AV

Kutana na Gertrude Mongella, mwenye umri wa miaka 75 kutoka Tanzania aliyeongoza ulimwengu katika kongamano la kihistoria la wanawake jijini Beijing'

Get monthly
e-newsletter

Kutana na Gertrude Mongella, mwenye umri wa miaka 75 kutoka Tanzania aliyeongoza ulimwengu katika kongamano la kihistoria la wanawake jijini Beijing'

Stella Vuzo
Afrika Upya: 
29 October 2020
Gertrude Mongella (katikati), Katibu Mkuu wa Mkutano wa Nne wa Dunia juu ya Wanawake, kwenye ...
UN Photo/Evan Schneider
Gertrude Mongella (katikati), Katibu Mkuu wa Mkutano wa Nne wa Dunia juu ya Wanawake, kwenye hafla ya chakula cha mchana iliyofanyika kwa waandishi wa habari kuhusu Mkutano wa Nne wa Dunia wa Wanawake unaokuja. (Beijing, China, 4-15 Septemba 1995).

Bi. Gertrude Mongella kutoka Tanzania alikuwa Katibu Mkuu wa Kongamano la Nne la Umoja wa Mataifa kuhusu Wanawake lililofanyika Beijing', Uchina mwaka wa 1995. Walienda, walijionea, walishinda na wameishi kusimulia hadithi....miaka 25 baadaye. Alizungumza na Stella Vuzi wa Umoja wa Mataifa kuhusu mawazo yake juu ya Umoja wa Mataifa unapofika miaka 75 pia.

Mama wa Beijing' angali anatetea haki za wanawake

Je, Gertrude Mongella ni nani?

  • Bi. Mongella alizaliwa Septemba 1945 katika kisiwa kidogo katika Ziwa Viktoria nchini Tanzania.
  • Ni mwanaelimu, mtetezi wa haki za wanawake, mwanasiasa na mwanadiplomasia.
  • Alitumikia Ofisi ya Waziri Mkuu akiwajibikia Masuala ya Wanawake kuanzia mwaka wa 1982 hadi 1985. Alikuwa Mbunge katika Bunge la Tanzania, na pia katika Bunge la Afrika Mashariki na hatimaye Bunge la Afrika.
  • Mnamo 1993-1995, kama mwanadiplomasia wa Umoja wa Mataifa aliongoza Kongamano la Nne la Ulimwengu kuhusu Wanawake kama Katibu Mkuu na Mwenyekiti, ambapo alichangia pakubwa kufanikisha kongamano hilo na tangu hapo amejulikana kama "Mama Beijing".
  • Gazeti la Courier kwa wakati huo liliandika ripoti kuwa ''nguvu za ajabu'' za Bi. Mongella zilichangia pakubwa kufanikiwa kwa kongamano la Beijing'. Gazeti hilo lilitoa ripoti kuhusu kujitolea kwake na moyo wa mama (ulioficha uthabiti wake), kulisaidia katika masuala magumu wakati wa kongamano hilo. Alilazimika kupatanisha wale ambao hawangeweza kupatanishwa:kujaribu kuleta mataifa yaliyokuwa katika pande pinzani katika mkondo wa maadili ili kukubaliana kuhusu maazimio ya mwisho.
  • Isitoshe, ni maazimio ambayo, kwa mara ya kwanza katika jukwaa la kidiplomasia la kimataifa, yalishughulikia masuala nyeti kama ujinsia wa wanawake. Ungeweza kuhisi wasiwasi wake, hata wakati alijibu kwa tabasamu kwamba yote yanaendelea vyema.
  • Bi. Mongella alikuwa 'Mama' wa kongamano la Beijing, na ni mmoja wa wavumbuzi wa diplomasia ya wanawake ambayo Beijing itakumbukwa kwayo kwa muda mrefu. Ilikuwa mara ya kwanza ulimwenguni ambapo maamuzi muhimu kwa kiwango hiki yaliwahi kuchukuliwa na jukwaa ambalo takribani washiriki wake wote walikuwa wanawake.
  • Uvumilivu, uthabiti, kuheshimu maoni ya kila mtu na unyenyekevu zilikuwa sifa kuu za diplomasia hii na sifa hizi zote alikuwa nazo Bi. Mongella.
  • Amejitolea sana katika umoja wa kisiasa wa Afrika, pamoja na kutetea ushiriki mkubwa wa wanawake katika uongozi wa kisiasa.

Tafadhali tufahamishe kidogo kukuhusu?

Mimi ni Gertrude Mongella, maarufu hapa Tanzania kama 'Mama Beijing' kwa sababu ya jukumu nililotekeleza kama Katibu Mkuu wa Kongamano Kuu la Umoja wa Mataifa la Wanawake huko Beijing mwaka wa 1995.

Nilikuwa na wakati mzuri huko nikijitayarisha juu ya kongamano hilo. Nilikuja kuelewa na kuthamini zaidi Umoja wa Mataifa, majukumu yake na wajibu unaotekeleza ulimwenguni.

Ulifikisha miaka 75 mwaka huu. Umoja wa Mataifa pia umetimiza miaka 75. Je, tajriba yako katika Umoja wa Mataifa ni gani?

Nina furaha sana leo, kwanza kwa sababu niko hai. Nafurahia ukweli kwamba nilinusurika wakati wa kuzaliwa nikiwa mtoto wa kike kwa sababu wakati nilipozaliwa, miaka 75 iliyopita, watoto wengi wa kike hawakunusurika. Nilizaliwa katika kisiwa kimoja katika Ziwa Victoria, kisha nikaenda kupata elimu katika Tanzania bara.

Nilizaliwa mnamo Septemba 1945 na Umoja wa Mataifa ulianzishwa mwezi mmoja baadaye mnamo Oktoba 1945. Sijui ikiwa mama yangu alijua kwamba wakati alikuwa akileta ulimwenguni mtoto huyu wa kike, shirika muhimu pia lilikuwa linaanzishwa. Ninajivunia kuwa sehemu ya Umoja wa Mataifa. Ninajivunia kuwa raia wa kimataifa ulimwenguni.

Kushiriki kwangu katika masuala na hafla za Umoja wa Mataifa kulinifunulia ulimwengu na kupanua mawanda yangu. Kulinikuza na kunifanya kuwa na uwezo wa kuvumilia wengine, hata tunapotofautiana. Nimepata nafasi ya kusafiri kote ulimwenguni, ikiwemo kwenda Beijing, ambapo nilikutana na watu wengi kutoka tamaduni tofauti na nilipata kujengeka sana. Ningependa kusema kwamba Umoja wa Mataifa ni muhimu kwa sababu umewaleta pamoja watu wa mataifa tofauti. Uanachama wa Umoja wa Mataifa umekua zaidi hadi kujumuisha wanachama ambao hawakuwepo wakati wa kuanzishwa kwake, pamoja na wale wanaotoka Afrika.

Je, unaweza kusema mafanikio matatu muhimu ya kongamano la Beijingnni yapi?

Kwanza, kongamano hilo lilileta mojawapo ya idadi kubwa zaidi ya wajumbe ambayo haikuwahi kuonekana popote ulimwenguni. Karibu watu 15,000 walikutana Beijing kujadili masuala yanayowahusu wanawake. Inabakia kuwa mojawapo ya makongamo makubwa zaidi.

Pili, kongamano hilo lilifanya masuala ya usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake kuangaziwa ulimwenguni. Lilileta aina ya 'mapinduzi' ambapo inabidi tuwachukulie wanawake na wanaume kama raia sawa wa ulimwengu huu. Wanawake hawafai kuchukuliwa kama 'waalikwa' kwenye sayari hii. Wanawake wanatoka katika sayari hii kama walivyo wanaume. Jukwaa la Utekelezaji ambalo lilipitishwa Beijing mwishoni mwa kongamano hilo ni waraka muhimu sana ambao nimewahi kuupata katika maisha yangu. Kushiriki kwangu kulikuwa taadhima hasa kuhusika katika kubuni waraka huu, pamoja na wengine kutoka kote ulimwenguni.

Tatu, Umoja wa Mataifa umesaidia kuinua hadhi na heshima ya wanawake katika mawanda ya kiulimwengu.

Gertrude Mongella, Secretary-General of the Conference
Kikao cha ufunguzi wa Mkutano wa Nne wa Dunia kuhusu Wanawake huko Beijing. Gertrude Mongella (wa pili kushoto), Katibu Mkuu wa Mkutano huo. Picha: UN Photo/Milton Grant

Je, maoni yako kuhusu Ajenda 2030 ya maendeleo endelevu ni yapi?

Tunahitaji kufanya kazi pamoja kuitekeleza. Tunahitaji kushirikiana na wanaume, hatuwezi kufikia mafanikio mengi peke yetu. Hatupaswi kuwaacha wanaume nyuma kwa sababu kuna hatari tukiwatenga wanaume. Tunapaswa kujitahidi kila wakati kuwaelimisha wanawake na kuwawezesha kiuchumi.

Stella Vuzo
More from this author