AV

Walioshambulia ndege na pia kuua wawili akiwemo mtoto wa umri wa miaka mitano, wafikishwe katika mikono ya sheria-Kallon

Get monthly
e-newsletter

Walioshambulia ndege na pia kuua wawili akiwemo mtoto wa umri wa miaka mitano, wafikishwe katika mikono ya sheria-Kallon

UN News
7 July 2020
By: 
Gari za UN zilizoharibiwa wakati washambulizaji wenye silaha waliposhambulia mji wa Monguno katika jimbo la Borno, Nigeria.
UN Nigeria
Gari za UN zilizoharibiwa wakati washambulizaji wenye silaha waliposhambulia mji wa Monguno katika jimbo la Borno, Nigeria.

Mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Nigeria, Edward Kallon ameeleza kusikitishwa na taarifa za mashambulizi yaliyotekelezwa na makundi yasiyo ya kiserikali katika eneo la Damasak jimbo la Borno nchini Nigeria mwishoni mwa wiki iliyopita tarehe 2 Julai.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya misaada ya kibinadamu,OCHA , mashambulizi hayo yaliwaua watu wawili akiwemo mtoto wa umri wa miaka mitano. Watu wengine walijeruhiwa na pia helikopta ya misaada ya kibinadamu ilishambuliwa na kuharibiwa sana

“Ninatuma salamu za rambirambi kwa familia za raia ambao wamepoteza maisha katika shambulizi na ninawatakia majeruhi, kupona haraka.”Amesema Bwana Kallon

Bwana Kallon amesema anakaribisha ahadi ya serikali kuchunguza shambulizi hilo na kuwaleta katika mikono ya sheria waliotekeleza tukio hilo baya.

Aidha Bwana Kallon amewapongeza maafisa waliookoa helikopita iliposhambuliwa,“ninalaani kuwa helikopita ya kutoa huduma za anga za kibinadamu ilipigwa risasi wakati wa shambulizi. Hakuna mfanyakazi wa misaada aliyekuwa katika helikopita na maafisa wote wako salama. Fikira zangu pia ziko kwa marubani wa helikopita hiyo na ninawapongeza kwa kuindesha na kuirejesha katika eneo salama hata katika hali hiyo ya hatari. Shambulizi na uharibifu wa helikoputa unaathiri vibaya uwezo wa watoa misaadakutoa usaidizi wa haraka kwa watu walioko hatarini kwenye maeneo ya ndani kote katika jimbo la Borno”

Huduma ya misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa kwa njia ya anga ni ya muhimu kuwahamisha raia waliojeruhiwa na inasalia kuwa uti wa mgongo kusaidia watoa misaada, mashirika ya Umoja wa Mataifa na mashirika yasiyo ya kiserikali kufika wanakotaka kwenda hasa katika maeneo ya watu waliko hatarini. Shirika la huduma za kibinadamu zinazotolewa na shirika la ndege za Umoja wa Mataifa (UNHAS), zilisafirisha abiria 66,271 na uokoaji wa kiusalama 70 na ule wa kiafya mara 30.