AV

Uganda yaongoza katika kuwakaribisha wakimbizi kwa mikono miwili

Get monthly
e-newsletter

Uganda yaongoza katika kuwakaribisha wakimbizi kwa mikono miwili

Nchi hii ina idadi kubwa zaidi ya wakimbizi Barani Afrika
Sulaiman Momodu
5 February 2019
Refugee students in a classroom in Uganda. Photo: UN Photo/Mark Garten
Photo: UN Photo/Mark Garten
Wanafunzi wa Wakimbizi katika darasa la Uganda. Photo: UN Photo/Mark Garten

Huku maelfu ya wanaume, wanawake na watoto waliotamauka wanapotoroka mizozo na majanga asilia na kutafuta maeneo salama, baadhi ya mataifa yanajadili ikiwa yatawakubali au kuwakataa wakimbizi. Hata hivyo, nchi ya Uganda imekaribisha idadi kubwa mno ya wakimbizi.

Robert Yatta mwenye umri wa miaka kumi na tatu alikuwa akisoma huku akiishi na shangazi yake katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba vita vilipozuka mapema mwaka wa 2017.

“Tuliamshwa na milio mikali ya risasi usiku mmoja,” alikumbuka wakati akihojiwa na Africa Renewal. “Shule zilifungwa na tukafungiwa nyumbani kwa juma moja kabla ya kutorokea kambi ya wakimbizi ya Bidi Bidi Kaskazini mashariki mwa Uganda.” Kambi hiyo ina wakimbizi zaidi ya robo milioni.

Kambi ya Bidi Bidi ilipokea maelfu ya wakimbizi kila siku wakati vita vilifikia kilele nchini Sudan Kusini mnamo mwaka 2016. Kambi hii yenye ukubwa wa kilomita 234 mraba inatumiwa kwa shughuli za makazi na kilimo. Ukubwa wake ni takriban jiji nzima la Birmingham, Uingereza.

“Maisha ni mazuri hapa Uganda,” anasema Yatta, japo ametengana na wazazi wake. “Ninaenda shuleni tena.”

Kijana huyu ni miongoni mwa wanafunzi werevu mno darasani mwake. Anazungumza Kiingereza kwa ufasaha na huwaelekeza kimasomo wenzake pamoja na vijana wa umri mkubwa kuliko wake.

Nchi yenye wakimbizi wengi zaidi barani Afrika

Japo ni nchi maskini, Uganda ina idadi kubwa zaidi ya wakimbizi barani Afrika. Ina zaidi ya wakimbizi milioni moja, wengi wakiwa ni kutoka Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Burundi na Somalia. Nchi za Kenya, Sudan, DRC na Uhabeshi pia zina idadi kubwa ya wakimbizi barani Afrika.

Mnamo mwaka 2018, Tume ya Umoja wa Mataifa kuhusu Wakimbizi (UNHCR) ilitangaza kwamba kuna wakimbizi milioni 68.5 ulimwenguni, ikiwa ni pamoja na wakimbizi wa ndani kwa ndani milioni 40. Mataifa yanayoendelea, hasa katika bara Afrika, ni wenyeji kwa 85% ya wakimbizi.

Mugisha Willent, mkimbizi wa miaka 26 kutoka DRC, alikumbuka namna alivyokimbia Goma mwaka wa 2000. “Nililolijua ni kwamba vita vilikuwa vikiendelea. Hivi sasa Uganda imetupa amani, mashamba na mengine mengi. Uganda ni nyumbani,” aliambia Africa Renewal.

Bi. Willent alikuwa miongoni mwa wanawake watatu walioshinda Tuzo ya Sauti za Ujasiri (Voices of Courage Award) kutoka kwa Ubalozi wa Wanawake Wakimbizi jijini New York mwaka wa 2018.

Akiwa nchini Uganda, yeye huwasiadia wasichana wasioenda shule, kina mama wachanga na wahanga wa dhuluma za kijinsia. Yeye hufanya kazi pia kama balozi wa vijana wa UNHCR na hivi karibuni alihutubia kikao cha Umoja wa Mataifa huko Geneva kwa niaba ya wanahirimu wake wa Uganda akipigia debe haja ya wakimbizi kutembelea maeneo yote katika nchi wenyeji bila vizuizi, uhuru wa kuwa na stakabadhi za usafiri wa kimataifa na usawa wa karo ya wanafunzi wakimbizi na wenyeji katika nchi husika.

Makaribisho kwa mikono miwili

Idadi ya wakimbizi nchini Uganda imekuwa ikiongezeka kuanzia mwaka wa 2013. Takribani wakimbizi 200 huwasili nchini humo kila siku kwa sasa.

“Uganda imeendelea kuwakaribisha wakimbizi kwa mikono miwili na wala haimzuii yeyote anayetafuta hifadhi kwetu. Hii ni kwa kufuatia utamaduni wa Kiafrika wa ukarimu,” anasema Hilary Onek, Waziri wa Misaada, Ukabilianaji na Majanga, na Wakimbizi wa Uganda.

Akihuhutubia mkutano wa Kamati ya Utendakazi ya UNHCR mnamo Oktoba, Bwana Onek alitaja kwamba serikali yake inaendelea kudumisha sera ya kuwakaribisha wakimbizi licha ya changamoto zinazoikabili.

Benki ya Dunia inaeleza kwamba uchumi wa Uganda unakua kwa asilimia ndogo ya 4.5% siku za hivi karibuni na kwa hivyo kupunguza athari zake katika juhudi za kuangamiza umaskini. Katika miaka ya 1990 na mapema miaka ya 2000, uchumi ulikua kwa 7%.

Wataalamu wa masuala ya ubinadamu wanaipongeza Uganda kwa sera yake ya kuwakaribisha wakimbizi kama hatua ya ukarimu wa hali ya juu duniani. Mkakati wa serikali huyajumuisha masuala ya wakimbizi katika mfumo wa mipangilio ya kitaifa.

“Ni muhimu kwa jamii ya kimataifa kutambua kwamba Uganda imekuwa na sera ya kuigwa juu ya wakimbizi tangu siku za awali kufikia sasa. Ingawa ilikabiliwa na ongezeko kubwa la wakimbizi mwaka jana, Uganda imesalia mfano mzuri wa uadilifu na mfumo bora wa kuwalinda wakimbizi ambao kwa bahati mbaya hauheshimiki kote duniani,” Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres alisema mwezi wa June 2017.

Sera ya wakimbizi ya Uganda inawahakikishia uhuru wa kutembea na haki ya kuajiriwa, ya elimu na ya afya, pamoja na haki ya kuanzisha biashara. Serikali pia inawapa wakimbizi vipande vya mashamba ili waweze kukuza mazao na kujenga makazi. Inawawezesha wakimbizi kujitegemea kiuchumi, na wakati uo huo kuwahakikishia haki wazipatazo raia wake.

Angèle Dikongué-Atangana, naibu Mkurugenzi wa UNHCR wa eneo la Mashariki na Upembe wa Afrika anawakumbusha wahakiki kwamba wakimbizi wana maarifa na ujuzi wa kuchangia katika mataifa wenyeji.

“Katika nchi ya Uganda, baadhi ya wakimbizi wameanzisha biashara na kuwaajiri raia, ilhali wengine wanachangia katika kuzalisha chakula kupitia shughuli mbalimbali za kilimo. Isitoshe, wengine wanafanya kazi kama wataalamu,” alisema Bi Dikongué-Atangana, akithibitisha kwamba wakimbizi wanaweza kuchangia sana katika maendeleo ya mataifa wenyeji kama wakipewa nafasi.

Mnamo Juni 2018, Robert Hakiza, mkimbizi wa asili ya Kongo anayeishi Uganda alikiambia kikao cha mashauriano ya Mashirika ya kibinafsi ya UNHCR huko Geneva kwamba shirika aliloanzisha kwa ushirikiano na wenzake­­ - Shirika la Vijana Wakimbizi Waafrika kwa Maendeleo Muhimu (—lilikuwa likisaidia kuwawezesha wakimbizi na wakati uo huo kuchangia jamii ya wenyeji wao. YARID, yenye kaulimbiu “Wakimbizi wanaweza kulazimika kuondoka nyumbani kwao, lakini hawaachi ujuzi na maarifa yao huko,” hutoa nafasi kwa wakimbizi na jamii wenyeji kukutana, kujadili changamoto na kutafuta masuluhisho kwa pamoja.

“Kuwafungia wakimbizi mipaka sio suluhisho. Miongoni mwao kuna madaktari, mawakili na wataalamu wengine waliofuzu kutoka vyuo vikuu ambao wanaweza kuchangia jamii zinazowakirimu pakubwa,” asema Bwana Hakiza.

Mfano wa kuigwa

Akizungumza na Africa Renewal, Mkurugenzi wa Afrika wa UNHCR, Valentin Tapsoba, alisema, “Msaada wa Uganda kwa wakimbizi unastahili kupongezwa, kwa kuwa wana sera endelevu ya kuwapokea wakimbizi. Tunajaribu kuyahimiza mataifa mengine kuiga mfano huo wa Uganda.”

“Ukarimu wa Afrika kwa wakimbizi ni wa ajabu. Mataifa ya Afrika yanafungua mipaka na mioyo yao kuwapokea wakimbizi. Jamii wenyeji wa wakimbizi zinawakaribisha wakimbizi hata kabla ya UNHCR na jamii ya kimataifa kusaidia.

Bwana Tapsoba alisema kuwa angependa kuona mchango zaidi kwa jamii wenyeji za wakimbizi kutoka kwa jamii ya kimataifa na akaonya kwamba udhamini duni huathiri usalama wa wakimbizi, utoaji chakula, hudumua za kiafya, makazi, na elimu miongoni mwa huduma nyinginezo.

Kulingana na taarifa ya UNHCR, kwa kuzingatia michango iliyotolewa, ufadhili wa mwaka wa 2018 unatarajiwa kuwa 55% pekee ya dola bilioni 8.2 zinazohitajika. Ufadhili huu unalinganishwa na 56.6% mwaka wa 2017 na 58% mwaka wa 2016. Kufikia mwezi wa Oktoba 2018, ufadhili kwa Uganda ulikuwa 42% pekee ya jumla ya bajeti iliyohitajika.

Huku ufadhili ukisalia kuwa changamoto kubwa, bwana Tapsoba anataja kwamba UNHCR inashirikiana na washirika wengine kuwezesha mamia ya wakimbizi kurejea makwao kwa hiari yao. Anasema Tapsoba, “Kuna mipango inayoendelea ya kuwarejesha nyumbani wakimbizi wa Kodivaa, Somalia, Msumbiji, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.”

Mbali na shughuli zake nchini Uganda, UNHCR inaangazia masaibu ya maelfu wanaohatarisha maisha yao kwa kuthubutu kujaribu kuvuka Saheli ili kuingia Libya na Bahari ya Mediterania kwa nia ya kuingia bara Ulaya. UNHCR inashirikiana na baadhi ya serikali pamoja na Shirika la Kimataifa Kuhusu Uhamiaji, kitengo cha Umoja wa Mataifa cha uhamiaji, kuokoa na wakati mwingine kukipa kikundi kama hiki makao mbadala.

Visababishi vikuu vya ukimbizi

Afisa Mkuu Mtendaji wa Benki ya Dunia, Kristalina Georgieva, anasema kwamba umaskini, mizozo na majanga asilia pamoja na mabadiliko ya hali ya anga ndivyo vyanzo vikuu vya kuhama kwa watu kutoka makwao. Benki ya Dunia itatumia dola bilioni 2 kati ya Julai 2017 na Juni 2020 kuwasaidia wakimbizi wa Afrika chini ya mpango wake wa Muungano wa Maendeleo wa Kimataifa.

Wataalamu wa maendeleo wanaamini kwamba kuzuia ni muhimu sana katika kusuluhisha tatizo la ukimbizi na uhamiaji. “Njia bora ya kuikabili hatari ya kibinadamu ni kutokuwa nayo,” anasisitiza Bi. Georgieva.


Sulaiman Momodu ni Afisa anayeripotia UNHCR.

Mada: 
Sulaiman Momodu
More from this author