ąú˛úAV

Gharama kubwa ya kupausha ngozi

Get monthly
e-newsletter

Gharama kubwa ya kupausha ngozi

Hatari kubwa hufungamana na tamaa ya kuwa na ngozi nyeupe
Pavithra Rao
9 April 2019
An ad of a skin whitening cosmetic product in Kumasi, Ghana.
Alamy Photo/Jbdodane
Matangazo ya bidhaa za kupambaza ngozi kwenye Kumasi, Ghana.

“Nimekuwa na ngozi nyeusi kwa miaka mingi na nilitaka kubadilisha na kwa mweupe. Nilitaka kuona ingekuwaje kuwa mweupe na sasa nina furaha,” asema Mshoza, raia wa Afrika Kusini ambaye jina lake halisi ni Nomasonto Mnisi.

Bi. Mshoza ni maarufu kwa muziki wake — na sasa kwa ngozi yake iliyopaushwa. Awali alidhamiria kupausha weusi uliokolea (mapaku meusi katika ngozi yake) lakini akaamua kuidumisha ngozi nyeupe kila mahali.

Kupausha ngozi si jambo jipya barani Afrika. Limekuwepo kwa miongo mingi. Bidhaa za kupausha ngozi zinauzwa katika Amazon, soko la mtandaoni.

Lakini Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) linatahadharisha kwamba upaushaji ngozi waweza kusabibisha uharibifu wa maini na figo, kichaa, uharibifu wa bongo za vijusi na saratani.

Mbinu mpya inayoenea sana ya kupausha ngozi ni kujidunga glutathioni — chembechembe asili zinazozalishwa na maini kuzuia uharibifu wa seli — mwilini kupitia kwa mishipa. Tiba ya kudunga glutathioni mishipani inaweza kupausha ngozi, na bidhaa hiyo sasa yaweza kupatikana kama vidonge vijalizo vya chembechembe za kuzuia kuharibika kwa seli, anandika Aneri Pattani, katika Makala kuhusu mada hii kwa New York Times.

Hivi karibuni, mashirika yanayouza bidhaa za kutunza ngozi nchini Ghana na mataifa mengine ya Afrika yamekuwa yakiimarisha matumizi ya glutathioni, yakijaribu kuwarai wajawazito wanaotaka kupausha ngozi za watoto wao wakiwa katika mifuko ya uzazi.

Mamlaka ya Vyakula na Dawa ya Ghana inatahadharisha kwamba haijaidhinisha bidhaa zozote zenye glutathioni ama kwa matumizi ya mtu binafsi au “kama vidonge ili kuongeza weupe wa watoto ambao hawajazaliwa.’

Dawa za kudunga ni hatari zaidi

“Ni hatari mno kwa wajawazito kumeza vidonge vya kupausha ngozi,” aonya Catherine Tetteh, mwanzilishi wa Wakfu wa Melanin, shirika la kibinafsi linalofanya kampeni dhidi ya upaushaji wa ngozi lenye makao yake Geneva.

Dawa zidungwazo mwilini kuongeza weupe wa ngozi ndizo “hatari zaidi, kwa kuwa hujui kilichoko ndani ya vidungwavyo … na wengi wananunua kutoka masoko yasiyo rasmi,” aeleza Shingi Mtero, anayefundisha kozi kuhusu siasa za kupausha ngozi katika Chuo Kikuu cha Rhodes, Afrika Kusini, katika mahojiano na Afrika Upya.

Muungano wa Wanasaikolojia Weusi upatikanao Marekani unasema kwamba kupendelea kwa rangi nyeupe kunaweza kuathiri namna mtu anavyojithamini, mielekeo kuhusu urembo na nafasi za kiuchumi. Na tasnia ya bidhaa za kutunza ngozi na vipodozi inafaidika kutokana na utashi mkuu wa wanawake wa Kiafrika kuwa na ngozi nyeupe.

Takwimu zilizokusanywa na Shirika la Afya Ulimwenguni (SAU) mwaka 2011 zilionyesha kwamba 40% ya wanawake Waafrika hupausha ngozi zao. Katika mataifa mengine idadi hiyo ni ya juu: idadi kubwa ya 77% ya wanawake Nijeria, 59% katika Togo, 35% Afrika Kusini, 27% Senegali na 25% Mali wanatumia bidhaa za kupausha ngozi.

Kabla-na-baada picha za wanawake waliopausha ngozi zao zimeenea katika masoko ya bidhaa za kutunza ngozi na vipodozi barani Afrika. Mwimbaji wa Kameroon Dencia anaendesha biashara inayofana kuuza krimu za kupausha ngozi. Anadai kwamba “weupe ni utakatifu.”

Heshtegi kama vile #skinwhitening na #yellowbone, zinazotangaza bidhaa za ngozi ambazo zasemekana kutoa matokeo ya haraka na kusababisha maisha ya furaha, zimetamalaki kumbi za mitandao ya kijamii, hasa Instagram.

Viungo vya kupausha ngozi

Krimu nyingi za kisasa za kupausha ngozi zina viungo vinavyozuia uzalishaji wa melanini, kemikali ya mwili inayoipa ngozi weusi wa asili. Mfano wa viungo hivyo ni haidrokwinoni, kiungo kinachoipa ngozi weupe. Ila SAU laonya kwamba athari zisizotarajiwa za haidrokwinoni ni pamoja na ugonjwa wa ngozi (unaozua mwasho), mapakupaku ya samawati-meusi katika ngozi na hata upofu.

Baadhi ya krimu zina steroidi (chembe za kutunisha misuli), misombo ambayo aghalabu huelekezwa na madaktari kutibu matatizo ya ngozi kama ukurutu, mzio na ugonjwa wa mwasho wa ngozi, na inayotakiwa kutumiwa kwa chini ya siku saba na katika sehemu zilizoathiriwa tu. Matumizi mengi ya krimu za steroidi kwa kipindi kirefu yanaweza kusababisha wembamba au udhaifu wa ngozi, alama zitokanazo na kunenepa upesi na haraka katika ngozi, na uwezo wa kuchubuliwa kirahisi.

Kwa kuwa stiroidi hupunguza idadi ya melanosaiti, au seli zinazozalisha melanini, wanaotengeneza krimu za kupausha ngozi huchanganya stiroidi katika bidhaa zao bila kujali.

Matumizi ya muda mrefu ya krimu hizi hatimaye husababisha utegemezi au uraibu kwani ngozi hurejelea rangi ya asili matumizi yakisitishwa kwa mujibu wa watafiti , , na katika kazi yao Fifty Shades of African Lightness: A Bio-Psychosocial Review of the Global Phenomenon of Skin Lightening Practices.

Kutokana na hatari hizi, mataifa ya Afrika yakiwemo Ghana, Côte d’Ivoire na hivi karibuni Rwanda, yameanza kupiga marufuku bidhaa za kupausha ngozi, hasa krimu zilizo na haidrokwinoni.

Lakini watengenezaji wanapambana na marufuku hizo. Huenda wasiorodheshe majina ya viungo vilivyopigwa marufuku katika mifuko ya bidhaa zao katika mazingira fulani fulani. Bidhaa za kupausha ngozi “zinapatikana kwa wingi katika maduka ya kuuza dawa, mitaani na masokoni,” anaongeza Bi. Tetteh.

“Sasa tunawaelimisha watu na kutwaa hizo bidhaa haramu,” anasema Francois Uwinkindi, Mkurugenzi wa Kitengo cha Magonjwa ya Saratani katika Wizara ya Afya ya Rwanda.

Kwa nini hamu kuu ya kupausha?

Tukio la kupausha ngozi limezua tofauti na suitofahamu, asema Bi. Metro, huku akiongeza “weupe umekwezwa na kuwasilishwa kama kigezo cha kilimwengu cha maendeleo. Watu wasemapo kwamba linahusu weupe, si kuwa mweupe kimwili hasa, ni kutaka kupata vitu ambavyo watu weupe hupata kwa njia rahisi — upendeleo, hadhi ya kiuchumi na kijamii.”

Bi. Mtero aendelea: “Ngozi nyeupe ndiyo wanayoitaka wanaume; ina mantiki fulani kwa wanawake kuingia kwenye kiwango cha ubora unaotakiwa na wanaume ili kuimarisha nafasi zao za kuolewa. Na ndoa ni aina ya mtaji wa kijamii — kuwa mke wa fulani, mzazi wa mtoto na mhusika anayeheshimiwa katika jamii. Haya yatamkweza mwanamke.”

Anaongeza, “wanaounga mkono upaushaji wanashikilia ndoto kwamba ngozi nyeupe itawasaidia kupata ajira bora, na kutongoza kwa njia rahisi mno.”

Nafasi bora za ajira na hadhi iliyokwezwa inayodhaniwa na watu kuletwa na ngozi nyeupe inatoa taswira tofauti—taswira ya wanawake wa Kiafrika wanaofanya uamuzi razini, uliozingatiwa vyema na wa kibiashara

“Hii ndiyo sababu ninaamini kupiga marufuku bidhaa hizi hakutasuluhisha tatizo hilo kikamilifu,” asema Ola Orekunrin, daktari wa tiba na mwanzilishi wa Flying Doctors Nijeria, huduma ya ambulansi za ndege katika Afrika Magharibi. “Tunastahili kuuweka wazi mdahalo kuhusu rangi ya ngozi na urembo. Vyombo vya habari, hasa vinavyolenga urembo, vinastahili kushirikisha aina nyinginezo za urembo zaidi ya ubora wa Kimagharibi, ili kumaliza huu upendeleo wa rangi.”

Kufuatia ufanisi mkuu wa sinema maarufu ulimwenguni Black Panther, ambayo pakubwa ilishirikisha waigizaji weusi, idadi inayoongezeka ya vijana wa Kiafrika wanaonea fahari rangi yao, huku wakibuni heshtegi kama #melaninpoppin na #blackgirlmagic kusherehekea rangi nyeusi ya ngozi yao.

Mwigizaji anayesifika kimataifa wa Kenya Lupita Nyong’o, aliyeshirikishwa katika Black Panther anaeleza Vogue, gazeti la Marekani la mitindo na mitindo ya maisha, kwamba, “siwezi kutoroka uhalisia wa namna nilivyo na rangi yangu au jamii pana, na namna inavyoweza kuona hilo.”

Anasema kwamba kujikubali na kuridhika na alivyo kulikuwa muhimu kwa maisha ya ufanisi.

Pavithra Rao
More from this author