AV

Zebaki kusalia historia kwenye uchimbaji dhahabu

Get monthly
e-newsletter

Zebaki kusalia historia kwenye uchimbaji dhahabu

UN News
By: 
Wachimbaji wadogo wa dhahabu wakichejua dhahabu kwa kutumia zebaki hali ambayo si tu inahatarisha afya zao bali pia mazingira. Picha: GEF
Picha: GEF. Wachimbaji wadogo wa dhahabu wakichejua dhahabu kwa kutumia zebaki hali ambayo si tu inahatarisha afya zao bali pia mazingira.
Picha: GEF. Wachimbaji wadogo wa dhahabu wakichejua dhahabu kwa kutumia zebaki hali ambayo si tu inahatarisha afya zao bali pia mazingira.

Huko mjini London, nchini Uingereza hii leo kumezinduliwa mradi wa thamani ya dola milioni 180 wenye lengo la kufanyia marekebisho sekta ya uchimbaji mdogo wa madini ya dhahabu ili kuepusha matumizi ya zebaki yanayohatarisha afya ya binadamu na mazingira.

Ukitekelezwa na fuko la uwezeshaji wa uhifadhi wa mazingira, GEF kwa ushirikiano na shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa, UNE, mradi huo utawezesha wachimbaji wadogo na wakati wa dhahabu kupata mbinu za kisasa za kuchejua dhahabu bila kutumia zebaki ambapo pia GEF itashirikiana na serikali kurasimisha sekta hiyo, kusongesha haki za wachimbaji wadogo na kuwawezesha kupata masoko.

Nchi nufaika ni 8 na ambazo ni Burkina Faso, Colombia, Guyana, Indonesia, Kenya, Mongolia, Ufilipino na Peru.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa mradi huo wa miaka mitano, Mkurugenzi miradi wa GEF Gustavo Fonseca amesema kuwa watu wengi wanatumia dhahabu kuanzia kwenye simu za kisasa, vito vya thamani ikiwemo pete za ndoa lakini gharama yake halisi kwa uhai wa binadamu inasalia kuwa jinamizi.

“Kwa mantiki hiyo, kuanzisha uchimbaji mdogo wa madini ya dhahabu usiotumia zebaki kutasaidia kuweka mpito salama wa ajira hiyo ili iwe na utu kwa mamilioni ya watu, huku tukitokomeza athari zake kwenye mazingira na kuwa na njia endelevu ya uzalishaji wa dhahabu,” amesema Bwana Fonseca.

Kila mwaka zaidi ya tani 2,700 za dhahabu huchimbwa duniani kote ambapo asilimia 20 hutokana na wachimbaji wadogo na wa kati ambao hutekeleza shughuli hizo katika mazingira magumu na hatarishi, wakikosa vifaa vya kazi na ujira mdogo.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa UNE, Joyce Msuya amesema uchafuzi utokanao na zebaki huathiri afya na bayonuai na hatimaye huingia kwenye chakula, maji na hewa.

“Hili ni tatizo la muda mrefu ambalo tunapaswa kulishughulikia sasa. Mpango huu unaonyesha kuwa pindi tunapoungana na kuchukua hatua za kulinda mazingira tunaweza kulinda afya ya jamii, kuwezesha watu kupata kipato na kulinda sayari yetu,” amesema Bi. Msuya.

Mada: