumbe.

Tulikuwa tumejumuisha pia uwezekano wa ‘kipindi cha msamaha’ ambapo wale walio na silaha kinyume cha sheria na kwa sababu moja au nyingine hawawezi kuuhalalisha umiliki huo, wanaweza kwenda tu kwa maafisa wa usalama na kuzisalimisha bunduki hizo hata baada ya kipindi cha mradi huu.

Changamoto nyingine ni kwamba, hata tunapowahimiza raia kuzisalimisha silaha hizi, jambo zuri kila mara ni kwamba silaha hizo zinastahili kuharibiwa. Hata hivyo baadhi ya serikali huamua kuziharibu kwa njia tunayoiita ya kiubaguzi: kutupa silaha zisizoweza kukarabatiwa na kuzihifadhi zile zilizo katika hali nzuri kwa manufaa ya maghala ya kitaifa.

Hata hivyo, tunahimizwa na hali kwamba mataifa mengi yameanza shughuli ya kuziharibu silaha hizo. Utakumbuka mpango wa Karamojong nchini Uganda, ambao ni miongoni mwa mipango inayonukuliwa zaidi. Kulikuwa na mwingine katika Kongo Brazzaville, mwingine nchini Mali, Nijeri na mipango mingine miaka ya 1990 na ya 2000.

Labda changamoto inayokatisha tamaa zaidi ni uhalisi kwamba silaha hizi mara nyingi huingizwa barani kutoka nje, na wakati mwingine zinatumiwa upya kutoka eneo moja la mzozo hadi jingine.

Ujumbe wako wa mwisho ni upi?

Ujumbe wangu unazilenga serikali za Afrika, vijana na wanawake:

Kwa serikali hizi: Zimeanzisha mpango muhimu ajabu wa ‘Kuzinyamazisha Bunduki’. Muhimu ajabu kwa kuwa ni kudhihirisha nia ya kisiasa kuimaliza mizozo katika bara hili. Ni changamoto inayokatisha tamaa, ila inayostahili kukabiliwa, na shabaha yenye msukumo: Afrika isiyo na mizozo.

Hili pia linahitaji kuweka mipango ambayo inalenga vyanzo haswa vya mizozo hii.

Mipango bora ya utawala ndio njia nzuri ya kupunguza mizozo kwa kiwango kikubwa. Hili litakwaza matumizi ya silaha. Hii itakuwa njia bora kuzinyamazisha bunduki barani Afrika.

Ujumbe wangu kwa vijana wa bara Afrika: Wana wajibu mkubwa wa kutekeleza katika mpango huu. Ni wao, kwa kuwa mara nyingi wao ndio kikosi cha mbele katika vita hivi kwa manufaa yao kuendelea kuishi, kwa manufaa ya maisha yao, kwa maisha yao ya usoni, na kadhalika. Katika kufanya hivyo, wakati mwingine wanachukua mkondo mbaya, mkondo wa mizozo. Bunduki hazisuluhishi tatizo, kuna njia bora za kupigania kilicho chako. Mashauriano, bidii na subira ndio suluhisho.

Ujumbe wangu kwa wanawake, ninataka kusema kwamba tunawaheshimu kwa wajibu muhimu ambao mmekuwa mkitekeleza katika nyakati ngumu, na wakati wapendwa wenu wanajeruhiwa kwa bunduki. Mpango huu ni fursa kwenu pia kushiriki katika kulimaliza baa hili la umiliki usiodhibitiwa wa bunduki. Saidieni na mziwache sauti zenu zisikike.

Sisi, kama Umoja wa Mataifa, tuko tu hapa kuzisaidia serikali katika kufanya yaliyo mema. Na mpango huu ni wao, wameustawisha kulingana na uhalisi wa kitaifa na uwezo wao. Sisi tunatoa msaada unaohitajika wa kiufundi tu.