AV

MINUSCA yabisha hodi magerezani CAR

Get monthly
e-newsletter

MINUSCA yabisha hodi magerezani CAR

UN News
19 June 2020
By: 
Gereza Kuu la Ngaragba nchini CAR limepokea vifaa vya kujikinga na COVID-19 kutoka MINUSCA na UNDP.
MINUSCA
Gereza Kuu la Ngaragba nchini CAR limepokea vifaa vya kujikinga na COVID-19 kutoka MINUSCA na UNDP.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, MINUSCA na shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNDP wamepatia gereza kuula Ngaragba msaada wa vifaa vya kusaidia kuepusha kuenea kwa ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19 gerezani humo.

Vifaa hivyo ni pamoja na barakoa, vifaa vya kujisafi vikiwalenga wafungwa na wafanyakazi.

Msimamizi wa gereza hilo Joël Hubert Yandome, akizungumza baada ya kupokea msaada huo amesema,“tunafurahia sana kupokea msaada huu. Huu ugonjwa hauna mipaka. Wafungwa na wafanyakazi wa gereza wanaweza kuambukizwa. Wafungwa wanaweza kufa kwa COVID-19. Tunafurahia sana kitendo hiki cha kikarimu kutoka kwa wadau wetu.”

Kwa kutumia vifaa hivyo, wafungwa na wafanyakazi wanaweza kujikinga na ugonjwa huo hatari ambao hadi sasa katika taifa hilo la Jamhuri ya Afrika ya Kati kuna wagonjwa 2,410 waliothibitishwa na kati yao hao 14 wamefariki dunia.

Leila Ben Othman ambaye ni mkuu wa kitengo cha masuala ya magereza, amesema kuwa,“hii ni awamu ya kwanza, magereza yote 12 nchini CAR yatapatiwa msaada wa aina mbalimbali ya vifaa vya kinga na vya kujisafi.”

Gharama ya msaada huo ni dola 120,000 na kuna glovu, dawa za kupuliza, barakoa, vipima joto vinavyotumia mionzi, sabuni, dawa za kutakasisha mikono na magauni ya kujikinga.

MINUSCA pamoja na kusaidia kuimarisha ulinzi wa raia, inasaidia pia masuala ya mchakato wa uchaguzi na masuala ya kibinadamu na kijamii.