AV

Venezuela yaibwaga Costa Rica kwenye kinyang’anyiro cha ujumbe Baraza la Haki la UN

Get monthly
e-newsletter

Venezuela yaibwaga Costa Rica kwenye kinyang’anyiro cha ujumbe Baraza la Haki la UN

UN News
18 October 2019
By: 
Kikao cha baraza la haki la binadamu mjini Geneva.
UN photo/Jean Marc Ferré
Kikao cha baraza la haki la binadamu mjini Geneva.

Hii leo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limechagua wajumbe wapya 14 wa Baraza la haki za binadamu la umoja huo watakaoanza jukumu lao tarehe 1 Januari mwaka ujao wa 2020.

Katika kinyang’anyiro hicho kilichofanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani hii leo, macho na masikio yalielekezwa kwenye kanda tatu ambazo zilikuwa na zaidi ya wagombea kwa kulinganisha na nafasi zilizokuwa wazi.

Mathalani ukanda wa Amerika ya Kusini na nchi za Karibea, nafasi zilizokuwa wazi ni 2 huku wagombea wakiwa ni 3; Brazil Costa Rica na Venezuela.

Baada ya upigaji kura ya siri ambayo inataka mshindi apate kura 97, Brazil ilikuwa inasaka kuchaguliwa tena kuendelea kwa awamu ya pili ya miaka 3 huku Costa Rica na Venezuela wakitunishiana misuli, kila mmoja akitaka kumshinda mwenzake.

Hata hivyo Venezuela iliibuka mshindi na hivyo nafasi ya ukanda wa Amerika ya Kusini na Karibea kuchukuliwa na Brazil na Venezuela.

Libya, Mauritania, Sudan na Namibia, nchi kutoka Afrika ambazo zilikuwa zinawania nafasi 4 za ukanda wa Afrika zote zimepata kura za kutosha.

Ukanda wa Asia – Pasifiki ni Indonesia, Japan, visiwa vya Marshall na Korea Kusini waliibuka washindi huku Iraq ikishindwa kupata kura za kutosha.

Kwa mataifa ya Ulaya Mashariki wagombea walikuwa 3 kati ya nafasi mbili ambapo Armenia na Poland waliibuka washindi dhidi ya Moldova.

Ujerumani na Uholanzi zilikuwa zinawania nafasi mbili kuwakilisha mataifa ya Ulaya Magharibi na mengineyo na nchi zote mbili zilipata kura za kutosha.

Kwa mujibu wa azimio namba 60/215 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, mgawanyiko wa kikanda wa wajumbe 47 wa Baraza la haki za binadamu ni 13 kutoka Afrika, 13 kutoka Asia na Pasifiki, 6 kutoka mataifa ya Ulaya Mashariki, wajumbe 8 kutoka Amerika ya Kusini na Karibea na wajumbe 7 kutokamataifa ya Ulaya Magharibi na mengineyo.

Azimio hilo linasema kuwa mjumbe anahudumu kwa miaka mitatu kinachoweza kufanywa kwa awamu mbili na hatokuwa na haki ya kuchaguliwa tena papo hapo baada ya kumaliza awamu mbili za miaka mitatu mitatu.

Mataifa yanayomaliza ujumbe wao tarehe 31 mwezi Disemba mwaka huu ni Misri, Rwanda, Afrika Kusini, Tunisia, China, Iraq, Saudi Arabia, Croatia, Hungary, Brazil, Cuba, Iceland, na Uingereza.

Mada: