AV

Zana za kidijitali zinaweza kusaidia Afrika kukabili ukosefu wa usalama wa chakula

Get monthly
e-newsletter

Zana za kidijitali zinaweza kusaidia Afrika kukabili ukosefu wa usalama wa chakula

Mazungumzo na mwanateknolojia wa kidijitali kutoka Uganda, Timothy Laku.
Afrika Upya: 
15 July 2021
Timothy Laku
Timothy Laku
Mtaalamu wa mabadiliko ya kidijitali Timothy Laku
Ikiwa huwezi kusoma sasa, sikiliza tu toleo la sauti: 
Sauti ya Kiingereza

Mtaalamu wa mageuzi ya kidijitali Timothy Laku, raia wa Uganda, anaamini kuwa Afrika ina hakika ya kufaidika pakubwa kutoka kwa mapinduzi ya nne ya viwandani, ambayo mtaalamu wa uchumi Klause Schwab, mwanzilishi wa Jukwaa la Uchumi Duniani, anasema yanasukumwa kwa kiasi fulani na teknolojia za kidijitali.

Matumaini ya kipekee ya Bwana Laku yanatokana na ukweli kwamba zana za kidijitali kwa sasa zinapatikana kwa Waafrika kwa njia ambayo teknolojia haikuweza kupatikana katika mapinduzi ya awali ya viwandani.

“Mapinduzi ya kwanza ya viwanda yalihusu injini za mvuke kutumika katika uchukuzi— meli. Mapinduzi ya pili ya viwandani ulitokea umeme ulipovumbuliwa. Mapinduzi ya tatu yalikuwa uvumbuzi wa kompyuta,” alisema, katika mahojiano na Afrika Upya.

"Ilichukua miaka 50 kwa Afrika kuridhia teknolojia katika mapinduzi ya kwanza na ya pili ya viwanda, na ilichukua miaka 10 kwa kompyuta kushika kasi barani."

Kuwa sambamba na maeneo mengine

Lakini sasa, anashikilia mtaalamu huyu wa kidijitali kuwa, "ni mara ya kwanza katika historia kwamba Afrika iko sambamba na maeneo mengine ulimwenguni.

“Ikiwa ni mtandao, Afrika pia ina mtandao; Ikiwa ni teknolojia inayojaribiwa nchini Japani, nchi za Afrika pia zinaijaribu. Kwa mfano, karibu nchi sita au saba tayari zinajaribu mtandao wa simu wa 5G barani Afrika,'' anasema.

Bwana Laku, ambaye ni Afisa Mkuu wa Teknolojia wa Bringo Fresh, kampuni ya Uganda inayotumia jukwaa la mtandaoni kuwaunganisha wakulima na watumiaji, hivi karibuni alizungumza kwenye mkutano ulioandaliwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa. Alitumia fursa hiyo kutafuta uungwaji mkono katika matumizi ya teknolojia kukabiliana na hasara na uharibifu wa chakula.

Ulimwenguni, tani bilioni 1.3 za chakula hupotezwa au kuharibiwa kila mwaka.

Katika Bringo Fresh, anasema: "Tunakusanya data kwenye upande wa usambazaji na upande wa mahitaji. Tunawapatia wakulima habari inayosaidia mipango yao ya uzalishaji na kuhakikisha soko thabiti la mazao yao. ”

Bringo Fresh pia inawafundisha wakulima kuhusu mazoea mazuri ya kilimo na kuhusu kuepuka hasara na uharibifu wa chakula.

Teknolojia katika kilimo

Bwana Laku anafurahia uwezo mkubwa wa simu za rununu katika kilimo cha Afrika. ''Acha tutoe mfano wa huduma ya pesa kwa simu. Wakulima wanaweza kuuza mazao yao na pesa hizo kusalia kwenye simu zao. Wakitaka kulipa karo za shule za watoto wao, wanahamisha pesa hizo kutoka kwa akaunti za simu zao za rununu hadi kwa akaunti za shule hizo. Hawahitaji kuondoka mashambani.

"Wanalipia bidhaa na huduma kupitia simu za rununu, na hiyo inamaanisha kuwa wanapata muda zaidi wa kufanya kazi kwenye mashamba."

Muungano wa Mfumo wa Simu za Rununu Duniani (GSMA) unaowakilisha maslahi ya makampuni ya simu za rununu ulimwenguni unasema katika ripoti yake ya 2021 kwamba, kote duniani, Afrika Kusini mwa Sahara imechukua "nusu ya huduma za pesa za rununu na theluthi mbili ya jumla ya shughuli hizo za pesa." Ripoti hiyo inashikilia kuwa takwimu hiyo itaongezeka katika miaka ijayo kwa sababu janga la COVID-19 linawalazimisha watu kutegemea huduma za kidijitali.

Bwana Laku anadai kuwa wakulima wanahitaji data muhimu ili kufanikiwa. Anaieleza namna hii: ''Katika mji mmoja, wakulima wanauza mfuko mmoja wa mahindi kwa $10. Lakini katika mji mwingine wa karibu, labda umbali wa dakika 30 kwa gari, mfuko wa mahindi unauzwa kwa $ 15. Habari hiyo ikiwa inapatikana kwa simu kwa wakulima kama hao, wanaweza kuuza mazao yao katika mji huo na kupata pesa zaidi. Kwa hivyo, wanafaidika kutoka kwa habari inayopatikana kupitia teknolojia. "

Kuunganishwa kwa utaratibu kwa teknolojia katika kilimo kunawavutia vijana wa Afrika katika sekta hii, anasema.

“Tunachokiona sasa ni kwamba vijana wengi wanashiriki katika kilimo. Wanaimarisha simu za rununu na matumizi ya kidijitali: wavuti, jukwaa la biashara mtandaoni, programu za rununu, uagizaji mtandaoni - mambo kama haya huwavutia.

Kuwavutia vijana

“Awali, kilimo kilimaanisha kwenda shambani na kulima udongo. Sivyo tena.''

Mchanganyiko wa uweledi wa kiteknolojia wa vijana na tajriba za wazee ni ushindi kwa pande zote.

Anasema: "Wakulima walio na umri mkubwa ambao hawajui kutumia teknolojia, ambao wanawaona wakulima wachanga wakitumia zana za kidijitali kuuza na kufaidika zaidi, sasa wanaanza kusema,"labda ni wakati wangu kuelewa kitu hiki kinachoitwa simu mahiri. Labda ninafaa kuanza kuelewa teknolojia hii.''

Je, itakuwaje kwa hasara ya baada ya uzalishaji?

Hasara za baada ya uzalishaji kwa kiasi fulani hutokana na ukosefu wa habari, ambao pia unaweza kusuluhishwa kwa uvumbuzi, Bwana Laku asema.

''Kwa hiyo, wakulima hawana habari ya kuwaruhusu kudhibiti harasa za baada ya uzalishaji. Hawajui jinsi ya kuhifadhi mazao kwa sababu hawajapatiwa mafunzo ya kitaalam ya kuweza kuhifadhi. Wamekuwa wakifanya kijadi, kama walivyofanya babu zao."

Wakulima na AfCFTA

Bwana Laku anatazamia kuwa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA) litakuwa baraka kwa wakulima wa Afrika. AfCFTA inahakikisha usafirishaji bure wa bidhaa na huduma zinazozalishwa barani.

"Maadam hakuna vikwazo vya mipakani, na kuna kiwango kimoja cha ushuru au hakuna ushuru kabisa, wakulima wanaweza kupanga na kusema, 'sawa, nina ardhi hii kubwa na kwa sababu ninaweza kupata masoko makubwa, ninaweza kuzalisha labda mara tano au mara 10 zaidi, '”anaelezea.

Anaongeza kuwa wakulima watahitaji habari kuhusu mahitaji na usambazaji katika masoko ya nje. "Na njia ya pekee ambayo habari hiyo inaweza kuwafikia ni kupitia majukwaa ya kidijitali"

Kikwazo, hata hivyo, katika mageuzi haya yote ya kidijitali, ni gharama ya mtandao. "Ikiwa gharama ya mtandao ni kubwa mno, haiwezekani kwa wakulima kutumia fursa ya teknolojia ya kidijitali," anasema. "Ufikiaji wa mtandao unapaswa kuwa haki ya kibinadamu."

Simu za bei rahisi zenye uwezo wa kuingia kwa mtandao zinasalia kuwa changamoto. GSMA inabainisha kuwa, "Katika Afrika Kusini mwa Sahara, kwa mfano, gharama ya wastani ya simu ya kiwango cha chini iliyo na uwezo wa kuingia kwa mtandao iliwakilisha zaidi ya asilimia 120 ya mapato ya kila mwezi kwa asilimia 20 ya watu maskini zaidi mwaka wa 2019."

Bwana Laku pia anataja miundombinu duni, haswa barabara mbovu, kama changamoto nyingine.

"Japo teknolojia inategemea mtandao, lakini ikiwa mkulima hawezi kusafirisha lori lote la mazao kutoka mji mmoja kwenda mji mwingine kwa sababu ni msimu wa mvua na barabara ni mbaya, mchakato huo hutamatika ghafla," anasema. “Mfumo wa usambazaji barani Afrika ni moja ya sababu inayofanya kila kitu kuwa ghali mno.

Mizozo au ghasia za kisiasa katika mataifa mengine pia ni kikwazo, anasema. "Kama kuna mzozo nchini, wakulima hawawezi kutumia teknolojia kikamilifu kwa maendeleo."

Uuzaji nje wa bidhaa ghafi kutoka Afrika zinazochakatwa nje ya nchi na kusafirishwa kurejea barani zitapunguza kasi ya ukuaji wa viwandani, anaonya.

Kuongeza thamani kwa mazao

“Kuna soko la bidhaa zilizoongezwa thamani barani Afrika. Kwa nini hatuwezi kujenga vifaa vya utengenezaji kuongeza thamani ya mazao yetu,” anauliza kwa swali la balagha.

"Kinachokosekana pia ni habari kuhusu ukubwa wa soko kwa bidhaa na pesa zinazopaswa kuwekezwa. Kwa mfano, ikiwa inaeleweka ni pesa ngapi zinaweza kupatikana kutoka kwa mfumo wa kuongeza thamani ya chokoleti na jinsi soko hilo lilivyo kubwa barani Afrika, basi wawekezaji zaidi wa ndani watavutiwa na mazungumzo ya kuongeza thamani.

"Kama ilivyo, inaweza kunichukua miaka 10 kupata faida katika nchi moja, lakini ikiwa nitaweza kufikia soko la watu bilioni 1.2 Afrika, tofauti na watu milioni 40 wa Uganda, basi, ghafla, faida ya uwekezaji itavutia." Kwa hali hii, AfCFTA inakaribishwa sana, anasema.

Mwishowe, Bwana Laku anawashauri vijana wa Afrika kujaribu kuwa wajasiriamali wa kijamii. "Watafute fursa huko nje na kufikiria kuhusu jinsi wanavyoweza kutumia zana za kidijitali kuzigeuza kuwa miradi yenye faida huku wakiongeza thamini kwa jamii zao."

More from this author