AV

UNHCR yapatiwa dola milioni 43 kusaidia wakimbizi katika mataifa manne

Get monthly
e-newsletter

UNHCR yapatiwa dola milioni 43 kusaidia wakimbizi katika mataifa manne

UN News
23 March 2020
By: 
Watoto wakimbizi wa ndani wakiwa kwenye hema lililochanika katika makazi ya wakimbizi wa ndani ya Abs nchini Yemen.
OCHA/Giles Clarke
Watoto wakimbizi wa ndani wakiwa kwenye hema lililochanika katika makazi ya wakimbizi wa ndani ya Abs nchini Yemen.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi,UNHCR, na mfuko wa masuala ya kibinadamu wa Thani Bin Abdullah Bin Thani Al-Thani huko Doha, Qatar leo wametiliana saini makubaliano ambapo mfuko huo utalipatia shirika hilo zaidi ya dola milioni 43.

Taarifa yailiyotolewa leo imesema mchango huo ni kiwango cha juu zaidi kwa shirika hilo kuwahi kupatiwa kwa mara moja na mtu binafsi na zitatumika kusaidia wakimbizi na wakimbizi wa ndani huko Yemen, Lebanon, Bangladesh na Chad.

Fedha zitasambazwa kupitia mikataba minne tofauti ambapo UNHCR inasema kuwa,“kwa mwaka wa pili mfululizo, mchango wa mkarimu huyo kutoka Qatar utasaidia mamilioni ya watu kupitia harakati za shirika hilo za kulinda na kupatia makazi wale wote waliofurushwa makwao.”

Akizungumzia mchango huo, Kamishna Mkuu wa UNHCR Filippo Grandi amesema kuwa msaada huo kutoka kwa Sheikh Thani Bin Abdullah umekuja kwa wakati na ni wa kiwango cha kutosheleza akisema kuwa,“utasaidia UNHCR kukidhi mahitaji ya wale wanaohitaji zaidi hasa waliokimbia na wale wanaowahifadhi katika maeneo hayo ambayo ni operesheni kuu nne za shirika letu. Mchango wa Sheikh Thani ni mfano wa ukarimu na utamaduni wa kiislamu na utatumika pia kupunguza adha kwa wakimbizi Asia, Mashariki ya Kati na Afrika.”

Kamishna Mkuu Grandi amekumbusha kuwa leo hii kuliko wakati wowote ule, suala la mshikamano ili kupunguza machungu yanayokabili mamilioni ya watu duniani kote ni muhimu zaidi.

“Naamini wakati umefika kwa dunia kutumia rasilimali zake na uwezo wake kushughulikia majanga duniani kote na waumini wa dini ya kiislamu watumie Zaka kama mbinu thabiti ya kufanya hivyo,”amesema Sheikh Thani Bin Abdullah

Mchango huu wa hivi karibuni zaidi utagawanywa katika maeneo manne. Fungu la kwanza litapelekwa Yemen kusaidia zaidi ya wakimbizi wa ndani 600,000, wakimbizi wanaorejea na jamii zinazowahifadhi kwa kuwapatia fedha ambazo zitawasaidia kujikimu mahitaji muhimu kama vile kodi ya pango, chakula, elimu na afya.

Fungu la pili litatumika kuwapatia fedha kila mwezi wakimbizi 143,000 wa syria ambao hivi sasa wanaishi maisha magumu nchini Lebanon, taifa ambalo hivi sasa linahifadhi idadi kubwa ya wakimbizi wa Syria ikilinganishwa na idadi ya wananchi wake.

UNHCR imesema fungu la nne litatumika kwenyeujenzi wa makazi ya wakimbizi wa Mynmar walioko Cox’s Bazar nchini Bangladesh na kwamba lengo ni kuona kuwa mazingira ya wakimbizi 84,000 wa kabila la rohingya ni bora.

Halikadhalika fungu la nne ni kwa ajili ya makazi, elimu na afya kwa wakimbizi 330,000 kutoka Sudan waliosaka hifadhi nchini Chad ambapo fedha zitapitishwa kwenye mfuo wa Sadaqah wa UNHCR huku zile za Yemen, Chad na Bangladesh zitapitishiwa mfuko wa Zakat wa UNHCR.

Mfuko wa Thani Bin Abdullah Bin Thani Al-Thani ulianzishwa kusaidia wakimbizi wa ndani na wale walio na uhitaji zaidi duniani kupitia UNHCR.