AV

Teknolojia yatoa tumaini kwa vifaru weupe wa Kaskazini wa Bara Afrika walio hatarini ya kuangamizwa

Get monthly
e-newsletter

Teknolojia yatoa tumaini kwa vifaru weupe wa Kaskazini wa Bara Afrika walio hatarini ya kuangamizwa

Pavithra Rao
Afrika Upya: 
22 October 2020
.
Vifaru ni wahanga wa kufukuzwa bila huruma na wawindaji haramu. Vifaru weupe wa kaskazini mweupe walitoweka mnamo 2018. Picha: Jemu Mwenda

Kenyan wildlife caretaker and guide, Jemu Mwenda, bittersweetly recounts one of his favorite memories of ‘Sudan,’ the male northern white rhino who died two years ago, making headlines across the world.

Mlinzi wa wanyamapori na mwelekezi porini nchini Kenya, Jemu Mwenda, anasimulia kwa kumbukizi yenye mseto wa furaha na uchungu kisa kimoja cha ‘Sudan,’ yule kifaru dume mweupe wa kaskazini aliyekuafa miaka miwili iliyopita, na kuwa kwenye vichwa vya habari kimataifa.

“Sudan alikuwa kifaru dume mweupe wa kaskazini wa mwisho aliyejulina kuwepo,” anafafanua Mwenda, anayefanya kazi katika Hifadhi ya Ol Pejeta, kituo cha wanyamapori nchini Kenya.

“Jioni moja nilipokuwa nikimlisha niliona akitokwa na machozi, na hilo lilinifanya kujiuliza: ‘Ni kitu gani kinachomliza?’”

Anaendelea: “Watu wanaweza kudhani kwamba wanyama hawana hisia, ila nilipomtazama Sudan machoni, nilihisi uchungu aliokuwa nao.

“Si rahisi kuwa ndiwe wa mwisho wa aina yako katika sayari yetu. Nadhani hisia ya kutoweka daima, bila kurudi tena, ni tanzia. Ni utupu ambao ungemfanya Sudan kuwa mwenye huzuni. Hili lilinibadilisha na kunisaidia kujua nina jukumu la kuwa sauti yake.”

Bwana Mwenda alitafakari kwa uchungu kuhusu kutoweka kwa vifaru dume weupe. Mwezi wa Mei 2019, shirika la Intergovernmental Science-Policy Platform on Biodiversity and Ecosystem Services (IPBES) lilikadiria kwamba takribani milioni 1 ya aina mbalimbali za mimea na wanyama zilikuwa katika hatari ya kutoweka daima. Shirika la IPBES lililoko Bonn, Ujerumani, husaidia kuimarisha uhusiano kati ya sayansi na sera kuhusu masuala ambayo yanahusiana na uanuwai wa viumbehai na huduma za mfumoikolojia.

Uwindaji wa kikatili

Vifaru haswa wameathiriwa sana na uwindwaji katili na majangili. Hifadhi ya wanyama ya Ol Pejeta ni makao ya vifaru jike wa kaskazini waliosalia — Fatu mwenye miaka 20 na Najin mwenye miaka 30.

Ni nini hufanya wanyama hawa wakubwa na wangwana wawe katika hatari ya kuwindwa?

Bwana Mwenda alieleza kwamba majangili huwalenga vifaru kwa sababu ya pembe zao zilizoundwa kwa keratin — elementi iliyomo katika kucha na nywele za wanadamu. Japo uuzaji wa pembe za ndovu uliharamishwa na Mkataba wa Biashara za Kimataifa ya Wanyama Walioko kwenye Hatari ya Kuangamia (CITES) tangu 1977, madai ya uwezo wake wa kimatibabu ndiyo yanayoendeleza utashi wake katika Mashariki ya Mbali.

“Ni ghali mno,” anasema, “haswa [kwa kuwa inaaminiwa kwamba elementi kutoka kwa pembe za kifaru] zaweza kutibu saratani, homa ya mafua, mtukutiko, na kuweza kutumiwa kama dawa ya kuongeza nguvu ya uzazi. Aidha, zinatumiwa kama ishara ya hadhi ya juu.” Kilo moja hugharimu kati ya $60,000 - $65,000 katika biashara ya magendo ya bara Asia,” anaongeza. “Watu wanahiari kulipa bei yoyote kudumisha afya yao.”

Uwindaji wa pembe za vifaru ulianza miaka ya 60 ya katika karne ya ishirini. Wakati huo idadi ya vifaru weupe ilikuwa takribani 2,400, kwa mujibu wa shirika la hisani la uhifadhi la Save the Rhino.

Maendeleo ya kiteknolojia

Japo serikali za kitaifa zilizo na idadi kubwa ya vifaru kama Afrika Kusini zinachukua hatua za kitamaduni kama kukata pembe ili kuwapunguzia hatari ya kuwindwa, ubunifu wa kiteknolojia unazingatiwa pia ili kukuza upya idadi ya wanyama hawa walio kwenye hatari ya kuangamizwa.

Mnamo Januari mwaka huu, Hifadhi ya Ol Pejeta ilitangaza habari za kutia moyo kwamba shahawa kutoka kwa marehemu Sudan na kifaru mweupe mwingine wa kaskazini aliyeaga ilihifadhiwa na kugandishwa na imechanganywa na mayai 12 kutoka kwa Fatu na Najin kuunda viinitete fanifu.

Viinitete hivi vilitarajiwa kupachikwa katika binamu wa kifaru wa kaskazini ambaye ni kifaru wa kusini. Hata hivyo, kwa sababu ya COVID-19, mipango hiyo ya upachikaji imesimamishwa kiasi.

Hata hivyo, mayai kutoka kwa kifaru mweupe wa kusini kule Ujerumani yalitolewa hivi karibuni na kuchanganywa na shahawa, na viinitete fanifu vinasubiri uhamisho.

Mchakato wa kuchanganya shahawa na mayai katika maabara (IVF) ulikuwa umefanikishwa na vifaru weupe wa kusini ambao hubeba viinitete vyao wenyewe, ila ni mara ya kwanza ambapo viinitete vya kifaru mweupe wa kaskazini vitabebwa na vifaru weupe wa kusini. Matokeo, kwa mujibu wa Hifadhi ya Ol Pejeta, yana uwezo wa kuasisi harakati za kuongeza idadi ya vifaru katika miaka ya usoni.

Bwana Mwenda anaamini kwamba kutumia teknolojia katika kuokoa vifaru kunaweza kuwa na manufaa makuu. “Nafikiri kwamba njia mbalimbali zaweza kujaribiwa ili kuokoa kifaru mweupe wa kaskazini, ikiwa ni pamoja na kupachisha, upandikizaji na kuchanganya shahawa na mayai katika maabara (IVF). Hizi mbinu saidizi za uzalishaji ni muhimu.”

Inaelekea kwamba watu wengi wanakubaliana naye. Waziri wa Utalii wa Kenya, Najib Balala aliwahimiza “wanasayansi kuchunguza namna ya kutumia teknolojia na ubunifu ili kuhakikisha kwamba vifaru hawatoweki kabisa duniani. Inafurahisha kuona kwamba huenda tukaweza kubadili tanzia ya kupoteza aina hii ya wanyama kwa kutumia sayansi.”

Kwa sasa, Bwana Mwenda anawahimiza watu kuwajali viumbe wenzao wenye uhai.

“Nahisi kwamba tuna jukumu kubwa la kuiboresha sayari hii, na haswa kwa kuwa mimi ni kijana, ninawajibika kuwasukuma vijana wenzangu wawe wenye kujali,” anasema “hali hii itakuwa na athari kwetu kama vijana na tuna jukumu la kuendelea kusaidia namna tuwezavyo.”

Pavithra Rao
More from this author