AV

UNHCR yaongeza hatua za kukabiliana na hali ya wakimbizi Sahel ghasia zikishika kasi

Get monthly
e-newsletter

UNHCR yaongeza hatua za kukabiliana na hali ya wakimbizi Sahel ghasia zikishika kasi

UN News
6 February 2020
By: 
Mwanamke aliyefurushwa Kaskazini mwa Mali ukanda wa Sahel akiwa katika makazi ya muda karibu na kituo cha basi Mopti
UNDP/Nicolas Meulders
Mwanamke aliyefurushwa Kaskazini mwa Mali ukanda wa Sahel akiwa katika makazi ya muda karibu na kituo cha basi Mopti

Kamishina Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR ameelezea hofu yake kuhusu kuzorota kwa kasi kwa hali ya kibinadamu kwenye ukanda wa Sahel ambako machafuko na kutokuwepo usalama kumewalazimisha maelfu ya watu kuzikimbia nyumba zao.

Akizungumza nchini Burkina Faso wakati wa kuhitimisha ziara kwenye mataifa matatu ya ukanda huo kamishina huyo Filippo Grandi amesema “Dharura iko hapa Sahel ambako watu wanakabiliwa na madhila makubwa, wanauawa, wanawake wanabakwa, Watoto hawawezi kwenda shule. Sahel ni mahali ambako ni lazima tuingilie kabla mgogoro huu haujawa zahma kubwa zaidi.”

Alipokutana na marais wa Burkina Faso, Niger na Mauritania bwana Grandi amezipongeza nchi hizo kwa kuendelea kukaribisha wakimbizi wakati zenyewe zinakabiliwa ba dharura ya kibinadamu kwa mfano Niger na Burkina Faso na kuongeza kwamba “Kwenye ukanda wa Sahel miongoni mwa nchi masikini kabisa duniani ndio zinazosalia kuwa zenye ukaribu zaidi "akishukuru ukarimu wa Niger, Mauritania na Burkina Faso ambazo zimepokea na kuhifadhi wakimbizi 165,000 waliokimbia machafuko Mali ambako hali ya usalama haina dalili yoyote ya kuimarika.

Bwana Grandi ameongeza kuwa “licha ya changamoto nyingi zinazozikabili nchi hizi tatu leo hii hatushuhudii ukarimu kama wao katika sehemu nyingi duniani.”Akipongeza pia mikakati yao ya suluhu ya muda mrefu kwa wakimbizi na watu waliolazimika kutawanywa kwa kuhakikisha utangamano miongoni mwa wakimbizi na wenyeji.

Idadi ya wakimbizi na wakimbizi wa ndani katika Sahel ya Kati inaendelea kuongezeka amesema Bwana Grandi na sasa imefikia zaidi ya milioni moja.

Grandi alipata fursa pia ya kukutana na baadho ya wakimbizi na wakimbizi wa ndani ambao anasema“Hadithi walizonisimulia Niger, Mauritania na Mali ni za kusikitisha na kutisha. Hadithi za watu lkuuawa na makundi yenye silaha hadithi za uharibifu wa nyumba, shule, vituo vya afya na hadithi za ukatili mkubwa dhidi ya wanawake.”

Hivyo amesema kwenye ukanda wa Sahel hatua za kukabiliana na mgogoro zisiwe za kiusalama pekee, ulinzi wa wale wanaolazimika kukimbia unasalia kuwa kipaumbele namba moja akitaka pia kuwe na uratibu mzuri baina ya raia na uongozi wa jeshi ili kuhakikisha fursa za kufikisha misaada ya haraka ya kibinadamu kunakohitajika.