AV

Kenya yaibuka kidedea ujumbe Baraza la Usalama la UN

Get monthly
e-newsletter

Kenya yaibuka kidedea ujumbe Baraza la Usalama la UN

UN News
22 June 2020
By: 
Upigaji kura katika uchaguzi wa mjumbe asiye wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Uchaguzi umefanyika kwenye makao makuu ya UN, New York, Marekani
UN/Eskinder Debebe
Upigaji kura katika uchaguzi wa mjumbe asiye wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Uchaguzi umefanyika kwenye makao makuu ya UN, New York, Marekani

Hatimaye Kenya imeibuka mshindi katika kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya ujumbe usio wa kudumu katika Baraza la Usalama la baada ya kuishinda Djibouti.

Uchaguzi huo umefanyika leo ikiwa ni duru ya pili baada ya hapo jana nchi mbili hizo kutoka kundi la Afrika na Asia-Pasifiki kushindwa kupata kura za kutosha za theluthi mbili, India pekee ikijaza kiti kimoja.

Katika uchaguzi wa leo uliofanyika katika mazingira ya kuepusha kuchangamana na wawakilishi wa nchi 192 wanachama wa Umoja wa Mataifa wakiwa wamevalia barakoa, Kenya imepata kura 129 huku Djibouti ikiambulia kura 62 huku kura 1 ikiharibika.

Katika barua yake kwa wawakilishi wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Profesa Tijjani Muhammad Bande amesema kuwa, “baada ya kupata theluthi mbili ya kura zinazohitajika kutoka kwa wapiga kura na kura zilizopigwa, Kenya imechaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kipind icha miaka miwili kuanzia tarehe 1 Januari mwaka 2021. Naipongeza Kenya kwa kuchaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Usalama.”

Profesa Muhammad-Bande pia ameshukuru wahesabu kura na wafanyakazi wa Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa kwa msaada wao wakati wa upigaji kura hii leo, akiongeza kuwa, “Baraza Kuu litatambua matokeo ya uchaguzi huu katika kikao chake cha kwanza cha wawi kitakachofanyika baada ya ukomo wa mazingira ya sasa ya COVID-19.”

Uchaguzi wa wajumbe wa Baraza la Usalama kwa mwaka huu ulikuwa unafanyika kujaza nafasi 5 za wajumbe wanaomaliza muda wao tarehe 31 mwezi Desemba mwaka huu.

Nchi zilizojaza nafasi hizo ni Kenya na India kutoka kundi la Afrika na Asia-Pasikifi, Norway na Ireland kutoka kundi la Ulaya Magharibi na makundi mengine, na Mexico kutoka kundi la Amerika ya Kusini na Karibea ambayo haikuwa na mpinzani.

Canada ilibwagwa katika kundi la Ulaya Magharibi na makundi mengineyo.

Wajumbe wanaomaliza muda wao ni mwisho wa mwaka huu ni Ubelgiji, Jamhuri ya Dominika, Ujerumani, Indonesia na Afrika Kusini.