AV

Huu sio wakati wa mashaka au kusita-Paul Kagame

Get monthly
e-newsletter

Huu sio wakati wa mashaka au kusita-Paul Kagame

UN News
23 September 2020
By: 
Paul Kagame
UN Photo/Cia Pak
Rais Paul Kagame wa Jamhuri ya Rwanda akihutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani tarehe 24 Septemba 2019. Mwaka huu wa 2020 Kagame amehutubia kwa njia ya video iliyorekodiwa kwasababu ya janga la COVID-19 duniani.

Rais wa Rwanda Paul Kagame akihutubia mjadala wa wazi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA 75 kwa njia ya video iliyorekodiwa amesema, huu si wakati wa mashaka au kusita pamoja na kuwa COVID-19 imesababisha matatizo makubwa kama vile vifo vya watu vinavyokaribia milioni moja.

Rais Kagame amesema pia kuwa janga hili la virusi vya corona sit u vimeishia katika kusababisha vifo bali pia vimewasukuma wengi katika ugumu usiotarajiwa, lakini kwa vyovyote,“tutashinda jaribio hili, kwani tunazo zana za kutamalaki katika afya, usawa wa kijinsia, mazingira, maendeleo endelevu, ujumuishaji wa kidijitali, na haki ya rangi zote. Inahusu maadili mazuri tunayowekeza katika taasisi zetu.”

Aidha Rais Kagame ameeleza kuwa dunia mwaka huu pia inaadhimisha miaka 25 tangu kufanyika kwa mkutano wa kimataifa wa wanawake, Beijing ambao uliweka ajenda ya mabadiliko juu ya usawa wa kijinsia ambayo inaendelea kuwaongoza watu wa ulimwengu.

“Uwezeshaji wa wanawake umetufanya sisi sote kuwa salama na wenye afya lakini usawa wa kijinsia bado haujapatikana katika nchi yoyote.” Amefafanua Bwana Kagame.

Kwa upande wa mabadiliko ya tabianchi

Kuhusu mabadiliko ya tabianchi, Rais Kagame amekumbushia kuwa miaka mitano iliyopita, makubaliano ya Paris kuhusu mabadiliko ya tabia nchi yalitiwa saini na kwa hivyo,“utekelezaji wa mfumo huu, kutapunguza kasi ya ongezeko la joto duniani na kuupa nafasi uchumi wetu muda wa kuenenda sawa na teknolojia mpya.”

Malengo ya maendeleo endelevu

Akizungumzia malengo ya maendeleo endelevu yaani SDGs, Bwana Kagame amesema imesalia miaka 10 kufikia mwaka 2030 kufikia kilele cha kuwa malengo hayo yamefikiwa lakini,“hebu na tusijidanganye kuhusu namna ambavyo itakuwa vigumu kuyafikia malengo katika muda uliopangwa. Nchi nyingi hususani katika Afrika zilikuwa tayari nje ya mstari kabla ya mwaka 2020. Janga la virusi vya corona vimevuruga ukuaji na ukusanyaji mapato duniani na pengine katika miaka kadhaa ijayo.”

Pia Paul Kagame amepongeza jitihada za shirika la afya la Umoja wa Mataifachini ya uongozi wa Dkt Tedros Ghebreyesus na akaahidi kuwa wataendelea kuimarisha WHO ili ifanye kazi zaidi kwa ufanisi.

“Ugonjwa huu umetuonesha umuhimu wa mfumo wa afya wa umma ulio imara.”Amesisitiza Bwana Kagame.

UNGA75, Paul Kagame, Rwanda

Mada: