AV

Ndoto ya mkimbizi wa Syria kuwa fundi umeme yatimia huko Ujerumani

Get monthly
e-newsletter

Ndoto ya mkimbizi wa Syria kuwa fundi umeme yatimia huko Ujerumani

UN News
4 June 2020
By: 
Mkimbizi kutoka syria Mohammad Alkhalaf akiwa kwenye chumba cha dereva kwenye treni huko Hamburg nchini Ujerumani ambako amepata fursa ya uanagenzi.
UNHCR/Gordon Welters
Mkimbizi kutoka syria Mohammad Alkhalaf akiwa kwenye chumba cha dereva kwenye treni huko Hamburg nchini Ujerumani ambako amepata fursa ya uanagenzi.

Hatimaye ndoto za mkimbizi kutoka Syria za kutaka kutumia ujuzi wake katika hisabati na fizikia zimetimia huko Ujerumani baada ya kupata kazi katika kampuni ambamo kwayo anatumia stadi zake.

Mkimbizi huyo Mohammad Alkalaf kutoka Syria ametizima ndoto yake baada ya kuajiriwa nafasi ya uanagenzi na kampuni ya rei ya Ujerumani.

Kupitia video ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, , Mohammad anasema kuwa “nilikua nikisaidia kilimo cha mizeituni katika shamba la familia huko Idblib, kaskazini-magharibi mwa Syria. Lakini nilikuwa na ujuzi mkubwa katika hisabati na fizikia na nilitambua kuwa nitaweza kufanya kazi katika kampuni za teknolojia kwa hiyo baada ya kuhitimu sekondari ya juu nilitumai kuwa nitasonga mbele zaidi.”

Hata hivyo vita vilipoibuka Syria ndoto alianza kuyoyoma na alikimbia nchi hiyo mwaka 2014 akitumai kuungana na kaka yake nchini Sweden. “Hilo halikuwezekana, lakini mwaka 2017 nikapatiwa hifadhi Ujerumani,” anasema Mohammad.

Akiwa Ujerumani, Mohammad amejifunza kijerumani na alitamani sana kuwa fundi umeme na alituma maombi 200 ya kazi. Kwa bahati Mohammad anasema, “niliona tangazo la Chance Plus, mfumo wa kufanya mtihani ili uweze kujiunga na kampuni ya Deutsche Bahn inayoandaa wafanyakazi wapya kupata fursa ya uanagenzi. Mfumo huu unatoa nafasi kwa waombaji 300 kila mwaka Ujerumani kote.”

Mohammad anasema kuwa anachopenda kuhusu ufundi umeme ni kwamba tasnia hiyo ina kanuni nyingi na wanapaswa kuwa salama akisema kuwa, “nadhani madaktari na mafundi umeme hawapaswi kufanya makossa kwa sababu uhai unategemea kutenda kwako kitu sahihi.”

Ulrike Stods ambaye ni mkuu wa mradi wa Chance Plus katika kampuni ya Deutsche Bahn anasema kuwa, “hapa Ujerumani sifa nav yeti ni muhimu sana kwa mtu kuweza kujumuishwa kwenye soko la ajira. Ndio maana ni muhimu kuwezesha kundi hili kupitia njia ya kawaida ya kupata hizi sifa na tunataka kuwasaidia kadri tunavyoweza.”

Ili aweze kuhitimu kazi ya ufundi umeme, Mohammad anajifunza stadi mbalimbali kuanzia kufunga na kudhibiti programu za kompyuta na miaka miwili tangu aanza mafunzo hayo tayari anaweza kukagua na kurekebisha treni akisema kuwa, “mimi ni mtu ambaye kila wakati nataka kufanya kazi yangu kwa ubora, na kila wakati najifunza kutokana namakosa na najaribu kujiendeleza zaidi.”

Kwa Mohammad mwenye umri wa miaka 28, kupata ajira ni muhimu kwa kuwa wanajaribu kuishi maisha mapya ugenini wakati huu ambapo sekta nyingi nchini Ujerumnai zimefungua fursa kwa wakimbizi huku zikiziba pengo la soko la ajira kama anavyosema Ulrike Stodt mkuu wa mradi wa Chance kwenye kampuni ya Deutsche Bahn.

“Tungependa kuhamasisha kampuni nyingine ziangalie wakimbizi na ziwapatie mafunzo na kuwajumuisha kwenye ajira. Tumekuwa na uzoefu mzuri sana na tumechukua wafanyakaiz wapya na ni inalipa,” amesema Bi. Stodt.

Mohammad ana uhakika kuwa iwapo atafaulu mtiani wake atapata kazi Deutsche Bahn na atakuwa na uwezo wa kuendeleza ndoto yake ya ufundi umeme, “mwanzoni nilipoteza matumaini. Sikuweza kufikiria chochote kuhusu maisha yangu ya baadaye kwa sababu ya vita nchini Syria. Sasa niko kwenye uanagenzi na nina uhakika wa ajira. Sasa ninaweza tena kufikiria mustakhbali wangu na nina matumaini zaidi.”