AV

Nyenzo mpya ya kidijitali yatumika kudhibiti nzige Somaliland -FAO

Get monthly
e-newsletter

Nyenzo mpya ya kidijitali yatumika kudhibiti nzige Somaliland -FAO

UN News
19 March 2020
By: 
Kundi la nzige kwenye eneo moja la shamba huko eneo la Salal, Somaliland
FAO
Kundi la nzige kwenye eneo moja la shamba huko eneo la Salal, Somaliland

Shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO kwa kushirikiana na serikali ya Somaliland wanatumia nyenzo mpya ya kidijitali eLocust3 kukabiliana na wimbi la nzige.

Katika eneo la kilimo la Luhaye nje kidogo ya mji wa Garissa Somaliland wataalam wana wale wa kilimo kutoka serikali ya Somaliland wakiendelea na harakati za kudhibiti nzige kwa kupizia dawa.

Lakini ili kuhakikisha nzige hao wanatokomea kabisa wataalam hao sasa wanasema wanatumia pia nyenzo mpya ya kidijitali ili kuongeza uwezo wa kukabili wadudu hao hatari.

Timu ya wataalam hao inaongozwa na Mohamed Mohamoud mkurugenzi wa idara ya ulinzi wa misitu kwenye wizara ya kilimo ya Somaliland ambaye ndiye anayesimamia ufuatiliaji wa nzige hao kupitia teknolojia ya eLocust3 inayoweza kutoa taarifa kwa wakati katika vita hivyo dhidi ya nzige anasema,“Tunapenda kutumia madawa haya kwa ajili ya usalama wa Wanyama, tuna mifugo mingi sana hapa Somaliland na pia dawa hizi ni Rafiki kwa mazingira na salama kwa binadamu katika jamii hii na wataalamu wanaozipulizia”

Na kuhusu teknolojia ya ufuatiliaji wa nzige hao amesema,“Tableti hii ni muhimu sana kwa sababu nadhani inafanyakazi kwa satilaiti na unapotuma ripoti inaonyesha muda gani, na lini uliendesha utafiti na taarifa zinakwenda moja kwa moja Roma kwa FAO na kwenye ofisi ya kanda inayohusika na nzige, hivyo ni ya muhimu sana na ina taarifa zingine pia kuhusu nzige hawa wa jangwani.”

FAO hivi sasa inachangisha fedha ili kuongeza uwezo wa wizara hiyo ya kilimo wa kuweza kukabiliana nzige hao endapo wimbi jipya litazuka.