Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipokubali kwa kauli moja Azimio 1325 kuhusu wanawake, amani na usalama kwa mara ya kwanza miaka ishirini iliyopita, kilikuwa kilele cha miaka mingi ya uanaharakati na kazi ya vikundi vya kiraia, mataifa, na wengine wengi.
Azimio hilo linasisitiza wajibu muhimu unaotekelezwa na wanawake katika uzuiaji na usuluhishaji wa mizozo, na kudai uwakilishi sawa katika michakato ya kukuza amani.
Namibia ilishikilia Urais wa Baraza hilo la wanachama 15 mnamo Oktoba 2000 Azimio hilo lilipopitishwa. Namibia pamoja na Mali na Tunisia iliwakilisha bara Afrika katika baraza hilo la Umoja wa Mataifa.
Balozi Selma Ashipala-Musavyi alikuwa Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Namibia katika Umoja wa Mataifa wakati huo na alikuwa katika kitovu cha majadiliano hayo. Anakumbuka hisia katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
“Kufuatia utambulisho wa hiyo mada [kuhusu wanawake, amani na usalama], kilichofuatia ilikuwa dakika nzima ya kimya, ikifuatiwa na mseto wa kicheko, mshangao wa wazi pamoja na kejeli na dhihaka”.
Bi. Ashipala-Musavyi, aliyestaafu kutoka kwa wadhifa wa Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Masuala ya Kigeni na Ushirikiano, anayakumbuka haya, na kusema, “sio kwa nia ya kujigamba, bali kuonyesha kwamba Azimio 1325 halikupatikana kwa urahisi.”
“Hisia ya wakati huo ilikuwa kwamba mada hiyo [wanawake, amani na usalama] haikuwa na nafasi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, bali ilistahili kujadiliwa katika Kamati ya Tatu ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa,” anasema, kuonyesha majadiliano makali yaliyofungamana na mchakato wa kupitisha azimio hilo.
“Hata hivyo, kwa sababu ya shinikizo kutoka kwetu, na msukumo kutoka kwa asasi za kiraia, pamoja na Mataifa mengine Wanachama, katika kundi letu, Baraza la Usalama, hatimaye liliijadili mada hiyo. Azimio 1325 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) lilikubaliwa na mengine sasa ni historia.”
- Azimio 1325(2000) la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
- Brochure: Women Transforming AV:
Safari ilianzia Beijing
Ulimwengu ulipojumika katika jiji la Beijing nchini Uchina, kwa Kongamano la Nne kuhusu Wanawake mnamo 1995, hatua muhimu ya mageuzi ya ajenda ya kimataifa kuhusu usawa wa kijinsia ilifikiwa na maswala ya wanawake kudhihirika wazi.
Kwa Namibia, miaka mitano tu baada ya uhuru wake wakati huo, hii ilikuwa fursa muhimu mno kwa taifa hilo kuhusika kama taifa huru na kugeuza mwelekeo wa kitaifa kuhusu kuwawezesha wanawake wa Namibia.
Hisia hii ilichochea kampeni ya Namibia kujiunga na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwaka wa 1999. Likiwa limeamua kuhalalisha kanuni za Kongamano la Beijing, taifa la Namibia lilijitolea kutoa mchango chanya na wa kudumu kwa amani ya kimataifa, likiongozwa pia na harakati zake za kujikomboa na katiba iliyojadiliwa kutokana na hiyo historia yake.
Huku tajriba ya Namibia katika mzozo ikidhihirisha kwamba aghalabu wanawake ni miongoni mwa wahasiriwa wakuu wa vita, mizozo, na ukosefu wa usalama, ilionyesha pia kwamba wanawake walikuwa muhimu sana katika harakati za ukombozi, wakiwa walimu, madaktari, wapiganaji na hata washirikkatika meza za majadiliano.
Mwaka wa 1999, ujumbe wa Namibia katika Umoja wa Mataifa ulielewa wajibu wa wanawake kama washirika muhimu katika kukuza na kudumisha amani na usalama wa kimataifa, na hivyo hawastahili kuzingatiwa tu kama ‘wahasiriwa’.
Kufikia wakati huo, urejelezi kwa wanawake katika stakabadhi za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, uliwaona zaidi kama wahasiriwa wa ubakaji, au katika majadiliano ya ubakaji kama silaha ya kivita. Hapakuwa na mapendekezo au matarajio kuhusu uwezo wa wanawake katika uzuiaji, usuluhishaji na utatuzi wa mizozo.
Namibia iliamini kwamba ulimwengu ulikuwa tayari kutambua wajibu kwa wanawake katika kuchangia michakato ya amani kupitia ajenda mahususi, iliyobuniwa kwa kuzingatia tajriba za kikanda na za kimataifa za wanawake, iliyolichochea kupigia debe Azimio 1325.
Taifa la Namibia limesalia katika mstari wa mbele wa nia hii, na mwanachama mwasisi wa Women, AV and Security Focal Points Network iliyozinduliwa mwaka wa 2016, kwa lengo msingi la kutekeleza Ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama (WPS) katika kiwango cha kitaifa.
Mipango ya 2020
Ili kuadhimisha miaka 20 ya kukubaliwa kwa Azimio 1325 la UNSC na kuendeleza kujitolea kwa wanawake katika amani na usalama, Namibia itazindua Kituo cha Wanawake cha Kimataifa cha Amani katika jiji kuu, Windhoek, tarehe 31 Oktoba 2020.
Kituo hicho kitakuwa taasisi ya ubora ya upatanishi na uzuiaji mizozo, kuwasidia wanawake na kukuza ujuzi unaokusudia kuchangia mustakabali wa mwanadamu.
Katika miongo mitatu iliyopita, Namibia imepigia debe usawa wa kijinsia, ikiwa ni pamoja na kutekeleza sheria na sera za kutoa nafasi sawa kwa wanawake na wanaume.
Namibia imefanya maamuzi makuu, ikiwa ni pamoja na wakati ambapo chama tawala cha kisiasa kilipoanzisha mpango wa uimarishaji usawa wa kijinsia, ambao umezoelewa katika siasa za kitaifa, na kuchangia uwakilishi wa wanawake katika bunge la kitaifa kuwa asilimia 47.
Hili pia limeleta manufaa kama vile ongezeko la idadi ya wasichana wanaosajiliwa katika shule za msingi na za upili, na kuimarisha idadi ya wanawake katika sekta ya kibinafsi.
Aidha, hatua zimepigwa katika kuzijumuisha sera zinazolenga masuala ya kijinsia na ufahamu katika mipango ya kitaifa na uundaji wa bajeti, pamoja na kuwapa maafisa mafunzo, na kupigania ujumuishwaji wa wanawake katika nafasi za kufanya maamuzi na uongozi wa kisiasa kwa jumla.
Bado kuna Changamoto
Licha ya ufanisi huu katika kutimiza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake, suala la dhuluma za kijinsia bado linatia wasiwasi na ubunifu unahitajika ili kuhakikisha kwamba wanawake wanaweza kuutekeleza wajibu wao kama mawakala wa amani katika ngazi za kijamii na kitaifa.
Mengi yanastahili kufanywa ili kuupanua ushiriki wa wanawake katika michakato ya amani, Kimataifa, pamoja na kikanda na kitaifa, ikiwa ni pamoja na kuwapa mafunzo wanawake wapatanisha, na kupigania hatua za usawa wa kijinsia kama vitu muhimu kwa sera za usalama na desturi.
Japo mengi katika Jukwaa la Hatua la Beijing (Beijing Platform for Action) ya 1995 yametekelezwa, mambo mengi yangali bado hayajatimizwa.
Katika ukumbusho huu wa miaka 20 wa azimio hili muhimu kuhusu wanawake, amani na usalama, sote tunastahili kuihamasisha jamii ya kimataifa kukumbatia kikamilifu wajibu muhimu ambao wanawake wanaweza na wanautekeleza kwa amani na usalama kila mahali.