AV

Walinda amani wa UN kutoka Chad wauawa katika shambulio Mali

Get monthly
e-newsletter

Walinda amani wa UN kutoka Chad wauawa katika shambulio Mali

UN News
12 May 2020
By: 
Kofia ya chuma ya buluu na vizibao mahsusi vya walinda amani wa Umoja wa Mataifa
UN/Marie Frechon
Kofia ya chuma ya buluu na vizibao mahsusi vya walinda amani wa Umoja wa Mataifa

Walinda amani watatu wa Umoja wa Mataifa kutoka Chad wameuawa siku ya Jumapili Kaskazini mwa Mali wakati msafara wao ulipokanyaga bomu lililotegwa barabarani karibu naeneo la Aguelhok kwenye jimbo la Kidal.

kwa mujibu wa taarifa ya mpango wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini, Mali , MINUSMA, bomu hilo pialimejeruhi walinda amani wengine wanne ambao sasa wanapatiwa matibabu.

Kufuatia shambulio hilo mkuu wa MINUSMA Mahamat Saleh Annadif amesema“nilazima tukusanye juhudi zetu kwa pamoja na kuwakamata magaidi waliohusika na shambulio ili waweze kujibu mashitaka ya uhalifu wao kwenye mkono wa sheria.”

Wakati akitoa heshima zake kwa walinda amani hao waliopoteza maisha wakiwa katika harakati za kuhakikisha amani ya kudumu inarejea Mali, mkuu huyo amelaani vikali shambulio hilo ambalo ameesma linalenga kutia dosari operesheni zinazoendelea kwa kulenga kwa makusudi raia na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres naye amelaani vikali shambulio hilo huku akituma salamu zake za rambirambi kwa familia , serikali na watu wa Chad kwa msiba huo mkubwa.

Ametoa wito kwa mamlaka nchini Mali kufanya kila juhudi katika kuwabaini wahusika ili wafikishwe mbele ya sheria, akikumbusha kwamba mashambulizi dhidi ya walinda amani huenda yakawa ni uhalifu wa kivita chini ya sheria za kimataifa.

“Vitendo hivyo vya kifedhuli havitoweza kuuzuia Umoja wa Mataifa kuendelea na dhamira yake ya kuwasaidia watu na serikali ya Mali katika kusaka amani na utulivu”ameongeza Guterres.

Nalo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeongeza sauti yake likilaani vikali shambulio hilo dhidi ya walinda amani wa MINUSMA. Wajumbe wa Baraza wamewatakia afueni ya haraka majeruhi na katika taarifa yao pia wamepongeza kazi ya walinda amani hao ambao wanahatarisha Maisha yao kila uchao ili kulinda ya wengine.

Wameitaka serikali ya Mali kufanya uchunguzi huru na wa kina na kisha kuwafikisha mbele ya sharia waliohusika na unyama huo.

Wamesisitiza kwamba kujihusisha katika kupanga, kuongoza, kufadhili au kuendesha mashambulizi dhidi ya walinda amani wa MINUSMA kunaweza kuwa msingi wa vikwazo ambavyo vinaweza kuwekwa na maazimio ya Baraza la Usalama.

Walinda amani kutoka Chad wakipiga doria katika mitaa ya Kidal nchini Mali.(maktaba Desemba 2016)
Walinda amani kutoka Chad wakipiga doria katika mitaa ya Kidal nchini Mali.(maktaba Desemba 2016)
MINUSMA/Sylvain Liecht