AV

Mlipuko mpya wa Ebola wagundulika kaskazini magharibi mwa DRC, WHO yapeleka timu kusaidia

Get monthly
e-newsletter

Mlipuko mpya wa Ebola wagundulika kaskazini magharibi mwa DRC, WHO yapeleka timu kusaidia

UN News
2 June 2020
By: 
Maafisa wa WHO wakiandaa chanjo ya Ebola huko Butembo DRC.
WHO/Lindsay Mackenzie
Maafisa wa WHO wakiandaa chanjo ya Ebola huko Butembo DRC.

Taarifa iliyotolewa hii leo tarehe mosi ya mwezi Juni, na shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO mjini Geneva Uswisi, Brazzaville Jamhuri ya Congo na Kinshasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, imeeleza kuwa serikali ya DRC imetangaza leo hii kuwa mlipuko mpya wa ugonjwa wa Ebola unaendelea katika aneo la Wangata huko Mbandaka katika jimbo la Équateur.

Tangazo hilo linakuja wakati mlipuko wa muda mrefu na mgumu wa Ebola mashariki mwa DRC ukiwa katika hatua ya mwisho wakati nchi hiyo pia ikipambana na COVID-19 na mlipuko mkubwa zaidi wa ugonjwa surua duniani. Taarifa za awali kutoka katika Wizara ya afya ya DRC ni kuwa wagonjwa sita wa Ebola kufikia sasa wamegundulika katika eneo hilo la Wangata ambapo wanne wamefariki dunia na wawili wako hai katika uangalizi. Watu watatu kati ya hao sita wamethibitishwa na vipimo vya maabara.

Inawezekana watu wengi zaidi wenye maambukizi watatambuliwa wakati ambapo uchunguzi unaendelea, imeeleza taarifa ya . Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus amenukuliwa akisema, “hii ni ukumbusho kuwa COVID-19 siyo hatari pekee ya kiafya ambayo watu wanakabiliana nayo. Ingawa tumejielekeza zaidi kwa mlipuko, WHO inaendelea kufuatilia na kushughulikia dharua nyingine nyingi za kiafya.”

Huu ni mlipuko wa 11 wa Ebola kwa DRC tangu kugundulika kwa mara ya kwanza kwa virusi hivyo vya Ebola nchini humo mnamo mwaka 1976. Jiji la Mbandaka na maeneo jirani yalikuwa maeneo ya mlipuko wa tisa wa virusi vya Ebola ambao ulitokea mwezi Julai mwaka 2018.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika, amesema, “hii inatokea katika nyakati za changamoto, lakini WHO imefanya kazi kwa miaka miwili iliyopita kwa kushirikiana na mamlaka za afya, CDC Afrika na wadau wengine kuimarisha uwezo wa kitaifa kushughulikia mlipuko. Kuimarisha uongozi wa kitaifa, WHO inapanga kutuma timu ya kusaidia katika kuongeza mapambano. Kutokana na mlipuko wa sasa kwa njia za usafiri na n chi jirani zilizoko hatarini, tunapaswa kuchukua hatua haraka.”

WHO tayari iko Mbandaka kusaidia mapambano dhidi ya Ebola kama sehemu ya mlipuko wa mwaka 2018. Timu ilikuwepo kusaidia kukusanya na kuzipima sampuli na kufuatilia wagonjwa.

Kazi inaendelea kutuma vifaa zaidi Kivu Kaskazini na pia kutoka Kinshasa ili kusaidia juhudi zinazoongozwa na serikali. Timu ya watu 25 kutoka WHO inategemewa kutumwa kuongeza nguvu.

Mlipuko wa 10 wa Ebola Kaivu Kaskazini, Kusini na Ituri uko katika hatua zake za mwisho na tarehe 14 ya mwezi Mei mwaka huu 2020, Wizara ya afya ilianza kuhesabu siku 42 kuelekea kumalizika kwa mlipuko wa Ebola nchini DRC.