AV

Mashambulizi ya ADF nchini DRC yanaweza kuwa uhalifu wa vita na dhidi ya ubinadamu -UN

Get monthly
e-newsletter

Mashambulizi ya ADF nchini DRC yanaweza kuwa uhalifu wa vita na dhidi ya ubinadamu -UN

UN News
7 July 2020
By: 
Raia waliofurushwa na mashambulizi ya LRA
UN Photo/Tim McKulka
Raia waliofurushwa na mashambulizi ya LRA

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imeonya kwamba mashambulizi yanayofanywa na kundi la wapiganaji la ADF Mashariki wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, yanaweza kuwa ni uhalifu wa vita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Kwa mujibu wa ripoti ya ofisi hiyo ya haki za binadamu iliyotolewa leo mjini Geneva Uswis mashambulizi ya kundi hilo dhidi ya raia yameshika kasi katika miezi 18 iliyopita na kupanua wigo wake hata katika maeneo ambayo hapo awali hawakuwepo.

Mashambulio hayo hadi sasa yameshakatili maisha ya watu zaidi ya 1,000, maelfu wengine kujeruhiwa, hivyo uchunguzi wa Umoja wa Mataifa umebaini kwamba mauaji hayo yanaweza kuwa uhalifu wa vita na dhidi ya ubinadamu.

Kwa zaidi ya miongo mitatu kundi la ADF limekuwa likiendesha operesheni zake za kijeshi katika eneo la Beni jimboni Kivu Kaskazini , lakini kufuatia operesheni za kijeshi za kulifurusha kundi hilo wapiganaji wake baadhi wamekimbilia maeneo mengine ikiwemo jimbo la Ituri ambako mashambulizi dhidi ya raia sasa yameshika kasi ikiwemo mauaji ya kutumia silaha kama AK47, magruneti lakini pia mapanga na visu.

Pia wapigani hao wamechoma vijiji, kusambaratisha vituo vya afya na shule na kuteka watu wakiwemo wanawake, wanaumme na watoto na kuwashinikiza kuingia jeshini kushiriki vita.

Ripoti hiyo imesema “Katika asilimia kubwa ya matukio haya njia na mwenendo wa mashambulizi unaonyesha bayana lengo la kuhakikisha hakuna anayesalimika. Familia nzima zimekuwa zikishambuliwa hadi kufa.”

Na kuongeza kwamba kusambaa kwa mashambulizi hayo na mfumo wa ushambuliajidhidi ya raia unafanya baadhi ya ukiukwaji huo wa haki za binadamu kuweza kuwa uhalifu wa vita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyoandaliwa na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (UNJHRO), tangu tarehe Mosi Januari 2019 hadi tarehe 30 Juni 2020 raia 1,066 wameuawa, 176 kujeruhiwa na 717 kutekwa na kundi la ADF kwenye majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri.

Katika kipindi hichohicho pia watoto 59 waliingizwa jeshini, shule moja, kituo cha afya na nyumba za raia zilishambuliwa, vitu kuporwa na kusababisha melfu ya watu kutawanywa.

Mada: