AV

Huku zikiwa na matumaini ya amani ya kudumu, Uhabeshi na Eritrea sasa zalenga kurejesha ushirikiano wa kibiashara

Get monthly
e-newsletter

Huku zikiwa na matumaini ya amani ya kudumu, Uhabeshi na Eritrea sasa zalenga kurejesha ushirikiano wa kibiashara

Nchi zote mbili zasema huu ni wakati wa maendeleo
Daniel Otieno
5 February 2019
President Isaias Afwerki and Prime Minister Abiy Ahmed sign the Joint Declaration of AV and Friendship between Eritrea and Ethiopia on 9 July 2018. Photo: Yemane Gebremeskel
Photo: Yemane Gebremeskel
Rais Isaias Afwerki na Waziri Mkuu Abiy Ahmed ishara Azimio la Pamoja la Amani na Urafiki kati ya Eritrea na Ethiopia mnamo 9 Julai 2018. Picha: Yemane Gebremeskel

Upepo wa mabadiliko unavuma katika Upembe wa Afrika kufuatia mkataba wa amani uliotiwa sahihi na Waziri Mkuu wa Uhabeshi, Abiy Ahmed na Rais wa Eritrea, Isaias Afwerki, huko Jeddah, Saudi Arabia, tarehe 17 Septemba.

Mataifa hayo mawili yamesitisha uhasama baina yao na kurejesha ushirikiano wa kibiashara na wa kidiplomasia.

“Biashara ya ndani inanawiri tena huku Waeritrea na Wahabeshi wakibadilishana bidhaa na huduma bila matatizo kuhusu sarafu. Birr-nakfa [sarafu za mataifa husika mtawalia] zilibadilishana kwa usawa. Haya ni mendeleo chanya – lakini ambayo yanahitaji kuimarishwa zaidi!” anasema Kjetil Tronvoll ambaye ni Profesa wa Norwe afuatiliaye matukio katika eneo la Upembe wa Afrika na ambaye pia ni mwaasisi wa Asasi ya Kimataifa ya Sheria na Sera (International Law and Policy Institute), inayojumuisha washauri mabingwa, na yenye makao yake huko Oslo.

Baada ya vita vikali vilivyodumu miaka 20 (kuanzia 1998 hadi 2018) na ambapo takribani watu 100,000 waliuawa, mkataba huo umewezesha huduma za usafiri wa angani kurejea, mawasiliano ya simu kuanzishwa tena, uhasama wa kijeshi kusitishwa na familia kuunganishwa tena.

Wakati Mkataba huo ukitangazwa, mamia ya wananchi walikumbatiana huku wakisherehekea katika mataifa husika. Viongozi wao pia wamefungua rasmi maeneo ya viingilio katika mipaka yao ambavyo vilikuwa vimefungwa kwa miaka 20.

Tangu mnamo 1998, hakuna mkuu wa nchi wala mwakilishi wa serikali aliyewahi kuitembelea nchi jirani, Uhabeshi au Eritrea. Nyaya za simu zilikuwa zimekatwa, na kwa hali hiyo kukatiza mawasiliano kati ya nchi hizo mbili.

Shirika la ndege la Ethiopia Airlines, ambalo lilisitisha safari zake kupitia Eritria mwaka wa 1998, sasa limerejesha safari hizo, ndege zake zikitua Asmara, jiji kuu la Eritrea kila juma. Hii ni hatua ambayo huenda ikapiga jeki ushirikiano wa kibiashara na kuchangia ukuaji wa kiuchumi.

“Huu ndio ujumbe wangu kwa Wahabeshi: upendo waonekana njia bora kwenu,” Waziri Mkuu, Ahmed alisema akiwa Jeddah, huku akiongeza kwamba, “Upendo ndiyo njia ya pekee kwetu na ndugu zetu Waeritrea.”

Rais Afwerki alisema, “Chuki, ubaguzi na kula njama sasa kumefika kikomo. Lengo letu kuanzia leo linastahili kuwa kuendelea na kukua pamoja. Sasa ni wakati wa kufidia muda uliopotea.”

Upeo wa mgogoro huo ulikuwa na athari halisi kwa maisha ya wananchi wa Eritrea na wa Uhabeshi. Astebeha Tesfaye, raia wa Uhabeshi ambaye ameishi Eritrea tangu mwaka wa 1998, anatumai kurejea nyumbani sasa. Alikuwa amezuru Eritrea kuwatembelea marafiki zake miaka 20 iliyopita wakati uhasama ulipozuka. Alilazimika kusalia Eritrea kutoka wakati huo.

“Nilikuwa nimeazimia kusafiri kwa basi siku ambayo ingefuata (kurejea Uhabeshi), lakini nikasikia kwamba barabara zimefungwa, na kwamba hakuna aliyeruhusiwa kuvuka mpaka kuingia au kutoka Uhabeshi au Eritrea,” Bwana Tesfaye aliambia shirika la habari la BBC.

Wengi wanamsifia Waziri Mkuu wa Uhabeshi mwenye umri wa miaka 41 kwa kuongeza kasi na kubadili toni na mwelekeo wa mazungumzo ya amani.

Bwana Ahmed alishangaza pande zote husika pindi alipochukua hatamu za uongozi kwa kutangaza kwamba Uhabeshi ingeirejeshea Eritrea mji wa mpakani uliozozaniwa wa Badme. Mji huo upo katika eneo la Gash-Barka, umbali wa kilomita 139 kusini magharibi mwa Asmara. Huku kikihalalisha uamuzi wa kuukabidhi mji huo kwa Eritrea, chama tawala, Ethiopian People’s Revolutionary Democratic Front, kilisema kwamba watu wa Uhabeshi na wale wa Eritrea wamefungamana katika masuala ya lugha, historia na unasaba.

Mkataba huo maarufu kama Mkataba wa Jeddah ulikuwa tokeo la hatua mbalimbali za amani zilizoanza tarehe 8 Juni 2018 kwa kumbatio la kihistoria kati ya viongozi wa mataifa hayo huko Asmara. Hilo lilifuatiwa na kutiwa sahihi azimio la pamoja tarehe 9 Julai kuko huko Asmara, kisha Mkataba wa Jeddah kabla ya kurejelewa kwa ushirikiano wa kidiplomasia na wa kibiashara tarehe 8 mwezi wa tisa.

Mkataba huo ulidhaminiwa na Mfalme wa Saudi Arabia, Salman bin Abdulaziz Al Saud, ambaye alikuwa mwepesi wa kuwatuza viongozi hao wawili Nishani ya Mfalme Abdulaziz (Medal of King Abdulaziz). Miongoni mwa waliohudhuria sherehe hiyo ya kutia sahihi mkataba huo ni Katibu wa Umoja wa Mataifa António Guterres na Mfalme wa Saudi Arabia Salman bin Abdulaziz Al Saud.

Ibara ya kwanza ya Mkataba wa Jeddah wenye hoja saba inasema: “Hali ya kivita kati ya mataifa haya mawili imekoma, na enzi mpya ya amani, urafiki na ushirikiano wa kina imeanza.”

Ibara nyinginezo zinashughulikia masuala mengine yakiwemo kuimarisha ushirikiano katika usalama, ulinzi, biashara na uwekezaji, na nyanja za utamaduni na za kijamii; kuanzisha maeneo bia ya kiuchumi; na kukabili ugaidi na “ulanguzi wa watu, silaha za kivita na dawa za kulevya, kulingana na mapatano na mkataba wa kimataifa.”

Ikiwa na mkataba huu, Uhabeshi ambayo haina bandari inaweza kutumia bandari za Bahari ya Shamu katika Assab, kusini mwa Eritrea, na Massawa iliyo kaskazini, bila kutozwa ushuru. Uhabeshi imekuwa ikilipa dola bilioni 1.5 kila mwaka kutumia bandari za Djibouti. Kwa upande wake, Eritrea itanufaika kwa kupata wateja milioni 100 wa Uhabeshi kutumia bidhaa zake (nambari mbili kwa wingi barani Afrika).

Kabla ya Mkataba wa Jeddah, majaribio mengi ya kuleta amani kati ya mataifa haya mawili yalifanywa bila kufaulu. Mnamo 2002, Uhabeshi ilikataa uamuzi wa Tume ya Mipaka. Uamuzi huo uliarifu kwamba Badme ni eneo lililofaa kumilikiwa na Eritrea.

Halmashauri ya Makanisa ya Ulimwengu yenye makao yake makuu nchini Switzerland na ambayo ina washiriki milioni 50 Uhabeshi na milioni 2.5 Eritrea, ilishindwa kuyapatanisha mataifa hayo mawili mwezi wa Septemba 2017. Kulingana na Gazeti la The EastAfrican lenye makao makuu jijini Nairobi, juhudi zaidi za Idara ya Marekani ya Masuala ya Nje, Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika hazikufua dafu.

“Mkataba wa Amani wa hivi karibuni utajaribiwa katika miezi ijayo,” anaeleza Martin Plaut, ambaye ni mtafiti mwandamizi, Upembe wa Afrika na Kusini mwa Afrika katika Taasisi ya Masomo ya Madola (Institute of Commonwealth Studies in the United Kingdom), Uingereza. Plaut anaongeza kuwa, “Ili juhudi za amani zidumu, ni sharti Uhabeshi na Eritria zikamilishe mabadiliko ya ndani ya nchi.”

Juu ya hayo anasema kwamba, “Waziri Mkuu wa Uhabeshi, Abiy [Ahmed] ameipigisha Uhabeshi hatua kubwa za mageuzi, bali Eritrea bado inahitajika kufanya mengi. Uimarishaji wa demokrasia na ujenzi wa ndani wa amani utahitajika ikiwa kasi kubwa ya mabadiliko itadumishwa katika eneo hilo la Upembe wa Afrika.”

Daniel Otieno
More from this author