Huku akisimama kando ya aliyekuwa Rais wa Marekani Barack Obama katika White House, Haben Girma, alionekana kuhitimisha kwa maneno yafuatayo lengo na shauku yake kuu maishani: ziteteeni haki za walemavu.
Ilikuwa ni siku moja yenye joto mnamo mwezi wa Julai 2015 Marekani iliposherehekea kumbukumbu ya 25 ya sheria Americans with Disabilities Act (ADA), sheria iliyoharamisha ubaguzi wowote kwa misingi ya ulemavu na, miongoni mwa mengine, kushurutisha kuwekwa vifanikishi vya kutembea katika maeneo ya umma, ikiwa ni pamoja na mifumo ya uchukuzi wa umma.
“Nikiwa Mmarekani mwenye urithi wa Eritrea na Uhabeshi, mababu zangu wananielekeza kuwa mimi,” ndivyo Bi. Girma alivyojitambulisha katika mazungumzo na Afrika Upya, mapema mwezi huu, karibu miaka sita baada ya sherehe hiyo katika White House.
“Mimi ndiye mtu wa kwanza aliye kipofu na kiziwi kufuzu kutoka Harvard Law School,” alisema “na watu wanadhani kwamba ulemavu wangu ulikuwa changamoto kwangu.”
Alisema: “changamoto kubwa ni ubaguzi dhidi ya walemavu, sio ulemavu wangu.” Kisha akauliza ghafla: “je, unafahamu kuhusu ubaguzi dhidi ya walemavu?”
Dhana ‘ubaguzi dhidi ya walemavu’ ni mpya kwa watu wengi’, asema, na “hilo ni sawa.” Na aliirejelea mara kadhaa katika mazungumzo kwa nia ya kusisitiza.
“Ubaguzi dhidi ya walemavu,” alifafanua “ni unyanyasaji ulioratibiwa dhidi ya walemavu, matendo na imani zinawaona kama duni wakilinganishwa na watu wengine.”
“Uwezo wa kuona haustahili kuwa hitaji”
Je, ubaguzi wa walemavu waweza kujumuisha ukosefu wa juhudi za haki kwa usawa, fursa sawa na haki ya kutembea kwa walemavu?
“Hilo ni sahihi,” Bi. Girma alisema: “Kuna mifano ya ubaguzi wa walemavu inayotuzunguka kote, ila ni vigumu kutambua kwa kuwa inaonekana ya kawaida.”
Na ili kuthibitisha hoja yake, alitoa mfano mmoja kati ya mingi mbayo ameishuhudia kwa miaka mingi.
Kwa mfano, alipotaka kuchangia shirika moja la kimataifa linaloshughulika na wakimbizi, hakuweza kufanya hivyo kivyke kwa kuwa tovuti husika haikufanya kazi na Voice Over, mulishi moja maarufu inayotumiwa na vipofu kusoma. Hatimaye, aliishia kumtegemea mtu mwenye uwezo wa kuona ili kutumia tovuti hiyo.
“Uwezo wa kuona haustahili kuwa hitaji la kutumia kurasa za tovuti,” alisema. “Huenda hicho kilikuwa kikwazo cha ajali kwa wafadhili vipofu, lakini ubaguzi wa ajali bado ni ubaguzi dhidi ya walemavu.”
Ubaguzi
Tafiti zimeonyesha kwamba ubanguzi wa walemavu umeenea. Unaweza kuwa ukosefu wa uwezo wa kutembea au ukosefu wa viwezeshaji katika mifumo ya usafiri wa umma, miundo ya majengo au hata mitazamo ya makusudi. Inaweza pia kuwa katika misemo iliyozagaa katika lugha.
Kwa mfano, lugha ulimwenguni kote zimejaa misemo maridadi na matusi yanayoelekea kulinganisha ulemavu na kitu hasi.
‘Kiwete’, ‘mwenye akili taahira’, ‘fall on deaf ears’, ‘make a dumb choice’, ‘turning a blind eye’ na kadhalika ni baadhi tu ya misemo inayotumiwa na watu kuwasilisha hoja zao, mara nyingi bila kujua athari, uchungu na dhuluma zilizofumbwa ndani yake.
Hadhi ya walemavu haijaheshimiwa kila mara, na hawajapewa haki sawa na fursa sawa.
Mwezi Mei 2008 ulimwengu ulipokubali UN Convention on the Rights of Persons with Disabilities and its Optional Protocol, mkataba wa kina wa haki za kibinadamu wa karne ya 21, uliendeleza mabadiliko ya ulimwengu katika mitazamo na namna ya kushughulikia masuala ya walemavu yaliyoanzia katika mataifa kivyao kama Marekani.
Haya yalikuwa matokeo ya miongo mingi ya utetezi kutoka kwa walemavu ili kuhakikisha kwamba haki zao za uraia za kutobaguliwa na usawa zinatambuliwa na kulindwa.
Mazungumzo hayo yaliyakinisha kwamba walemavu wana haki sawa na binadamu wengine wote na wanastahili kuzifurahia haki hizo.
Ubunifu
Mwaka mmoja baada ya sherehe hiyo katika White House, Bi. Girma alielezea mkusanyiko wa waboresha programu wa kimataifa kwamba ubunifu wa kiteknelojia unaweza kusaidia kuondoa vizingiti.
“Kama huwezi kukifanya kitu kwa njia moja, ni fursa ya kuunda kitu kipya. Mwalimu kipofu hakuweza kusoma kwa macho yake, kwa hivyo aliuunda mfumo wa kusoma kwa kutumia vidole vyake. Mfumo huo uliitwa jina lake, Braille.”
Miaka mingi baadaye, Bi. Girma aliuboresha mfumo huo wa Braille hata zaidi kwa kuunda mfumo wa mawasiliano wa text-to-braille.
“Niliunganisha tarakilishi ya breli na kicharazio cha nje ili watu waniandikie, na maneno yao yangejitokeza ghafla katika breli. Hili linaniwezesha kusoma wanachokisema, kisha ninajibu kwa sauti au lugha ya ishara au tarakilishi, kutegemea anachokihitaji mtu,” alisema.
Kwa miongo iliyopita, kadri maendeleo katika teknolojia yalivyowawezesha watu kuwasiliana, ndivyo ilivyowezesha mawasiliano kwa watu wengi. Na “programu zinapoundwa kwa kuzingatia uwezo wa kutumiwa, walemavu kama mimi, wanaweza kuzitumia na wanaweza kuungana na kushiriki maarifa na watu wengine,” aliukumbusha mkusanyiko wa waboresha programu.
Kama mwanaharakati, mtetezi wa haki za walemavu na wakili, utetezi na chaguzi za kitaalam za Bi Girma zimeelekezwa na tajriba zake za kila siku.
Ubunifu wa kiteknolojia, ikiwa ni pamoja na wa kidijitali, ni silaha muhimu katika kuendeleza hali ya kutembea, ilhali, katika jamii ambazo hazina maendeleo makubwa ya kiteknolojia, ubunifu wa kidijitali, huku ukitambuliwa kimataifa kama ulio muhimu, unaweza kuchukua muda mrefu kabla ya kupata ushawishi.
“Tatizo sio teknolojia, tatizo ni ubaguzi dhidi ya walemavu,” alijibu. Ubaguzi dhidi ya ulemavu unaathiri elimu, huduma ya afya, na kila sekta ya jamii.”
Kwa hivyo, kukabiliana na ubaguzi dhidi ya walemavu ili kuondoa vizingiti vya kijamii ni vita vya kila mara kwa Bi. Girma. Kama Mmarekani mwenye urithi wa Eritrea na Uhabeshi, “Mababu zangu wananielekeza kwamba niwe mimi,” na “kupinga ubaguzi wa rangi, wa kijinsia, na ubaguzi dhidi ya walemavu kila mara pia kunanielekeza kuwa mimi,” aliongezea.
“Na iwapo watu watahisi kuwa na msukumo,” alitaja, “mbona wasikichukue kizingiti kimoja katika jamii na wajitolee kufanya kazi ya kukiondoa kizingiti hicho?”
Zaidi ya yote, “ni matumaini yangu,” aliongezea, kwamba “watu wengi zaidi watapata msukumo wa kuuangamiza ubaguzi dhidi ya walemavu.”