AV

Walinda amani wanawake kutoka Tanzania wasema, "wanawake DRC wanafunguka zaidi kwetu kuelezea masahibu yao."

Get monthly
e-newsletter

Walinda amani wanawake kutoka Tanzania wasema, "wanawake DRC wanafunguka zaidi kwetu kuelezea masahibu yao."

UN News
1 June 2020
By: 
Sajini Tekla Kibiriti wa kikundi cha 7 cha kikosi cha TANZBATT 7 kilichoko kikosi cha kujibu mashambulizi cha MONUSCO, FIB, akitoa huduma ya afya kwa wanawake wakazi wa kata ya Matembo iliyoko Beni jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemorkasia ya
TANZABATT 7/Ibrahim Mayambua
Sajini Tekla Kibiriti wa kikundi cha 7 cha kikosi cha TANZBATT 7 kilichoko kikosi cha kujibu mashambulizi cha MONUSCO, FIB, akitoa huduma ya afya kwa wanawake wakazi wa kata ya Matembo iliyoko Beni jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemorkasia ya Congo, DRC.

Kuelekea siku ya walinda amani duniani kesho Mei 29, siku ambayo mwaka huu inamulika wanawake walinda amani wa Umoja wa Mataifa na mchango wao katika ujenzi wa amani ya kudumu, tunamulika askari wanawake wa Tanzania wanaohudumu katika kikosi cha saba cha kikosi cha kujibu mashambulizi, FIB cha ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Maudhui ya mwaka huu ni wanawake katika ulinzi wa amani: Ni ufunguo wa amani, yakilenga kuangazia miaka 20 tangu kupitishwa kwala Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalotaka harakati zote za ujenzi wa amani kwenye mizozo zijumuishe wanawake.

Ni kwa mantiki hiyo, FIB inajumuisha wanawake wakiwemo wale wa kikosi cha 7 cha Tanzania, TANZBATT 7 chenye makao yake makuu huko Beni jimboni Kivu Kaskazini.

Wanawake hao wanatoa huduma mbalimbali zikiwemo za afya, elimu na ujasiriamali.

Miongoni mwao ni Private Diana Mushi ambaye amesema katika kazi yake amejifunza madhara ya vita kwa wanawake, wajawazito, watoto na wazee na zaidi ya hapo,“tunakuwa tunawatembelea mara kwa mara na kusaidiana nao kimawazo, na kuelekezana katika ujasiriamali, na pia kutoa elimu kwa wazazi jinsi ya kuwalea watoto, na pia kuwaelimisha wanafunzi ili wasikate tamaa kulingana na hali iliyopo DRC”

Private Diana akaangazia pia umuhimu wa askari wa kike kwenye ulinzi wa amani akisema“Wanawake wa DRC wanaathirika na mambo mengi ambayo mengine wanashindwa kuzungumza na wanaume, inapaswa kuongea na wanawake wenzao tukiwemo sisi askari wa kike, na tumekuwa tunazungumza nao wanatuambia shida zao nyingi na sisi tunapeleka ujumbe ngazi za juu na kuweza kusaidiwa kulingana na matatizo yao.”

TANZBAT 7 ina jumla ya wanajeshi 949 wakiwemo askari wa kike 63. Kikosi hicho kinatekeleza majukumu yake kwa mwaka mmoja na kitakamilisha awamu yake mwezi Oktoba mwaka huu wa 2020.

Azimio namba 1325 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitishwa tarehe 31 mwezi Oktoba mwaka 2000.