AV

Tunawapatia wanawake DRC stadi za ujasiriamali -Private Anna

Get monthly
e-newsletter

Tunawapatia wanawake DRC stadi za ujasiriamali -Private Anna

UN News
1 June 2020
By: 
Walinda amani wanawake kutoka Tanzania katika mazungumzo na mwanamke mkazi wa Beni, nchini DRC
TANZABATT 7/Ibrahim Mayambua
Walinda amani wanawake kutoka Tanzania katika mazungumzo na mwanamke mkazi wa Beni, nchini DRC

Mlinda amani mwanamke kutoka Tanzaina ambaye anahudumu katika ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC, MONUSCO,amethibitisha umuhimu wa uwepo wa askari wa kike katika ulinzi wa amani katika taifa hilo lililogubikwa na mizozo.

Private Anna Malima Musa wa kikosi cha 7 cha TanzaniaTANZBATT 7,kwenye kikosi cha kujibu mashambulizi cha, FIB amesema hayo wakati huu ambapo dunia hii leo inasherehekea siku ya walinda amani ulimwenguni, maudhui yakiwa niwanawake walinda amani ni ufunguo wa amani ya kudumu.

Akizungumza kutoka makao makuu ya kikosi hicho huko Beni, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini nchini DRC, Private Anna amesema kuwa,“wanawake wana changamoto nyingi kama magonjwa na unakuta hawezi kumwelezea mwanaume. Unakuta mama ana magonjwa lakini hajui afanye nini kutokana na mazingira magumu na hana uwezo wa kwenda hospitali. Hivyo tukikutana nao tunawapa elimu ya jinsi ya kujikinga, hususan hili gonjwa laCOVID-19, tumewapa elimu ya kunawa mikono, kutumia vitakasa mikono, kutumia barakoa.”

Na akaenda mbali zaidi kuhusu msaada wao kwa wanawake wenye watoto lakini hawana njia ya kipato akisema,“unakuta ni mama hana mume, ila ana kundi la watoto, hivoy tunawapatia elimu ya kujishughulisha, mfano ushonaji, upandaji wa maua na anaweza kujishughulisha hata ufumaji na hatimaye akapata kipato cha kuweza kupeleka watoto shule.”

TANZBATT 7ina jumla ya wanajeshi 949 na miongoni mwao 63 ni askari wa kike.

Kikosi hicho cha Tanzania kinahudumu kwa mwaka mmoja na kinatarajia kukamilisha kazi yake mwezi Oktoba mwaka huu wa 2020.

Umoja wa Mataifa umeangazia walinda amani wanawake mwaka huu ikiwa ni miaka 20 tangu kupitishwa kwa azimio namba 1,3,2,5 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa tarehe 31 mwezi Oktoba mwaka 2000 likitaka mchakato wowote wa amani na usalama ikiwemo operesheni za ulinzi wa amani zijumuishe walinda amani wanawake.