AV

Zaidi ya watu 150 wauawa Ituri, DRC katika siku 40 zilizopita

Get monthly
e-newsletter

Zaidi ya watu 150 wauawa Ituri, DRC katika siku 40 zilizopita

UN News
20 April 2020
By: 
Kamishna Mkuu wa haki za binadamu, Michelle Bachelet alipotembelea Bunia, huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC mwezi Januari mwaka huu wa 2020
MONUSCO
Kamishna Mkuu wa haki za binadamu, Michelle Bachelet alipotembelea Bunia, huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC mwezi Januari mwaka huu wa 2020

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR, imesema inatiwa hofu kubwa na mauaji ya zaidi ya watu 150 katika maeneo ya Djugu na Mahagi kwenye jimbo la Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC

Mji wa Bunia katika jimbo la Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Maisha yanaendelea wakati huu ambapo ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa,inasema kuwa katika siku 40 zilizopita mashambulizi yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 150.

Mashambulizi hayo yanafanywa na watu waliojikita huko Djugu likiwemo kundi lililojihami la CODECO lenye idadi kubwa ya watu wa kabila la walendu,ingawa viongozi wa walendu wanadai kutohusika na vikundi hivyo.

Msemaji wa OHCHR Rupert Colville akizungumza na wanahabari kwa njia ya video amesema kuwa idadi hiyo ni pamoja na raia 107 waliouawa mwezi Machi pekee huku wengine 43 wakisalia majeruhi na kwamba idadi iliyobakia ya vifo ambayo ni 49 ni ya mwezi huu wa Aprili pekee.

Bwana Colville anasema kuwa mashambulizi ya raia yaliongezeka mwezi Machi huko Djugu baada ya kiongozi wa CODECO Ngudjolo Duduko kuuawa tarehe 25 ya mwezi huo wa Machi ambapo kikundi hicho kilijigawa katika makundi matano na kufanya mashambulizi,“Ukatili wa washambuliaji hao ambao wanatumia mapanga kuua wanawake na watoto, kubaka, kupora mali, kuharibu nyumba na kuua mifugo, unadokeza kuwa nia yao ni kuchochea hofu na kiwewe miongoni mwa jamii ili waweze kukimbia na wao watwae maeneo ambayo yana maliasili.”

Amesema kuwa licha ya ukatili huo, makabila yanayoathirika zaidi hususan wahema lakini pia Allur, Ndo Okebo na Mambisa, kwa kiasi kikubwa wamejizuia.

Hata hivyo amesema makabila hayo yana hofu kuwa iwapo mashambulizi yataendelea bila hatua kutoka vikosi vya usalama, yatalazimika kuunda kikundi chao cha mgambo ili kujibu mashambulizi, jambo ambalo linaweza kuchochea mapigano hayo ya kikabila.

Msemaji huyo wa OHCHR amerejelea ripoti yao ya mwezi Januari kuhusu mapigano ya kikabila kwenye jimbo hilo la Ituri akisema kuwa iwapo ghasia zitabainika kuwa zimepangwa ili kuathiri eneo kubwa ya jamii basi zinaweza kuwa uhalifu dhidi ya binadamu.

Ni kwa mantiki hiyo wametoa rai kwa mamlaka za DRC kuimarisha usalama kwa kupeleka vikosi na maafisa kwenye jimbo hilo ili kuchunguza pia madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu na wahusika wafikishwe mbele ya sheria.

Tangu kuanza kwa mwaka huu wa 2020, zaidi ya watu 334 wameathirika na mapigano ya kikabila katika jimbo la Ituri ambapo kati yao hao 206 wameuawa, 74 wamejeruhiwa na 54 wametekwa nyara.