AV

Waziri mchanga kabisa Afrika awafungulia milango wanawake na wasichana

Get monthly
e-newsletter

Waziri mchanga kabisa Afrika awafungulia milango wanawake na wasichana

Bogolo Kenewendo mwenye umri wa miaka 32 kutoka Botswana pia ni mshauri wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu ushirikiano wa kidigitali
9 April 2019
Bogolo Kenewendo of Botswana is also adviser to the UN Secretary-General on digital cooperation
Alamy Photo
Bogolo Kenewendo wa Botswana pia ni mshauri wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa juu ya ushirikiano wa digital.

Bogolo Kenewendo anaeleza kwamba, “nilikuwa mtoto wa kawaida wa Botswana na nilipata malezi ya kawaida.”

Bi. Kenewendo, aliyejiandaa na kulenga zaidi ya umri wake, anajaribu kuwa mwenye staha. Akiwa na umri wa miaka 32, yeye ndiye waziri mchanga zaidi wa Botswana na anasimamia Wizara ya Uwekezaji, Biashara na Viwanda.

Kama mtoto Motopi, kijiji kidogo katikati ya Botswana, Bi. Kenewendo ailijiona akichangia katika maendeleo ya Botswana.

Alikutana na Mke wa aliyekuwa Rais wa Marekani, Bi. Michelle Obama mwaka wa 2011 Washington D.C. kama mshiriki katika Mpango wa Viongozi Wachanga wa Afrika, ushirika ulioanzishwa 2010 na Idara ya Masuala ya Kigeni ya Marekani.

Alijitosa katika siasa mwaka wa 2017 Rais mstaafu Ian Khama alipomchagua katika Baraza la Mashauriano ya Upeo lililopewa jukumu la kushughulikia changamoto zinazokabili sekta ya kibinafsi ya Botswana.

Baadaye mwaka huo, Rais Khama alimteua kuingia bungeni kulingana na kipengele cha katiba kinachomruhusu Rais kuufanya uteuzi huo kwa bunge la taifa la Botswana.

Baada ya kuhitimisha masomo yake Uingereza na kupata shahada ya uzamili katika taaluma ya Uchumi wa Kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Sussex, Bi. Kenewendo alifuzu kuwa mtaalamu wa uchumi katika Wizara ya Biashara na Viwanda nchini Ghana. Kabla ya wadhifa huo alikuwa mshauri wa masuala ya kiuchumi katika shirika la utafiti kuhusu sera, Econsult Botswana.

“Mimi ni shabiki wa umoja wa Afrika, nilifurahi kufanya kazi Ghana, ambako kuna historia pevu ya vuguvugu la umoja wa Afrika,” aliambia Afrika Upya katika mahojiano.

Bwana Khama alipompisha Mokgweetsi Masisi kuwa Rais mwezi wa Aprili 2018, Rais mpya alimteua Bi. Kenewendo katika baraza la mawaziri la Botswana kusimamia uwekezaji, biashara na uchumi, hatua iliyoungwa mkono na wanaharakati wa masuala ya kijinsia nchini humo.

Kama mbunge, Bi. Kenewendo aliwatetea watoto na wanawake, akisisitiza hasa uwakilishi wa wanawake katika sekta zote. Moja kati ya mafanikio yake ilikuwa kudhamini hoja ya kuongeza umri wa kuridhia mahusiano ya kimapenzi katika nchi yake kutoka miaka 16 hadi 18.

Chini ya uongozi wake, Wizara ya Uwekezaji, Biashara na Uchumi ya Botswana itahitimisha usajili wa biashara kidijitali mwezi Mei, hatua itakayowezesha kampuni na biashara ndogondogo kusajiliwa mtandaoni. Lengo ni kuboresha wepesi wa kufanya biashara nchini humo.

Anasema mamake ndiye kielelezo chake kwa kuwa, “alinifundisha kuwa imara wakati wa dhiki.”

Kuhusu mustakabali wake, Bi Kenewendo asema kwamba anapanga kuanzisha jamii ya mtandaoni ambako vijana wa Kiafrika wanaweza kutangamana na kubadilishana tajriba zao. Mradi huo utasaidiana na Wakfu wa Molaya Kgosi — mpango wake wa sasa wa kuwezesha uongozi wa wanawake na vijana katika shule za Botswana.

Bi. Kenewendo amepokea tuzo mbalimbali kwa juhudi zake katika shughuli mbalimbali, ikiwemo moja mwaka wa 2012 na Junior Chamber International Botswana, shirika la misaada, likimtambua kama mmoja kati ya vijana bora katika nchi ya Botswana. Mwaka wa 2016 alipokea Tuzo ya Wanamageuzi wa Botswana na Tuzo ya Mwanamke Ngangari kwa michango yake kwa biashara na uongozi.

Kimataifa, Bi. Kenewendo ni mwanachama wa Jopo la Upeo kuhusu Ushirikishi wa Kidijitali, lililoanzishwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kupendekeza namna serikali, sekta ya kibinafsi na mashirika ya haki za kibinadamu na washikadau wengine wanaweza kushirikiana katika masuala ya kidijitali. Mwenyekiti wa Jopo hilo ni Melinda Gates, wa Wakfu wa Bill & Melinda Gates, na Jack Ma, Mwenyekiti Mtendaji wa Alibaba Group Holding.

Mwaka wa 2009 alikuwa mjumbe mchanga akiiwakilisha nchi yake katika Kikao Kikuu cha 64 cha Umoja wa Mataifa. Aliteuliwa kuwasilisha taarifa katika mojawapo wa hafla kwa niaba ya vijana wa Afrika kwa Katibu Mkuu.

Anawashauri vipi vijana? “Imarisheni utendakazi wenu. Mkitazama historia kwa makini mtagundua kwamba uongozi wa vijana barani Afrika si kitu kigeni. Wanamapinduzi wengi walikuwa vijana,” Bi. Kenewendo anasihi.

More from this author