AV

Shehena nyingine ya vifaa vya uchaguzi yawasili CAR

Get monthly
e-newsletter

Shehena nyingine ya vifaa vya uchaguzi yawasili CAR

UN News
18 June 2020
By: 
Mapokezi ya vifaa vya uchaguzi kwenye mji mkuu wa CAR, Bangui.
MINUSCA
Mapokezi ya vifaa vya uchaguzi kwenye mji mkuu wa CAR, Bangui.

Nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, shehena ya tatu ya vifaa vya uchaguzi imewasili katika mji mkuu wa nchi hiyo Bangui. Vifaa hivyo vimetolewa na Umoja wa Mataifa na wadau wake ukiwemo Muungano wa Ulaya, EU, na ni kwa ajili ya uchaguzi wa Rais na wabunge uliopangwa kufanyika nchini humo mwezi Desemba mwaka huu.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini CAR, , umesema kuwa shehena hiyo ya tani 32 inajumuisha kompyuta ndogo za kubeba kiganjani au Tablet, vifaa vya kuhifadhi chaji ya betri, paneli za sola pamoja na betri ambavyo vyote vitasaidia kazi ya uandikishaji wapiga kura inayoanza tarehe 22 mwezi huu wa Juni.

Katika uwanja wa ndege wa Bangui Mpoko, Waziri Mkuu wa CAR, Firmin Ngrebada akiwa na maafisa wa serikali na Naibu Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini humo, Denise Brown, walishuhudia kuwasili kwa vifaa hivyo.

Akizungumzia mchakato wa maandalizi, Bwana Ngrebada amesema kuwa,“unaendelea vizuri na kwamba ramani ya upigaji kura imeshakamilishwa, vituo vya kujiandikisha nchini kote, mafunzo kwa wakufunzi ambao watafundisha wasimamizi wa vituo vingine na hatua inayobakia sasa ni uandikishaji na utambuaij wa wapiga kura.”

Maandalizi ya uandikishaji wa wapiga kura CAR yanaendelea licha ya kuenea kwa ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19 nchini humo ambapo Denise Brown ambaye pia ni Naibu Mkuu wa MINUSCA anasema kuwa,“sisemi kwamba ni rahisi, tulikuwa na mgeni ambaye niCOVID-19, lakini kwa ushirikiano na serikali, shirika la afya la Umoja wa Mataifa, , na Waziri wa Afya, tunapambana na kuenea kwa virusi na tunashawishika kuwa kwa azma ya serikali, kwa msaada wa MINUSCA, UNDP na mfumo mzima wa Umoja wa Mataifa, tutafika kama ilivyopangwa.”

Vifaa hivi ni nyongeza ya shehena nyingine ya tani 69 iliyowasili nchini CAR mwezi uliopita ikijumuisha fomu na vikasha vingine vya uchaguzi.

MINUSCA inasema kuwa itaendelea kufanya kazi kwa ushirikiano na wadauwa kitaifa ili kupatia taifa hilo msaada uwe wa vifaa na usambazaji, usalama na kufanikisha mijadala ya kisiasa ili uchaguzi uwe huru, shirikishi na wa amani na hatimaye kuimarisha demokrasia na amani ya kudumu CAR.

Pamoja na vifaa vya uchaguzi, MINUSCA katika harakati za kusaidia taifa hilo kukabili COVID-19, imesambaza barokoa, vikasha vya huduma za kujisafi, sabuni kwa jamii za Bangassou jimboni Mbomou.