AV

Sudan Kusini, Sudan, CAR, Libya na Haiti kunufaika na ufadhili wa OCHA/CERF

Get monthly
e-newsletter

Sudan Kusini, Sudan, CAR, Libya na Haiti kunufaika na ufadhili wa OCHA/CERF

UN News
24 June 2020
By: 
Wanawake na watoto waliotawanywa kutokana na mapigano Jebel Marra, Darfur Kaskazini, wakijihifadhi katika kituo kipya cha Tawilla
OCHA
Wanawake na watoto waliotawanywa kutokana na mapigano Jebel Marra, Darfur Kaskazini, wakijihifadhi katika kituo kipya cha Tawilla

Taarifa iliyotolewa hii leo na ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia misaada ya dharura, OCHA imeeleza kuwa Mratibu Mkuu wa misaada ya dharura ya kibinadamu kwenye Umoja wa Mataifa ambaye pia ni mkuu wa, Mark Lowcock, hii leo ameachia dola za kimarekani milioni 25 kutoka mfumo mkuu wa dharura wa Umoja wa Mataifa, CERF kwenda kwa shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji, IOM ili kusaidia mashirika yasiyo ya kiserikali yaliyoko mstari wa mbele katika kutoa hudua ya afya ya kuokoa maisha, huduma za maji na za kujisafi katika mapambano dhidi ya COVID-19 katika Jamhuri ya Afrika ya kati, Haiti, Libya, Sudan Kusini na Sudan.

Ufadhili huu kwenda katika nchi mbalimbali utagawanywa kwa mashirika yasiyo ya kiserikali, NGOs kwa ngazi ya kitaifa ili kusaidia mahitaji muhimu ya kibinadamu katika vipaumbele vya nchi vya kiafya ikiwemo afya ya akili na msaada wa kisaikolojia, maji, vifaa na mahitaji mengine ya kujisafi. Msisitizo utaelekezwa zaidi kwa masula ya jinsia ikiwemo unyanyasaji wa kijinsia na mahitaji ya watu wanaoishi na ulemavu.

Mark Lowcock, amesema, “tunapopambana na COVID-19 katika nchi ambazo tayari zinakabiliana na majanga ya kibinadamu, kazi ya wafanyakazi walioko mstari wa mbele ni muhimu zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Kwasababu yao, watu walio katika uhitaji mkubwa wa maji safi na salama ya kunywa, huduma za afya na kujisafi, ambayo ni mahitaji ya msingi unayoyahitaji kupambana na virusi vya corona, wanayapata, popote walipo.”

Naye Mkurugenzi Mkuu wa IOM, Antonio Vitorino amepokea taarifa hiyo kwa kusema, “ushirikiano wetu imara na OCHA na CERF unaturuhusu kuendeleza usaidizi kwa mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo yako mstari wa mbele katika janga la COVID-19 kote duniani. Ufadhili huu unaimarisha juhudi za kufanya kazi bega kwa began a mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo ni muhimu katika kushughulikia huduma za kibinadamu.”

Tangu kuundwa kwake, CERF imetoa misaada ya kibinadamu ya kufikia dola bilioni 6.5 kwa mamilioni ya watu kote katika zaidi ya nchi 100. Hili lisingewezekana kama si ukarimu na misaada kutoka maeneo mbalimbali.