AV

Uhamiaji ulio salama na ulioratibiwa

Get monthly
e-newsletter

Uhamiaji ulio salama na ulioratibiwa

Mkataba wa kimataifa kuhusu uhamiaji waweza kukabili dhana hasi kwamba wahamaji ni kero
Kingsley Ighobor
5 February 2019
Rescue operations of African ...
Photo: IOM / Malavolta
Shughuli za uokoaji wa wahamiaji wa Afrika zinafanyika kwenye Channel ya Sicily, Italia. Picha: IOM / Malavolta

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Chansela wa Ujerumani, Angela Merkel na Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May walitembelea mataifa ya Afrika mnamo Agosti 2018 na kuibua matumaini ya kuongeza uwekezaji wa kigeni wa moja kwa moja (FDI) katika bara hili.

Bwana Macron alizuru Nijeria, Bi Merkel naye akatembelea mataifa ya Ghana, Nijeria na Senegali, ilhali Bi. May alizuru Kenya, Nijeria na Afrika Kusini.

Mbali na suala la uwekezaji wa kigeni wa moja kwa moja (FDI), viongozi hawa wenye ushawishi mkubwa walikuwa wakitafuta namna ya kuzuia milolongo ya wahamaji ambao hutoka bara Afrika kwenda bara Ulaya kwa nia ya kutafuta nafasi za ajira na maisha mazuri.

“Ninaamini katika mchezo unaowapa wote ushindi. Wacha tusaidie Afrika kufaulu. Wacha tuwape matumaini mapya vijana wa Afrika papa hapa Afrika,” Rais Macron alisema akiwa Nigeria na akaeleza kwamba kulikabili tatizo la uhamiaji katika chimbuko lake kungenufaisha mataifa ya Ulaya.

Eduardo Porter na Karl Russell, waandishi wa habari wa New York Times walikariri kauli za Rais wa Ufaransa: “Ikiwa mataifa tajiri yanahitaji wahamiaji wachache, labda hatua bora kwayo ni kayasaidia mataifa maskini kutajirika, ili watu wachache wapate mshawasha wa kuhamia kwingine.”

Waafrika walio safarini

Kila siku mamia ya Waafrika, wakiwemo wanawake na watoto, huondoka kutafuta utajiri halisi au wa kufikirika tu Ulaya au Marekani. Takribani wahamiaji milioni moja kutoka kusini mwa Jangwa la Sahara waliingia Ulaya kati ya 2010 na 2017 kulingana na Kituo cha Utafiti cha Pew, shirika lisilopendelea upande wowote na lenye kusisitiza ukweli lililoko jijini Washington, D.C.

Kituo cha Pew kinabainisha mataifa ya Ghana, Kenya, Nijeria, Senegali, Somalia na Afrika Kusini kama vituo muhimu vya wahamiaji wa mataifa ya kusini mwa Jangwa la Sahara wanaoelekea Ulaya na Marekani. Kituo hicho kinaorodhesha Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, São Tomé na Príncipe, Eritrea na Namibia kama nchi zilizo na idadi inayokua kwa kasi sana ya wahamiaji wa kimataifa wanaoishi nje ya nchi zao asilia.

Ripoti ya mwaka 2018 kuhusu Uhamiaji Ulimwenguni ya Shirika la Kimataifa kuhusu Uhamiaji (SKU) yasema kwamba Waafrika wanahama kwa sababu ya “mizozo, kuteswa, uharibifu na mabadiliko ya mazingira, pamoja na ukosefu mkubwa wa usalama wa watu na pia wa nafasi za kujiendeleza.” Njia za uhamiaji zitumiwazo sana na Waafrika ni pamoja na Algeria hadi Ufaransa, Burkina Faso hadi Côte d’Ivoire, Misri hadi Milki za Uarabu, Moroko hadi Uhispania, na Somalia hadi Kenya.

“Kati ya wahamiaji milioni 258 ulimwenguni, milioni 36 ya wahamiaji wa kimataifa wanaishi Afrika, huku milioni 19 wakiishi katika nchi isiyo yao barani Afrika na wengine milioni 17 wakiishi Ulaya, Marekani Kaskazini na maeneo mengineyo,” Ashraf El Nour, Mkurugenzi wa SKU New York, alieleza Africa Renewal.

Uhamiaji unapokosa kudhibitiwa na kusimamiwa vyema, unaweza kusababisha hisia hasi na za udanganyifu kuhusu wahamiaji ambazo huchochea semi za chuki dhidi ya wageni, kutovumiliana na ubaguzi wa rangi,” Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alisema katika hafla moja huko jijini New York mnamo Septemba iliyopita.

“Usemi kuwa wahamiaji ni tishio na chanzo cha hofu, ambao umetamalaki vyombo vya habari vya kimataifa kuhusu taarifa za uhamiaji, ni udanganyifu,” alisema Mukhisa Kituyi, Katibu Mkuu wa Mikutano ya Kibiashara na Maendeleo ya Umoja wa Mataifa (UNCTAD), baraza la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia biashara, uwekezaji na masuala ya maendelea, katika mahojiano na Africa Renewal.

Uhamiaji ulioratibiwa

Wataalamu wanasema kwamba Mkataba wa Kimataifa kuhusu Uhamiaji, ambao ni mkataba wa kwanza uliowahi kuafikiwa kwa majadiliano kati ta mataifa kuhusu uhamiaji wa kimataifa, unaweza kutumiwa kukabliana na mitazamo hasi kuhusu wahamaji.

SKU lasema mkataba huo utasaidia kutimiza “uhamiaji salama, ulioratibiwa na unaokubalika,” huku ikiutaja kama fursa ya “kudhibiti uhamiaji, kukabili changamoto zinazohusiana na uhamiaji wa kisasa, na kuimarisha mchango wa wahamiaji na uhamiaji kwa maendeleo endelevu.

Mkataba huo unajumuisha malengo 23, yakiwemo kupunguza mambo yanayowazuia watu kuanzisha vitegauchumi endelevu katika mataifa yao ya asili; kupunguza hatari ambazo wahamiaji hukabiliana nazo katika hatua mbalimbali za kuhama kwa kuheshimu uhamaji, kulinda na kutimiza haki zao za kibinadamu na kuwapa ulinzi na usaidizi; mbali na kuweka mazingira yanayowawezesha wakimbizi wote kuimarisha jamii husika kwa uwezo wao wa kibinadamu, kiuchumi na kijamii, na kwa hivyo kuwezesha michango yao kwa maendeleo ya kudumu katika viwango vya kijamii, kitaifa, kieneo na kimataifa.

Mkataba huo pia unapendekeza uwezeshaji wa matumizi ya pesa nyumbani kwa njia ya haraka, salama na nafuu pamoja na kuimarisha ushirikishi wa wahamiaji katika masuala ya pesa; kuhakikisha kwamba wahamiaji wana ithibati ya kutambuliwa kisheria na usajili mkamilifu; na pia kuwapa wahamiaji nafasi ya kupata huduma za kimsingi.

Mkataba wa Kimataifa kuhusu uhamiaji haushurutishi kisheria, hata hivyo vipengele vyake vyaweza kurejelewa na wanaotunga sera kuhusu uhamiaji na wanaharakati wa haki za kibinadamu katika hali ambapo wahamiaji wanadhulumiwa.

Kulingana na utafiti uliofanywa na Baraza la Utafiti wa Sayansi za Kijamii (BUSK), shirika lililoaanzishwa kisheria lenye makao yake Afrika Kusini, mitazamo hasi au hata vurugu dhidi ya wahamiaji hutokana na hofu kwamba wao hunyakua nafasi za ajira kutoka kwa raia wenyeji au kwamba wao hushiriki uhalifu.

Katika utafiti huo, ambao ulizingatia mitazamo ya wananchi wa Afrika Kusini kuhusu wahamiaji, 30% ya umma waliwalaumu wahamiaji kwa “kuiba nafasi za ajira za wenyeji wenye bidii”, huku 30% wakitaja vitendo vya uhalifu vya wahamiaji.

Hata hivyo, tawi la Afrika Kusini la SKU lilipinga kwa kueleza kwamba, “uhamiaji hauhujumu makadirio ya muda mrefu ya ajira au ujira wa wafanyakazi asilia,” na kuongeza kwamba “wahamiaji huchukua nafasi maradufu ya kuwa wajasiriamali wakilinganishwa wenyeji.” Serikali ya Afrika Kusini hukashifu uvamizi unaofungamana na chuki dhidi ya wageni.

Mkabala wa kiuchumi wa uhamiaji

Bwana Kituyi alisema kwamba tafiti nyingi kuhusu uhamiaji zinalenga “shida zinazowakabili wahamiaji, migogoro kuhusu mshikamano wa kimataifa na changamoto za kibinadamu.” Alitamani kwamba uhamiaji uangaziwe kwa kuzingatia mkabala wa maendeleo ya kiuchumi.

Mhamiaji wa asili ya Msumbiji, Bi Lúcia Kula, ambaye ni mtafiti Uingereza, aliafiki na akaongeza kwamba majadiliano kuhusu uhamiaji yanastahili kulenga michango ya wahamiaji kwa jamii zao mpya.

“Miongoni mwa mambo muhimu ambayo wao (wahamiaji) hufanya katika mataifa wanamoingia ni kuongeza thamani. Wanaingia katika nyanja ambamo wana ushindani mzuri … na hali hiyo yaweza kuinua uchumi wa mataifa husika,” Bwana Kituyi alifafanua.

Wahamiaji wengi ni wataalamu wenye vipaji na wao hutoa huduma za kitaalamu katika mataifa yao mapya. Iso Paelay, kwa mfano, alitoka Liberia miaka ya 90 wakati vita vilikuwa vimechacha na kuanzisha makao mapya Ghana. Huko Ghana, Paelay aliinukia kuwa mtangazaji maarufu katika TV3, shirika la habari maarufu katika nchi hiyo. Yaonekana, hasara ya Liberia ilikuwa faida ya Ghana.

Bwana Kituyi azungumzia hali ambapo wahamiaji huenda katika mataifa mengine kujihusisha na biashara ya vyakula vya makabila yao. “Wanaanza kuunda mbinu za kupata vyakula kutoka kwa mataifa yao,” alisema. Mikahawa ya vyakula inayomilikiwa na Wahabeshi ipatikanayo Nairobi nchini Kenya ni pamoja na Abyssinia, Habesha na Yejoka Gadenthat na huwauzia wateja wake vyakula kama vile injera.

Mhahawa wa Kimataifa wa Abuja unaopatikana Union, New Jersey, huuza vyakula vya kiasili ya Nijeria kama vile eba, amala na fufu pamoja na pombe maarufu ya Gulder. Waafrika na watu wengine wengi huzuru “Senegal Ndogo”, mtaa mdogo Harlem katika jiji la New York kwa wingi, kununua chochote cha asili ya Kiafrika — vyakula, kanda za video za muziki, bidhaa za nywele, vitu vya kidini na mavazi yaliyoshonwa barabara.

Huku wakifanya kazi kwa bidii, wakipata pesa na kuchangia kwa mataifa yao mapya, wahamiaji wa Kiafrika pia “hutuma pesa kiasi fulani nyumbani kusaidia familia zao,” Bwana Kituyi alieleza. Asilimia themanini na tano (ya pesa wapatazo wahamiaji) husalia katika nchi wanamoishi na ni 15% pekee ambayo hutumwa nyumbani katika nchi zao asilia.

“Sehemu kubwa ya pesa ninazopata hapa (Marekani) ninazitumia papa hapa; ninalipia bili na kununua vitu nihitajivyo. Nyingine ninatuma kuwatunza wazazi wangu,” anaafiki Christy Emeagi, wakili aliyegura Nijeria “kwa kuwa niliwatakia watoto wangu ambao hawakuwa wamezaliwa maisha mema.”

Kujumuishwa kwa mbinu salama na za haraka za kutuma pesa nyumbani katika Mkataba wa Kimataifa kuhusu Uhamiaji kutakuwa habari za kuwapendeza wahamiaji wa Kiafrika.

Benki ya Dunia inaripoti kwamba pesa zilizotumwa na wahamiaji kwa nchi za Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara mwaka wa 2017 zilikuwa takribani dala bilioni 34. Hizo ni zaidi ya msaada rasmi wa maendeleo (MRM) wa dala bilioni 25 kwa eneo hilo mwaka huo.

Bwana Kituyi anasema, “inaudhi kuona mashirika ya kutuma pesa kama vile Western Union, PayPal na mengine (aghalabu yakiwa ya kimataifa) yakidai ada za juu kulipia huduma ya kutuma pesa.”

Wataalamu wanaamini kwamba itachukua muda mrefu kutimiza malengo ya Mkataba wa Kimataifa kuhusu Uhamiaji. Hata hivyo, athari ya dharura ya mkataba huo ni kwamba uhamiaji salama, ulioratibiwa na unaokubalika ni miongoni mwa mijadala muhimu kimataifa. Na hiyo ni hatua nzuri.