AV

Kutana na Sajini Desta anayesifika kwa kutengeneza magari ya UNMISS, Sudan Kusini

Get monthly
e-newsletter

Kutana na Sajini Desta anayesifika kwa kutengeneza magari ya UNMISS, Sudan Kusini

UN News
1 June 2020
By: 
Almaz Kabtimer Desta, Sajenti raia wa Ethiopia anayefanya kazi katika Mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNIMISS akihudumu kama fundi makenika
UNMISS
Almaz Kabtimer Desta, Sajenti raia wa Ethiopia anayefanya kazi katika Mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNIMISS akihudumu kama fundi makenika

Wanawake wanaohudumu katika shughuli mbalimbali za Umoja wa Mataifa kote duniani wanaendelea kujizolea umaarufu kutokana na uchapakazi wao. Mmoja wao ni Almaz Kabtimer Desta, Sajenti anayefanya kazi katika Mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNIMISS akihudumu kama fundi makenika.

Sajini Almaz Kabtimer Desta ni raia wa Ethiopia ambako alijiunga na jeshi miaka sita iliyopita baada ya kukamilisha kozi yake ya miaka miwili kuhusu ufundi wa magari. Hapa ni mjini Yambio, katika jimbo la Equatoria Magharibi nchini Sudan Kusini, analala chini ya gari kurekebisha hitilafu ili shughuli za walinda amani waziendelee. Askari huyu wa kike anakarabati kwa wastani gari nne kwa siku moja na anasema hii ndiyo kazi anayoipenda,

"nilijiunga na jeshi kwa sababu ni taaluma ya heshima mbayo mara zote nilitaka kuifanya. Ufundi wa magari ndio ninaoufurahia,kuyafanya magari yaendelee kufanya kazi.”

Akiwa ni mmoja wa walinda amani wanawake 47 waliotumwa kutoka Ethiopia kuja kuhudumu mjini Yambio, Desta anasema anashukuru kwa fursa hii ya kufanya kazi kama mlinda amani wa Umoja wa Mataifa. Askari huyu anafurahi pia namna watu wa Sudan wanavyompenda,

“Inagusa sana moyo kutambua jinsi Sudan Kusini ilivyo nzuri na watu wake. Wananitendea kama rafiki yako, binti yao na familia yao. Ninajihisi kama nyumba yangu ya pili.Inatia moyo kuwaona wananichukulia kama mfano wao wa kuigwa kwa kuwa ni mlinda amani na fundi wa kike ninayefanya kazi zangu na wafanyakazi wenzangu wa kiume.”

Ingawa Sajini Desta ni mlinda amani anayejitolea kwa dhati, anakiri kwamba kuwa mbali na familia na wapendwa wake, haswa wakati wa janga laCOVID-19, ni ngumu.

“Kuwa mbali na familia katika janga la afya duniani kote, inaogofya. Katika mawasiliano yangu ya kila siku na familia yangu huko nyumbani, kama Facebook, ninawaeleza kuhusu wanachotokakiwa kufanya ili kujikinga na kubakia salama dhidi ya janga.”

Pamoja na ugumu na kujitolea ambavyo walinda amani wanapaswa kuwa navyo, Sajini Desta anaipendekeza kazi hii kama chaguo la kazi kwa wanawake wa umri mdogo kote duniani.

“Ninawashauri wanawake wenzangu kujilinda na ndoa za mapema. Pia ninapenda kuwashauri wanawake wote kuchagua sekta hii, ambayo bado imehodhiwa na wanaume. Tunaweza na tunapaswa kuonesha usawa wetu na tufurahie umakenika kama hilo ndilo linalotuvutia.”

Wakati ulinzi wa amani ukiendelea kubadilika, walinda amani wa kike kama Sajini Desta, wanategemewa kuchukua jukumu kubwa zaidi ndani ya jamii wanayoitumikia.