AV

Kuua wahudumu 7 wa afya Somalia ni ukatili usiokubalika -UNICEF

Get monthly
e-newsletter

Kuua wahudumu 7 wa afya Somalia ni ukatili usiokubalika -UNICEF

UN News
2 June 2020
By: 
Mwanamke akipita pembeni ya gari la wagonjwa ndani ya hospitali ya Benadir mjini Mogadishu, Somalia.
UN/Ilyas Ahmed
Mwanamke akipita pembeni ya gari la wagonjwa ndani ya hospitali ya Benadir mjini Mogadishu, Somalia.

Mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF amelaani vikali mauaji ya wahudumu wa afya ambao kazi yao ni kuokoa maisha ya kibinadamu nchini Somalia na kusema ukatili huo hauna nafasi na haukubaliki.

Katika taarifa yake iliyotolewa Ijumaa mkurugenzi huo Henroetta Fore amesema “Nimegadhabishwa na kitendo ya kuwateka na kuwauwa wahudumu saba wa afya katika kituo cha afya cha Kusini mwa Somalia. Kuwalenga wahudumu wa afya ni ukiukaji mkubwa wa sharia za kimataifa na unaweza kuwa ni uhalifu wa kivita. Mashambulizi haya ya kikatili yanaingilia suala la muhimu la ulinzi wa haki ya afya na watekelezaji wa unyama huo lazima wawajibishwe.”

Bi. Fore ametuma salamu za rambirambi kwa familia, marafiki na watu waliokuwa wakifanyakazi na marehemu hao , lakini pia kwa mfuko wa Zamzam waliokuwa wakifanya nao kazi watu hao waliouawa ambao ni moja ya washirika wakubwa wa nchini Somalia.

Mkuu huyo wa UNICEF ameongeza kuwa wahudumu hao wa afya ni mashujaa ambao wanaweka usalama wao rehani ili kutoa huduma za kuokoa maisha kwa watoto na familia zao.

Bi. Fore ameahidi kwamba “Kujitolea kwao na uwajibikaji wao tutauenzi na utakuwa katika mioyo yetu tunapoendelea kufanya kazi zetu kuwafikia Watoto walio hatarini Zaidi nchi nzima.”