AV

Sayansi kwa vitendo ni ‘tamu’ kuliko kuelezewa -Mwanafunzi

Get monthly
e-newsletter

Sayansi kwa vitendo ni ‘tamu’ kuliko kuelezewa -Mwanafunzi

UN News
3 June 2020
By: 
Kutokana na janga la Corona lililosababisha shule kufungwa, nchini Tanzania wabunifu MITZ Group wamebuni kifaa cha kuwezesha wanafunzi (pichani) kufanya mafunzo ya sayansi kwa vitendo wakiwa nyumbani bila mwalimu.
UN Tanzania
Kutokana na janga la Corona lililosababisha shule kufungwa, nchini Tanzania wabunifu MITZ Group wamebuni kifaa cha kuwezesha wanafunzi (pichani) kufanya mafunzo ya sayansi kwa vitendo wakiwa nyumbani bila mwalimu.

Nchini Tanzania, wanufaika wa kifaa maalumu cha kujifunza sayansi kwa vitendo pasi na uwepo wa Mwalimu kilichobuniwa na vijana wanane kutoka jijini Mwanza nchini humo, wamezungumzia jinsi ambavyo kinawasaidia.

Miongoni mwa watumiaji wa kifaa hicho chenye mwongozo wa kitabu ni mwanafunzi Wilhelmina Richard kutoka mjini Mwanza ambaye anasema kuwa, “tulivyokuwa tunafundishwa Sayansi, sikufahamu hivi vitu kwa uhalisia. Kwa hiyo nilivyoona matangazo yake nikamwambia mama aninunulie. Nilikuwa sifahamu resista au kapasita inafanananje. Kusoma Sayansi kwa vitendo ni tamu na inafurahisha. Ukiwa unafanya kwa vitendo unaelewa vitu vingi kuliko tu kuelezewa. Unajua vitu vingi na kwa hiyo sasa hivi sikariri bali naelewa."

Kevin Paulambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa kikundi hiki kijulikanacho kama MITZ Group anadadavua kwa kina namna ambavyo mwanafunzi anaweza kujifunza akisema kuwa, “kifungasho kizima kinatoa maelezo kutoka kitabu halisi, kwa mfano kutoka kitabu cha fizikia kidato cha pili, kuna jaribio la kuchaji au kuondoa chaji katika kifaa kiitwacho kapasita, ni jaribio ambalo linaweza kumrahisishia mwanafunzi kuelewa ni jinsi gani taa ya kamera inafanya kazi. Kwa hiyo kutoka kwenye kitabu halisi anaangalia maelezo na akija kwenye kitabu chetu cha mwongozo kinamwelezea jinsi ya kufanya na namna gani unaanza hadi kumaliza. Anachukua kitu kimoja kimoja na kuunganisha kwa mujibu wa maelezo. Mchoro unatakiwa uendane na alichokitengeneza yeye na mwisoni akipata muunganisho wote vizuri, inatakiwa kapasita iwashe taa yenyewe bila kuwa na betri, na halafu taa ile itawaka kwa muda fulani na kisha itafifia kuonesha kuwa kapasita imemaliza chaji yake na ndivyo taa ya kwenye kamera inavyofanya kazi.”

Ameenda mbali akisema kuwa, “hicho hakiishii hapo, akifanya hivyo tumempatia kifaa zaidi ya kimoja, ili aweze kufanya jaribio zaidi ili kwa kubadilisha kifaa ili hatimaye aweze kuchambua kisayansi athari za kila kitu kimoja kimoja.”

Bwana Kelvin anasema aghalabu kwa muongozo wa kitabu hiki maalum na karatasi ya kazi mwanafunzi ataweza kuelewa kinagaubaga somo la sayansi pasi na shaka akisema kuwa, “na pia tunahamasisha mwanafunzi awe na ainisho lake mwenyewe la kile alichofanya na ndio maana tumeweka nafasi ndani za kujaza na kuchora jedwali ndani la kujaza ainisho la zoezi lake kwa vitendo na hii itamsaidia kujenga uwezo wa kuelewa somo la sayansi kwa ujumla.”